Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi. Nimpongeze mwanautamaduni, Sanaa na michezo nambari moja Tanzania, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameonesha utayari kwenye ku-support utamaduni, Sanaa na michezo kama ambavyo jina la Wizara lilivyo na shughuli zake wanazozifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumemwona mara kadhaa akienda kwenye matamasha mbalimbali yanayohusiana na masuala ya utamaduni, Sanaa na michezo. Flow ya fedha pia kuelekea kwenye Wizara hii ni tofauti kulikoni miaka mingine yoyote ya nyuma tukiangalia flow ya fedha watu ambao wanafuatilia mwenendo wa bajeti kwa mwaka baada ya mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua ni kwa sababu pia kuna msukumo mkubwa wa AFCON na ninajua pia hata wakiuliza katika lobbying tunamfahamu ni miongoni mwa lobbyist namba moja kwenye mambo mbalimbali ya kidunia na kikanda kwa maana ya Africa. Ninafikiri hata sababu mojawapo ya kuleta AFCON Tanzania ni pamoja na ushawishi wake kwenye nafasi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia wasaidizi wake Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali kwa sababu wanakimbizana kutuhakikishia kwamba nchi inaenda kwenye masuala ya utamaduni, sanaa na michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Wizara nimewapongeza hapo lakini ninajua kuwa Wabunge wengi wameshajadili, wameshazungumza pia kuhusiana na mienendo ya vilabu vyetu kwa mfano kwa upande wa Simba na Yanga na vilabu vingine of course kwa sababu kuna vilabu lazima vijue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze na niwaombe sana muendelee kuwa waadilifu kwa sababu sisi tunaamini Serikali ndiyo balancing. Kila watu ni mashabaki kwenye vilabu vyao vya Simba au Yanga ama Azam na timu nyingine, lakini Serikali ndiyo balancing. Kwa hiyo, tuwaombe waendelee kuwa waadilifu kwenye eneo hilo, mnajua kila mtu anajua wajibu wake na majukumu yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya uchache wa muda nitajielekeza kwenye hoja moja tu mradi namba 6505, ujenzi wa kiwanda na ununuzi wa mitambo ya uchapaji wa magazeti ya Serikali TSN. Ukifuatilia taarifa ya Kamati wameshauri baadhi ya vitu ambapo pia vinaweza vikashtua watu kwa nini tumeshauri kwamba Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali aende akapitie pale TSN aone kuna changamoto gani ambazo zilitokea, lakini nitaeleza kwa ufupi sana ili waelewe kwa nini tumesema kwamba waende wakakague, tuna wasiwasi kuna kitu hakipo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza mradi una maeneo mawili. Kuna upande wa ujenzi wa kiwanda, eneo la pili ni ununuzi wa mitambo na vifaa kwa ajili ya kuendesha mradi wote wa TSN. Kwa hiyo, upande wa kwanza kwenye ujenzi, tarehe 7 Juni, 2023, TSN ilisaini mkataba na Kampuni ya Group Six International ambayo ilipewa kazi ya kujenga hilo jengo ambalo ndilo kiwanda tunachokizungumza ilikuwa na takribani bilioni 3.8. Malengo na mkataba ulikuwa unaeleza kwamba ndani ya miezi sita wawe wameshamaliza kujenga jengo yaani structure iwepo ili kiwanda cha TSN kianze kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka ninavyozungumza, kwa hiyo ukiangalia hapo hesabu kuanzia Juni ilitakiwa Novemba wakabidhi jengo, lakini mpaka ninapozungumza jengo halijakamilika na halijafika 50% na kamati tumeenda kukagua, bado kuna changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho kimetushtua sana ni kwa sababu mwenyewe kwenye maisha yangu tu hata ya ujenzi sijawahi kuona na kila mtu hapa anajenga tunafahamu, huwezi kununua furniture kabla haujamaliza kujenga, lakini TSN wamenunua mitambo, ambalo eneo la pili, nilisema ni ununuzi wa mitambo, wameshanunua mitambo 78% jengo halijafika 50%. Mitambo tunayozungumza hapa sasa hivi, wamekodi godauni, limewekwa pale wanawasha AC full time kwa mwaka wanalipa milioni 45 kwa ajili ya kupuliza ile mitambo isiharibike.