Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia kwenye Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Nianze moja kwa moja kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa ndiye mwanamichezo namba moja Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nimpongeze Waziri wa Wizara hii pamoja na Naibu Waziri bila kumsahau Katibu Mkuu, Ndugu yangu Gerson Msigwa pamoja na Watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na muda ninaomba niende moja kwa moja kwenye zile mada zangu ambazo nitachangia siku ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali ione ni namna gani inaweza kutoa fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati na kwa mtiririko ulio sahihi ili tuweze kukamilisha vile vitu ambavyo tumejipangia hasa hasa kwenye Wizara. Ninasema hivyo kwa sababu gani wakati tunafanya ziara ya Kamati tuliweza kutembelea maeneo mbalimbali, lakini pamoja na hayo tuliweza kwenda kwenye kiwanda au Kampuni ya Magazeti ya Serikali. Pale tunaona fedha zimetolewa kwa ajili ya kujenga jengo, lakini hazikwenda kwa mtiririko unaotakiwa. Kwa hiyo, jengo halijakamilika, lakini vifaa tayari vimekwishanunuliwa ina maana kwamba mashine zote zimenunuliwa na zimewekwa kwenye maghala ya taasisi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapoteza fedha nyingi sana kwanza hii mitambo imekaa zaidi ya miaka miwili chini inaenda kuharibika lakini siyo hivyo tu, pamoja na mitambo hii kuharibika, pia fedha inatumika nyingi kwa ajili ya kukodisha maghala yale. Pamoja na hayo, Serikali inaingia hasara, kwa mwaka mmoja katika uchapishaji Serikali inatoa zaidi ya shilingi 2,000,000,000 kwa ajili ya kuchapisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizo ni nyingi sana zingeweza kutumika kufanya mambo mengine, lakini kwa sababu mitambo imenunuliwa na jengo halijamalizika. Kwa hiyo, kazi inashindwa kuendelea. Tunaishauri Serikali ione ni namna gani fedha zitatolewa kwa mtiririko ili ile Kampuni jengo lao liweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, niendelee kuipongeza Wizara kwa kazi inayoifanya, lakini ione ni namna gani itaandaa mikakati ya kuboresha viwanja vingine vyenye hadhi ya Kitaifa na Kimataifa kwa ajili ya michezo au mashindano, kwa sababu kwa sasa uwanja unaotumika ni Uwanja wa Mkapa pekee yake na tunajua 2027 tunakwenda kwenye mashindano ya AFCON.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuipongeze Serikali kwa kuamua kujenga Uwanja wa Arusha pamoja na Dodoma lakini hapohapo niendelee kuishauri Serikali kwa sababu pale Kilimanjaro tuna Uwanja wa Memorial ione namna gani itaenda kuujenga ule uwanja ili wale wanaocheza kwenye Viwanja vya Arusha waweze kwenda kufanya mazoezi kwenye Kiwanja hicho cha Moshi kwa sababu ni karibu na Arusha. Tuna uwanja wa ndege, na tuna hoteli za kitalii za kutosha. Jambo hili liweze kufanyiwa kazi ili na sisi Kilimanjaro tuweze kupata nafuu hiyo katika uwanja wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wazungumzaji wengi wamezungumza katika jambo hili na mimi ninaomba niunge mkono kwamba je, tumekubali kwamba singeli ndiyo itakuwa inawakilisha Tanzania kwenye jambo la muziki? Kwa nini, tunasema hivyo? Singeli ni muziki mzuri, lakini basi tuangalie je, unakidhi maudhui ya Kitanzania? Kwa sababu wote tunaona mara nyingi nyimbo zinazoimbwa zimebeba maneno ambayo hayaendani na maudhui ya Kitanzania. Kwa hiyo, tuone ni namna gani tunaweza kufanya jambo hili likawa linaleta heshima na kulinda hadhi ya Watanzania hasa wanawake wanadhalilishwa sana kwenye ile michezo wanayocheza kwenye hizo singeli, haipendezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, ninaomba kuishauri BASATA iangalie ni namna gani inaweza kuendelea kuibua vipaji vya wasanii hasa vijana ili kuongeza hamasa kwa vijana wetu, lakini pia kuongeza ajira na kipato kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo ninataka kuishauri Serikali iangalie ni namna gani itapunguza ile hela ya kiingilio pamoja na ada kwa sababu bado ni fedha nyingi sana na vijana wetu hawa ndio kwanza wanajitafuta, hawawezi kulipa fedha zote hizo. Nia ni njema sana kulinda haki zao, lakini ni namna gani basi tuweze kuwasaidia vijana hawa na wao waweze kupata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hata leo kikundi kikienda kuimba kwenye ngoma kama kuna uchaguzi au kuna matamasha yoyote kuna vile vikundi vidogovidogo vya akinamama vinaenda kuimba na wao wanapaswa wajisajili na kulipa hizi hela bado wanajitafuta, hawajaweza kuwa na fedha za kutosha kufanya vitu kama hivi. Kwa hiyo, tunaomba kuishauri Serikali ni namna gani iangalie jambo hili ili tuweze kuwasaidia hawa ndugu zetu waweze na wao kupata ajira na kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kufikia hapo, ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)