Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi hii. Nami nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote kwa uwasilishaji mzuri. Pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji kwenye sekta ya michezo na sekta zote ambazo zipo chini ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, goli la mama limechangia sana hamasa kwenye mpira wa miguu, lakini vilevile uwekezaji kwenye ujenzi wa Chuo cha Malya, ujenzi wa Uwanja wa Mpira kule Arusha na mipango ya kujenga Uwanja wa Mpira hapa Dodoma ni sehemu ya uwekezaji ambao utahamasisha na kuimarisha sana michezo hasa mpira wa miguu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nimeisikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri nimeona nikumbushe baadhi ya mipango ambayo ilikuwepo hapo katikati kama miaka mitatu, miaka minne iliyopita ambayo haijatekelezwa na Serikali. Kulikuwa na mpango wa kununua angalau mpira mmoja kila kijiji, mpira mmoja kila shule, mpira mmoja kila mtaa; jezi seti moja kila kijiji, jezi seti moja kila mtaa angalau hiyo ingehamasisha sana. Hata hivyo, viwanja vya kiijiji, viwanja vya mtaa vilikuwa ni vya muhimu sana; uwekezaji mdogo sana unahitajika hasa eneo tu la ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, usajili wa hizi timu zetu, hivi kweli yangu kutoka Kitunda, timu yangu kutoka Kiloli, timu ipate usajili Dar es Salaam, kwa nini, Mamlaka ya Usajili isiende kwenye Halmashauri ya Wilaya? Timu za mpira wa miguu ziwe zinasajiliwa kama ambavyo wajasiriamali wanavyosajili vikundi vya ujasiriamali. Hiyo ingeboresha sana kupata timu ambazo zimesajiliwa katika wilaya zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kukumbusha mambo machache kuhusu historia ya mpira. Kama isingekuwa Ligi ya Dar es Salaam kuanzishwa mwaka 1929 kusingekuwa na maendeleo mazuri ya mpira wa miguu Tanzania; na kama kusingekuwa na Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ambavyo vilisababisha Serikali ya Kikoloni ikaziondoa timu za majeshi na timu za Taasisi za Serikali kwenye Ligi, basi timu za Simba na Yanga zisingekuwa na umaarufu zilizo nao leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu sana kukumbuka hiyo historia, lakini timu ya kwanza ya wananchi au timu ya kwanza ya kiraia kucheza Ligi ya Dar es Salaam ilikuwa Cosmopolitan. Kwa hiyo, ni muhimu sana kukumbuka kwamba Timu ya Cosmopolitan ni timu kogwe kuliko timu za Simba ya Yanga na lazima kuipa Timu ya Cosmopolitan heshima. Mamlaka za Mpira wa Miguu Dar es Salaam zisaidie hii timu ya Cosmo angalau iweze kupanda daraja ili iweze kutoa ushindani kwa Simba na Yanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, …

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, anasema tuipe heshima Timu ya Cosmo, ninaomba atusaidie Mheshimiwa kwamba, hiyo timu ipo wapi mpaka sasa hivi? Ahsante!

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Timu hii ya cosmopolitan ipo kwenye Jimbo lako na sasa hivi inashiriki Ligi Daraja la Tatu. Kwa hiyo, ni muhimu sana kijana wangu aelewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo matatizo makubwa sana kwenye michezo hasa kwenye mpira wa miguu. Tatizo la kwanza, kuna tatizo la kukosekana kwa uadilifu kwenye mpira wa miguu watu wanajali zaidi mapenzi ya Simba na Yanga bila kujali maendeleo ya mpira wa miguu. Tatizo la timu kucheza chini ya kiwango kwenye ligi ninaomba Serikali na Mamlaka za Mpira wa Miguu ziliangalie sana hilo jambo, yaani timu inaamua kucheza chini ya kiwango kwa sababu inacheza na timu fulani. Sasa kuna kuwa na mapatano ya aina gani? Inatakiwa uchunguzi ufanyike ili kubaini tatizo hilo na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la kuahirishwa Mechi ya Simba na Yanga, Mamlaka za Mpira zilisema zinafanya uchunguzi, lakini tangu ziseme zinafanya uchunguzi mpaka leo taarifa ya uchunguzi haijatolewa hadharani, halafu inaibuka ratiba tu ya Ligi kuendelea bila taarifa ile, Watanzania wanakuwa hawajatendewa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, Sheria 17 za soka, zimekuwa zikilegezwa katika baadhi ya mechi. Kuna matatizo makubwa ya ma-referees wengine wanapewa adhabu kila siku. Ninaomba sana Mamlaka za Mpira wa Miguu zisimamiwe vizuri ili zisimamie Ligi yetu vizuri na iwe bora kweli kweli siyo bora kwenye karatasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, niipongeze sana Simba Sport Club, timu ya Simba imeiletea sana sifa nchini. Mwaka 1974 isingekuwa penati Timu ya Mahalla Ghazl El Kubra ilikuwa imeshatolewa mashindanoni, Simba iliingia Nusu Fainali ya Klabu Bigwa Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1993 Simba iliingia Fainali ya Kombe la CAF ambalo ni kabla ya kuunganishwa makombe mawili Kombe la CAF na Kombe la Washindi ambalo sasa hivi ndio Kombe la Shirikisho na mwaka huu imeingia Kombe la Shirikisho. Simba Sport Club imekuwa ni nembo kubwa ya soka la Kimataifa la Tanzania, ni muhimu sana kila mtu aunge mkono maendeleo ya soka Tanzania, kupitia timu hizi za Simba na Yanga. Ahsante sana. Ninakushukuru Sana. (Makofi)