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo mitambo imeshafika, mradi unasema kununua mitambo saba, wameshaleta saba, mitano imeshakombolewa bandarini lakini miwili bado ipo bandarini. Tunapozungumza, bandarini kuna mitambo ya shilingi bilioni 6.9, hatujui ina hali gani kwa sababu hatukufika bandarini kukagua mitambo ambayo ipo bandarini, mashine zile za uchapaji ambayo ipo pale ambayo ni mitambo mitano na imegharimu 15.3 bilioni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wameiweka pale kwenye godauni. Kuna gharama za uendeshaji wa kutunza hilo eneo, kuna gharama za kodi tunalipa na hii kununua mitambo ilikuwa 2022, pamoja na kwamba ninajua ile ni special order. Kwa hiyo, ile mitambo ilitengenezwa kwa ajili ya ku-feed mahitaji ya kiwanda chetu. Ninajua kwamba ilibidi watoe pre, ndiyo maana tumesaini 2022 halafu imeanza kuletwa mpaka sasa hivi 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, sijawahi kuona hiki kitu, ndiyo maana tunaomba CAG akaangalie pale. Tunajua kuna mambo yanaendelea na yule mama pale ana mwaka sasa hivi, yeye kabla hata hajaingia yule Mkurugenzi Mtendaji wa pale TSN hayo mambo yalishafanyika huko nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sijui kama hii Serikali ipo namna gani, kwa sababu, kwanza unaweza ukashangaa kwamba mitambo ipo pale ni mitambo ya Serikali na Serikali ni moja hii hii. Kwa nini, hii mitambo badala ya kuiweka pale kutumia gharama kuilinda na kuihifadhi ili isiharibike, kwa nini wasingeweka kwenye entity nyingine ya Serikali ambayo inafanya printing? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hii TSN tunapozungumza ndiyo tulisema tutengeneze kiwanda cha uchapaji ili hata kulinda nyaraka za Serikali zisiwe zinachapishwa kwenye makampuni binafsi. TSN bado inatumia makampuni binafsi kuendesha shughuli zao za ki-media, kiuandishi na kiuchapaji, wanalipa makampuni ku-print taarifa zao. Maana yake tunapoteza pesa, tukiweka hiki kiwanda tuna uwezo wa kuokoa 60% ya gharama za uchapaji wa taarifa zinazozalishwa kwenye magazeti ambayo yapo TSN, magazeti ya Serikali tunayafahamu Daily News na mengineyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua tulishazungumza pia kwenye Kamati, tuwaombe sana Wizara, tunaomba waokoe kwa sababu hizi ni fedha tunazozungumza ni fedha za Watanzania. Hizi figures nimetaja kwa sababu ununuzi wa mitambo peke yake ni bilioni 23 full. Kwenye ujenzi inakwenda bilioni tano kwa sababu kuna part ya kwanza ya ujenzi na part ya pili ya kuweka infrastructure za maji na umeme. Kila akitokea Waziri mpya anapelekwa pale kwenda kukagua lile jengo limebaki pale white elephant.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kiti chako na viongozi ambao wanatusikiliza, hebu tumieni busara. Pelekeni flow ya hela iwe nzuri pale, mWende mkamalize lile jengo. Malizeni lile jengo ili ile mitambo ianze kutumika. Kama haiwezekani, basi pelekeni kwenye entity nyingine ya Serikali ambayo inafanya printing ili ile mitambo ikatumike kwa sababu hizo fedha ni za walipakodi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaongea hivi kwa uchungu sana, kwa sababu tumeenda pale kuona. Kwa hiyo, nilitaka nizungumze hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia cha mwisho nawapongeza sana TFF kwa sababu tulienda kukagua one of the sports academies (vituo vya michezo) viwili; kimoja kipo Tanga na kingine kipo Kigamboni. Tumeona vijana wadogo wa under fifteen waliopita pale wameshinda kwenye michezo ya under fifteen mara mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba pia Serikali iendelee kuona umuhimu wa kuanzisha sports academies kwa sababu pia tuna miaka miwili kwenda kwenye AFCON. Pengine itasaidia kukuza vipaji na pengine hata sisi watu wa Ikungi tunaweza tukapata sports academy na pengine tunaweza tukapata pia kiwanja cha riadha, kwa sababu unajua sisi watu wa Singida tunakimbiza upepo sana, ndiyo maana mnaona hata Alphonce Simbu ameshinda kwenye Mashindano ya Boston juzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninaunga mkono Hoja ya Kamati.