Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye wizara hii. Kwanza ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha michezo ya Tanzania. Wote tumeshuhudia goli la mama, jinsi gani Mheshimiwa Rais alikuwa anazihamasisha timu zetu katika kuwapa motisha washilingi kadhaa katika timu zetu ili wale wachezaji wetu wapate morale ya kuweza kuwakilisha nchi yetu. Hayo tumeyaona matunda yake, tumeona matunda yake kwa timu za Yanga na Simba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo niwapongeze timu ya Simba kwa kuingia fainali katika Kombe kubwa la Shirikisho. Pia niwapongeze timu ya Yanga kwa hatua waliyofikia. Asiyekubali ushindi si mshindani. Yanga imejikubali, sasa kwa pamoja tuungane twendeni tukawaunge mkono wenzetu Watanzania wenzetu wana Simba Sports Club warudi hapa na kombe hili la shirikisho. Huo ndio uzalendo na ndio Utanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nimpongeze Mheshimiwa Waziri Profesa Kabudi, Naibu Waziri na Katibu wake Mkuu Msigwa, amefanya kazi kubwa sana Katibu Mkuu huyo, hakuna sehemu ambayo hakanyagi. Mheshimiwa Waziri amefanya kazi kubwa sana sana sana sana; lakini Naibu Waziri. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuweka ile timu pale, kuna mzee mmoja na kijana mmoja; timu kali kweli kweli. Ukiunganisha maarifa yale ya kijana na ya yule mzee pale Profesa basi nina imani mambo yanaenda vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mimi utajikita katika Wilaya yangu ya Temeke. Wilaya ya Temeke ilipata fursa kubwa ya kupata Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru. Uwanja ule wa Uhuru ndio uwanja ambao mwaka 1961 Uhuru wa Tanzania ulipatikana katika Uwanja ule wa Uhuru. Ni uwanja wenye kumbukumbu kubwa na wenye historia kubwa ya uhuru ambao upo Temeke. Kama haitoshi niishukuru Serikali wameweza kujenga tena uwanja mkubwa kuupanua Uwanja wa Mkapa. Huko kwa Mkapa kwa kweli ni uwanja mkubwa na upo katika Wilaya ya Temeke. Hiyo kwa wana Temeke na kwa Watanzania ni tunu kubwa sana kwetu, ni tunu ya wana Temeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu; niombe sasa, kulikuwa na mashindano ya UMITASHUMTA, UMISHUMTA na michezo mingine mingi tu, Uwanja wa Uhuru ulikuwa unachachuka kwa michezo hiyo na michezo mingine ya kijeshi; lakini sasa naona hivyo vitu havipatikani, kwa nini, kumetokea nini? Ile michezo ilipokuwa inakuja pale kwenye Uwanja wa Uhuru kama ile michezo ya vijana, wanafunzi wanatoka katika mikoa mbalimbali wanakuja pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Dar es Salaam kuwa jiji, tumepewa ni jiji la kiuchumi bado na sisi ni mkoa kama mkoa mwingine. Tunaomba yale mashindano yaje. Wakati mashindano yale yanakuja pale sisi kama Wanatemeke ndiyo faida yetu, Wajasiriamali, mama lishe na wale wauza vinywaji; wote wanaozunguka kwenye uwanja ule na wengine wote wanaotoka pembezoni kote kwa Dar es Salaam wanafaidika na ile biashara; ndiyo sababu uwanja ule ukawa ni tunu na ni faida kwa Wanatemeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna lile gawio ambalo kama michezo inachezwa pale, wanacheza timu kubwa kubwa na mapato yanapatikana kwa wingi, gawio lile linatakiwa liletwe pale kwenye Halmashauri ya Temeke ili tuangalie nini tunataka kufanya kwa wakati huo. Hata hivyo, utakuta hilo gawio linakwenda maeneo maeneo tu. Sasa sisi faida yetu pale kama Wanatemeke ni nini? Kufagia takataka? Haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima niombe Serikali, kwamba ipange utaratibu maalum wa kuhakikisha kwamba kile kidogo kitakachopatikana katika michezo ile basi na Wanatemeke nao wapate walau kidogo, angalau kuboresha kwenye huduma za jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale