Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ndugu zangu wa CHADEMA kule, CHADEMA naomba mnipatie na mimi tano ziwe 10. Wamekubali. Sasa ... (Kicheko)

MWENYEKITI: Samahani Profesa, samahani Profesa.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Ndiyo.

MWENYEKITI: Mic yako iko sawa?

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, unanipata?

MWENYEKTI: Nakupata, endelea.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu dakika 10 za CHADEMA umenipata? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, sasa ni hivi ndugu zangu, mimi nadhani hii miradi ya barabara (miundombinu) ukifuatilia duniani kote, nchi zote ni miradi ya kudumu. Kwa hiyo, kwa upande wa Tanzania lazima tuipitishe bajeti kwa sababu lazima barabara zijengeke. Hata huko Marekani na wapi, barabara lazima zijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba nina barabara moja na ninatoa shukrani nyingi kwamba Mheshimiwa Rais alivyokuwa jimboni nilimwomba vitu viwili tu; barabara na mradi wa umwagiliaji na vyote vimekubalika Serikalini. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais na miradi yangu imekubalika inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaongelea barabara yangu kwa kifupi, hiyo ya kilometa 92. Barabara yangu inaunganisha vijiji vyote 68. Kiuchumi inakubalika, ni roho ya Mkoa wa Mara na Tanzania nzima. Barabara hii makadirio yake mwaka 2020 gharama yake ilikuwa Dola za Marekani milioni 50. Leo hii mwaka 2025 gharama zake ni dola milioni 53. Kwa hiyo, unaona ndani ya miaka mitano ambavyo hatukutekeleza huu ujenzi wake kwa haraka, gharama zimeongezeka kwa zaidi ya dola milioni tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Wizara ya Ujenzi, kwanza tujaribu kutekeleza miradi hii ya barabara kwa haraka, kwa sababu tutapunguza ongezeko la gharama za ujenzi wa barabara za lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara yangu ina miradi miwili ndani yake. Ina kilometa 40 ambazo nadhani wiki hii wanamaliza majadiliano na mkandarasi. Kwa hiyo, nawaomba TANROADS na Wizara waweze kumpatia mkataba aanze kujenga kabla ya tarehe 01 mwezi wa Saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii nayo ina mradi wa pili, daraja kubwa la kisasa ambalo gharama yake ni karibu shilingi bilioni 60. Naishukuru Benki ya Dunia (World Bank) wamekubali kufadhili hii barabara. Kwa hiyo, naomba TANROADS na Wizara waharakishe kupata no objection. Niliwaomba kwamba yakiwa magumu saa nyingine wau-outsource watu ambao tumefanya kazi nao tuweze kupata hiyo fedha haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo dakika nilizokuwa naomba kuongezewa nataka kutoa mapendekezo ya kupata fedha za kutekeleza miradi ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, sasa hivi ukienda kwa kila Mtanzania ukiuliza anachohitaji ni vitu vitatu; maji, umeme, na barabara. Tukiri kwamba bajeti yetu ni finyu, haiwezi ikatekeleza kwa haraka sana. Sasa, haya ndiyo mapendekezo yangu ya kupata fedha za kutekeleza ujenzi wa barabara zote ikiwemo na ya kwangu ya Musoma Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuongeze bajeti, na kuongeza bajeti ninamaanisha miradi mikubwa mikubwa kwa miaka miwili inayokuja tuipunguzie bajeti kwa 40%. Hiyo bajeti iliyopunguzwa 40%, siyo kwamba tunasimamisha miradi mikubwa, ila tunaipunguzia na hizo fedha ziende kwenye ujenzi wa barabara, maji, na umeme. Hiyo ni strategic planning na financial deployment. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha pili cha fedha za kujenga barabara lazima tuanze kukopa kwenye benki zetu za ndani na ambazo Serikali ina hisa. Tukubaliane tuwe na concessional loans, yaani wasitoe riba zaidi ya asilimia nne. Hiyo itafanya Wizara ya Ujenzi ipate fedha za kutekeleza miradi yake, concessional loans kutoka kwenye benki zetu za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha tatu, ile PPE tunayosema triple P (Public Private Partnership) ianze kujenga barabara na hizi barabara za triple P tunapaswa kuanza kupata tozo (road tolls). Hizi ni fedha nyingi sana na sehemu nyingine kote duniani ukienda barabara kubwa unasimama mahali unalipa au unakuwa umelipa kabla ya kuanza safari yako. Hayo ni makusanyo makubwa sana yatafanya barabara zetu ziweze kupata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha nne, hauwezi ukakwepa kukopa nje. Hili la mikopo jamani lisiwatie homa sana, tutaliongea kwenye bajeti. Tuna takwimu ya mikopo ya nchi kubwa duniani hapa. Kwa hiyo, nasi tusiogope kukopa ili mradi hiyo mikopo itumike kama inavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mikopo mizuri hapa ninayoongelea ni mikopo ile ya riba kidogo, ambayo ni ya 0.05 mpaka three percent, concessional loans. Hiyo ndiyo mikopo ya World Bank, mikopo ya IMF, mikopo kama hiyo tuichukue, tujenge barabara, tusambaze maji, tusambaze umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha nne ni EPC+F yaani E ni Engineering, P – Procurement, C – Construction na Financing, EPC +F. Huu ni mtindo unatumika sehemu nyingi sana duniani. Mnamtafuta mtu ambaye ana fedha, ana uwezo wa ujenzi wa barabara, mnampatia barabara anajenga mnalipana pole pole, lakini hapa tahadhari ni kwamba usiende kwenye EPC+F wakati wewe hujui gharama za barabara yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi Musoma Vijijini wakija, najua barabara yangu ni dola milioni 53. Kwa hiyo, naweza kumpokea kwa sababu najua tayari najua gharama za barabara. Kwa hiyo, hii ni njia nyingine ya kuweza sisi kupata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, njia ya mwisho ni kwenda kwenye Dar es Salaam Stock Exchange. Miradi mikubwa yote duniani inaendeshwa kwa stock exchange. Hata migodi yote mikubwa unaiona duniani ni stock exchange. Sasa kwa sababu viwanja vyetu vya ndege vingine ni makampuni, kama kiwanja cha ndege Dar es Salaam na Kilimanjaro, hivyo viwanja vya ndege viende kwenye stock exchange ya Dar es Salaam na tuweze kupata hapo fedha za kuweza kujenga viwanja na barabara. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni mapendekezo ya ujenzi wa barabara za Tanzania. Bado tunakuwa waoga, tunajenga barabara kwa mtindo ambao baadaye unafanya unakuwa wa gharama kubwa. Barabara za highways zote tuseme Dodoma Morogoro, Musoma - Mwanza hizo barabara zinapaswa kuwa na njia nne, mbili kwenda, mbili kurudi na zinavyozidi kwenda zinapaswa kuwa na njia tatu na sehemu za kupumzikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka hii barabara ....

MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa muda wako ulishaisha tafadhali.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya nashukuru sana, naomba waendelee kujenga barabara ya Musoma Vijijini na tuendelee kutafuta fedha za kujenga barabara. (Makofi)