Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika bajeti hii ya Wizara hii ya muhimu sana. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Profesa Kabudi pamoja na timu yake yote; Naibu Waziri na timu yake yote kwenye wizara kwa kazi kubwa ambayo wameifanya, wanaendelea kuifanya kwenye wizara hii na kwa kuaminiwa kuendesha wizara hii pana na ya muhimu sana. Profesa Kabudi ni mwalimu wa wengi ikiwa ni pamoja na mimi ninayezungumza hapa, ni mbobezi sana kwenye Sekta ya Sheria; lakini pia CV yako kwenye Sekta ya Habari ni kubwa. Ninaamini kabisa kwamba akisaidiwa na Naibu Waziri kijana ambaye kazi ipo kwenye damu yake basi tutapasua anga na tutakwenda vizuri. Mungu awaongoze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo amefanya uwekezaji mkubwa katika Sekta hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Hata tunavyoona sekta binafsi kuna watu wengi wafanyabiashara wakubwa ambao wameingiza mitaji yao hapo sio kwa sababu nyingine, wanavutwa na wanakuwa na imani kwa kuona kwamba Mheshimiwa Rais mwenyewe yupo mstari wa mbele katika hili. Kwa hiyo mafanikio yote haya yanatokana na yeye mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana nami kwamba, masuala haya ya utamaduni, sanaa na michezo ambayo yapo associated na mambo ya burudani, kwa miaka mingi na hasa katika mila zetu za Kiafrika, kwa Kiswahili cha leo yamekuwa yakichukuliwa poa tu, kwamba ni mambo ya ziada ziada. Wasanii wanaburudisha watu baada ya kazi, wanaburudisha watu wakiwa kazini ili kuwapa hamasa na maeneo mengine mengine. Haikuonekana kama ni jambo ambalo linaweza kuwa na impact kwenye uchumi na ndiyo maana hata wasanii wa zamani kama Mzee wetu Morris Nyunyusa, akina Mwinamila, akina Mbaraka Mwinshehe, hata baadhi ya wacheza mpira maarufu hata kustaafu kwao hakukuwa kuzuri sana kwa sababu hawakuweza kuenziwa ipasavyo kutokana na historia, labda na mila, kwamba sanaa ni kitu ambacho ni cha ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa imedhihirika kwamba sanaa ndio soft power ya nchi na kila kitu sasa hivi kinakwenda softly na wana mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi na katika kui-brand nchi na kujenga taswira ya nchi kwa dunia nzima. Kwa hiyo basi, upo umuhimu mkubwa wa Serikali ikiwakilishwa na Wizara hii kuhakikisha kwamba inaweka mifumo mizuri zaidi ya kisheria na kitaasisi ili kuwalinda wasanii, kuwalea na kuwawezesha hasa katika maeneo ya mitaji na elimu ya kazi yao ili sasa waweze kufanya kazi yao vizuri. Kwa maneno mengine tunahitaji uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Afrika Magharibi wamejitahidi sana kuwekeza kwenye eneo hili mapema sana; na ndiyo maana hata ukienda nje wasanii na wanamichezo wengi waliyobobea wanatoka huko Afrika magharibi. Hata fedha za remittances wanazorudisha nyumbani kwa kufanya kazi hizi nje wenzetu kule wanapata fedha nyingi sana. Tazama sisi kwetu kwa mfano kijana wetu Mbwana Samatta jinsi ambavyo anatuwakilisha vizuri na nina hakika kuwa kuna kipato ambacho kinachorudi nchini. Tunahitaji kuwa nao wengi na hatuwezi kuwa nao wengi ikiwa hatutawekeza vizuri na kwa nguvu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo malalamiko kwa wasanii wadogo wadogo, kwamba, wenzetu wa BASATA wamekuwa viranja zaidi kuliko walezi. Ile Sheria Namba 23 ya Mwaka 1984 pamoja na kanuni zake imewapa mamlaka ambayo wasanii wadogo wanaona kwamba yanatumika zaidi kama fimbo kuliko kuwalea. Kosa dogo sana lina faini kubwa na mengine yanapelekwa kuwa makosa ya jinai na hata kuwaharibia rekodi zao hawa wasanii. Badala ya kwamba mengine yawe ni ya kupewa elimu tu; mtu anaanza kufanya michezo yake hapa kwa kutumia makopo yake ya pale nyumbani, anatakiwa kuelimishwa na kuendelezwa na si kupewa kosa la jinai kwa vile eti hajajisajili. Huwezi kuanza kukimbia kabla hujatembea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunachoomba ni kwamba BASATA itengeneze vyanzo vingine vya mapato, isitegemee sana hizi faini na tozo na kadhalika. Kazi yao ni kubwa wana uwezo mkubwa sana wa kupata mapato wakiwa bado wanaendelea kuwalea hawa wasanii wadogo ili waweze kukua na kufikia level ambazo kwa kweli tunazihitaji. Hilo linahitaji tu mfumo wa kitaasisi na marekebisho ya sheria na kanuni zile zitengenezwe vizuri ili ziwasaidie hawa vijana waweze kukua zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa michezo, hasa mpira wa miguu; tunaipongeza sana sana Serikali, Mheshimiwa Rais kwa kweli amekuwa champion. Ninaungana kabisa na wenzangu waliotangulia, Mheshimiwa Ndulane na dada yangu Mariam Kisangi; kwamba kwa kweli ipo haja ya Mheshimiwa Rais kupewa tuzo kama mwanamichezo, kama mwanasanaa na kama mwanautamaduni namba moja. Ipo haja kabisa ya kufikiria namna ya kufanya hivyo kwa namna nzuri kwa sababu amefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye Jimbo langu la Mwanga, jiografia ya Mkoa wa Kilimanjaro Wilaya za Same na Mwanga zinabeba 60% ya Mkoa wa Kilimanjaro; lakini ukiangalia wilaya hizi mbili zimekuwa nyuma sana katika upande wa mambo ya kuwasaidia kukuza michezo; kwa mfano viwanja vya michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mwanga Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga imefanya kazi nzuri sana. Imejenga uwanja ambao una fence na una pitch nzuri na jukwaa moja. Mheshimiwa Rais wa TFF, ndugu yangu Wallece Karia, nimtaje hapa kwa shukurani sana, kwamba alikuja kufunga ligi yangu, ligi ya Tadayo Cup na aliuona ule uwanja ulivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba, ninaomba aje Mwanga baada ya bajeti hii ili autazame ule uwanja. Nimwombe sana, kwamba kwa haraka atafute fedha kidogo ili tuurekebishe ule uwanja, tuuwekee majani haya ya kisasa ili hata mazoezi ya AFCON yafanyike pale pia. Sehemu hii ya Mkoa wa Kilimanjaro ya 60% ipate nayo cake hii ya AFCON na burudani nyingine ambazo zitaendana na hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mwanga na Wilaya ya Same zipo mahali pazuri na hasa pale kwangu Mwanga hata wanaotaka kwenda kupanda Mlima Kilimanjaro wanaweza wakaja wakafanya mazoezi ya kupanda mlimani. Sekta binafsi imeitikia vizuri kuna hoteli na maeneo ya kukaa. Kwa hiyo, nina-encourage sana Mheshimiwa Waziri karibu Mwanga uje uone lakini utafsiri namna ya kuhuisha ule uwanja kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)