michezo ikichezwa ikitokea mmoja ameumia atakimbizwa Hospitali ya Temeke, akitokea mwingine ameumia atakimbizwa muhimbili. Basi waangalie namna watakavyokwenda kusaidia angalau kitengo cha mifupa pale Temeke au kitengo cha mifupa kile cha Moi; angalau kukiongezea vitu yaani changamoto zao kidogokidogo ili na sisi tuone tumefaidika kutokana na mechi zinazoendeshwa katika uwanja wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiungana na mwenzangu kwenye Kiswahili, hapa yeye amezungumzia lahaja za Kiswahili, mimi nitazungumzia ushairi wa Kiswahili. Wapo washairi na wapo walioienzi lugha hii ya Kiswahili kwa kutunga mashahiri, kama marehemu Shaban Robert. Sisi wazee wa zamani tumemsoma vizuri sana Shabani Robert kwenye mashairi yake yule “Amina umejitenga, kufa umetangulia. Ile hali kama huwa umeifumba baada ya kuchanua, nakuombea kwa mola mema kukufanyia”. Hayo mambo yalitukaa kwenye akili sisi tuliosoma wakati huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliona pia kitabu cha Wakati Ukuta, Peni na Mlamba, tumemwona mtunzi. Je, watunzi hao tunawaenzi kwa kiasi gani katika kuendeleza Kiswahili cha nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Profesa, wapo maprofesa wengine ambao mimi siwajui ambao wamekienzi Kiswahili. Hata Dkt. mdogo Nyambari Nyangwine, hakuna mwanafunzi wa Dar es Salaam ambaye hakukutana na kitabu cha Nyambari Nyangwine. Yeye yule alitusaidia sana katika kukidadavua Kiswahili sisi ambao hatuwezi kusoma sana. Alijaribu kukidadavua Kiswahili kutoka kwenye Kiswahili fasihi na kuwafundisha wanafunzi. Naye tumevisoma na hakuna mwanafunzi ambaye alishindwa kufaulu Kiswahili form four kama hakupita kwa Nyambari Nyangwine, lazima tumsifu kwa kile alichokifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye kuenzi wazee; ninaona, ndiyo baada ya uhuru pale kwenye picha ya Bismini kuna picha ya askari monument na tumeona kuna maeneo kadhaa kuna picha za Baba wa Taifa. Sasa, Tanzania inakwenda kuingia katika historia mpya ya kupata Rais mwanamke wa kwanza, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Je, histori ya Tanzania imejipanga vipi katika kuhakikisha tunamwachia alama mama huyu? Tumwekee mnara. Kwa sababu kwenye Kiswahili au cultural heritage ina-include monument ambazo zinatakiwa zitengenezwe sanamu mbalimbali, picha kubwa na minara ya kihistoria ili kuwaenzi hawa watu. Pamoja na marais wengi ambao wamepita hapa, lakini sisi tunaomba huyu mwana mama wa kipekee tumuenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka vile vile nimpongeze leo kwa mara nyingine tena Mbunge wa Rufiji kwa jinsi ambavyo ameweza kumuenzi mama, Bibi Titi Mohammed Mandangwa. Ndugu zangu Bibi Titi Mohammed Mandangwa leo anaenziwa kule Rufiji lakini alipigania uhuru wa nchi hii. Sisi wa Rufiji wenzie tunafurahi na tunaona jinsi gani na tunampongeza sana Mbunge huyo wa Rufiji, tunamwombea kwa Mungu, Inshallah, amrudishe ili lile tamasha liendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Bibi Titi Mohammed alirudi tena aliishi Temeke Ngarambe, lakini alikuwa na wadogo zake katika kutetea...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa...
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie. Alikuwa na ndugu zake Bibi Asha Ngoma, Mwamvua Mrisho, Mama Dezi, Bibi Sitti Kilungo ambaye ni Mama Mtemvu na Tatu Ligawike. Akinamama hawa wote kwa pamoja....
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa hatuna muda....
MHE. MARIAM N. KISANGI: ... walitetea uhuru wa nchi hii...
MWENYEKITI: Hatuna muda naomba uhitimishe...
MHE. MARIAM N. KISANGI: ... na tunawakumbuka Wanatemeke na tunawashukuru sana kwa mchango wao. Ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)