Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi. Ninaomba nianze kuungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais ambaye ni mwanamichezo namba moja wa nchi yetu kwa sababu kwa mpango wake mzuri wa sekta hii ya michezo ameinua sana michezo nchini. Hongera sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ninajisikia fahari sana kuchangia wizara hii ambayo inaongozwa na mwalimu wangu mahiri sana Mheshimiwa Profesa Kabudi ambaye amenifundisha katika fani ya sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hongera sana kwa Profesa kwa uteuzi huu, jambo ambalo sikujua ukiwa mwalimu, sikujua pia kama wewe ni bingwa wa singeli. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Naibu Waziri, ndugu yetu Mheshimiwa Mwinjuma kwa kazi nzuri, ninakushukuru sana na wewe ni mtu rahimu sana, ni mtu muungwana sana. Kwa kweli wananchi wa Muheza walipata Mbunge mahiri ahsante sana. Nimshukuru Mheshimiwa Msigwa pamoja na Naibu wake kwenye Wizara hii ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nichangie maeneo machache mchana huu. Nianze na jambo la kwanza ni kuhusu mikopo kwa wasanii na hapa niwasemee mahususi wananchi wangu wa Jimbo la Lupembe na wananchi wa Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Waziri alikuja Jimbo la Lupembe kufunga Swalle Cup mwaka 2023, alishuhudia wingi wa vijana wenye vipaji vya muziki, vipaji vya michezo. Kule Jimbo la Lupembe tunao vijana wengi wenye vipaji vya muziki na michezo. Tunao vijana kama akina Buki Boy kutoka pale Madeke, lakini Manisaiso, tunao akina B2K kutoka pale Makambako, akina Mack Ford kutoka Makete ambaye ameimba wimbo maarufu sana wanasimama na mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao vijana kama wakina Masai the don, kaimba wimbo maarufu sana, unaitwa mama mitano tena. Hao vijana wamealikwa mpaka Ikulu kwenye hafla kwa ajili ya Sanaa. Kwenye mpango huu wa mikopo ninaomba, mikopo hii isilenge watu wakubwa tu, iwalenge pia na vijana hawa chipukizi ili wapate mikopo hii waweze kuinuka pia katika sanaa yao ya muziki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nichangie pia kuhusu viwanja vya michezo. Nimeona kwenye bajeti ya awamu hii, wana mpango wa kujenga viwanja mbalimbali ndani ya mikoa na ndani ya halmashauri. Sisi Mkoa wa Njombe ni eneo muhimu sana kwa kuwekeza kwenye michezo. Wasiojua sisi Mkoa wa Njombe tumewahi kutoa wachezaji mahiri katika nchi hii na hasa katika Jimbo la Lupembe. Wasiojua, Fred Mbuna katokea Jimbo la Lupembe ninakozaliwa mimi na amekuwa mchezaji mzuri kwa timu ya Yanga, lakini pia tumekuwa na mchezaji Nico Nyagawa kafanya vizuri sana kwenye Simba mpaka leo yupo. Hawa ni icon ya Mkoa wa Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Mkoa wa Njombe kwenye mpango huu muukumbuke kuupatia uwanja wa mpira kwa heshima ya hawa wachezaji na wananchi wa Njombe. Jimbo la Lupembe tunalo eneo kubwa, mkitaja maeneo Lupembe yapo ya kutosha. Tunavyo viwanja vingi tu pale Mtwango, Nyombo, Kidege, Wanginyi. Mnaweza kuchagua kati yake mkajenga uwanja mzuri sana kule Njombe kwa ajili ya michezo ya vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine pia nataka nichangie hapa leo kwa mchana huu, ni kuhusu ligi za Waheshimiwa Wabunge. Kumekuwa na ligi nyingi za Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yao, Wabunge wamekuwa wakitumia fedha nyingi sana kwa ajili ya hii michezo. Ninaomba Wizara hii i-coordinate hii michezo ya Wabunge, itambue Wabunge kama ni wadau kwenye hii michezo ili iwasaidie ufundi pale panapobidi, lakini pia kufuatilia hii michezo ili iwe sehemu ya kukuza michezo ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, ninaomba niseme hapa. Nimeona pia huu mpango wa kuanzisha taasisi ya kusimamia miundombinu ya michezo, hili ni jambo kubwa sana Mheshimiwa Waziri. Miundombinu mingi sasa hivi kama umetazama, tumeanza kutia aibu, kucheza mpira kwenye viwanja vilivyojaa maji, kuwa na viwanja vitu vimeharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini taasisi hii ya kusimamia miundombinu ninaomba ianze mapema, ianze kusimamia viwanja vya michezo. Hii itatusaidia kuwa na uhakika wa viwanja vyetu kwenye sehemu ya ulinzi pamoja pia na usalama wa viwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kuchangia kidogo. Kuna jambo moja Mheshimiwa Waziri ambalo pia wengi wamesema sana humu ndani tangu asubuhi, ni kuhusu mchezo wa Simba na Yanga. Jambo hili limeleta taharuki kubwa isiyokuwa na sababu, tumemwona Mheshimiwa Waziri akienda kwenye kikao, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, walipotoka hawakusema jambo lolote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Ligi naiheshimu sana, Mheshimiwa Rais wa TFF namheshimu sana, wanafanya kazi kubwa sana, lakini kuna shida gani kutuambia maamuzi waliyofikia?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kwa mujibu wa Kanuni zetu, suala hilo unalolizungumzia lipo kwenye shauri la kisheria, katika ngazi ya maamuzi. Kwa hiyo, nikuombe usizungumzie masuala hayo ndani ya Bunge na kulihusisha Bunge na masuala ya kisheria na kulitia Bunge katika migogoro. TFF na vilabu wana kanuni zao, wanatawaliwa na mamlaka zao za CAF na za FIFA. Endelea.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea maelekezo ya kiti na siwezi kupingana nayo, ninaheshimu. Nilichotaka niseme tu ni kwamba, kwa sababu kuna hisia za mashabiki wa Tanzania tunaomba vyombo vyetu vya vilabu waheshimu sana hisia za mashabiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuacha haya mambo kwenye giza bila kuwa na ufafanuzi, nani kakosea, nani kapatia, hii sio sawasawa kwa sababu mpira sio mpira wa busara, ni mpira wa sheria, mwenye kadi nyekundu, kadi nyekundu, mwenye njano kadi ya njano.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)