Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiwani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata fursa hii. Kwanza, namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya katika Sekta ya Michezo na kuhakikisha kwamba viwanja kwa ajili ya AFCON vinatayarishwa. Tunajua kuna Viwanja vya Dodoma, Arusha na baadhi ya viwanja vingi ambavyo vinafanyiwa ukarabati. Tunamshukuru sana kwa kazi hii kubwa ambayo anaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tunampongeza Waziri, Mheshimiwa Profesa Kabudi pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha kwamba Wizara hii inafanya majukumu yake kama ambavyo wamejipangia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja nianzie kwenye Kombe la Muungano. Kombe hili tuliliacha miaka mingi , lakini ni miaka miwili sasa Serikali zetu hizi mbili kupitia Wizara ya Habari na Michezo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ile Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zimelirudisha tena kombe hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawakumbusha hawa Waheshimiwa Mawaziri kwamba kombe hili lina hadhi kubwa sana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, ni vyema kwamba mashindano haya yasishirikishe tu timu nne kutoka Bara na timu nne kutoka Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuige wenzetu ambao wanafanya mashindano hayo ikiwemo Spain. Kuna Kombe La Mfalme linashirikisha timu nyingi. Halikadhalika Afrika Kusini na Misri, wote wana mashindano hayo, ukiacha ligi kuu ambazo zinaendeshwa nchi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika katika jambo hili, zawadi ambazo zinatolewa ni ndogo. Kwa mfano, juzi tumeshuhudia kule Timu ya Dar es Salaam Young African ikichukua kombe lile na zawadi ya shilingi milioni 50 kwa kuifunga Timu ya JKU ya Zanzibar. Kwa kweli kwa hadhi ya kombe hili, namwomba Mheshimiwa Waziri ashirikiane na Mheshimiwa Waziri Tabia wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kombe hili liwe na zawadi kubwa ambayo inafika hata shilingi milioni 100. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar kuna mashindano wanachezesha yanaitwa Yamle Yamle Cup. Mashindano haya huanza kwa timu zaidi ya 80, lakini fainali yake inakuwa ni fainali moja kubwa sana na ya kibabe ambapo mara zote mgeni rasmi huwa ni Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na zawadi kubwa nazo huwa zinatolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili, kwenye Mashindano ya Yamle Yamle, naomba Mheshimiwa Waziri azungumze na viongozi wake akiwemo Mheshimiwa Rais Karia. Hili jambo la kufuta haya mambo ya Ndondo Cup, siyo jambo zuri sana kwa sababu jambo hili la hizi Ndondo Cup, mashindano kama yale ya Yamle Yamle ndiyo ambayo yanawafanya wachezaji wetu wa Tanzania kukuza vipaji vyao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona mfano kwamba, asubuhi hapa nilikuwa ninampa taarifa Mheshimiwa Taletale kwamba, ile Zanzibar timu zao kuwa imara, kuwa zinafanya vizuri, hazifungwi mabao matano na manne; ule ni uimara wa ZFF jinsi ambavyo inasimamia ile ligi vizuri. Hakuna mabao matano, hakuna mabao manne au sita. Hamna habari ile. Wala hausikii wachezaji kugombana na waamuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, timu ni gharama na mashindano ni gharama. Timu zinagharamika, ufadhili upo sawa, lakini haitoshelezi kuziendesha timu. Kwa hiyo, naiomba TFF, jambo la kusimamia ligi kwa uadilifu ni jambo muhimu sana na litatupeleka mbele sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Zanzibar kuna wachezaji zaidi ya 50 ambao wako huku Tanzania Bara wanacheza kwenye vilabu mbalimbali vya Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Yote hii ni kwa nini? Ni kwa sababu wameonekana katika mashindano mbalimbali ambayo yanachezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, namwomba Mheshimiwa Waziri kitu kimoja pia kwamba, kuna ruzuku ambayo inatoka CAF na FIFA, ambayo kwa makubaliano yao TFF na ZFF wamekubaliana kwamba kila mwezi wawapatie wale ZFF shilingi milioni tano. Kwa kweli hili ni jambo la kusikitisha sana. Leo tuko Mei lakini hakuna hata senti iliyopelekwa ZFF. Kadhalika, kuna mwaka 2024, nadhani kuna miezi kadhaa ile fedha nayo bado haijaenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TFF wale ZFF ni ndugu zenu na Karia yupo anasikia. Wawasaidie ile elfu tano tano ili nao wakuze lile suala la michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye AFCON, Zanzibar ni lazima tumpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kurekebisha miundombinu ya viwanja vya michezo. Tunashukuru kwamba hata Ligi Kuu ya NBC kuna baadhi ya mechi zinachezwa kwenye Uwanja wa Amani Complex. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tumeshuhudia vilevile kwenye hili Kombe la Muungano kwamba mashindano yale yamefanyika katika Uwanja wa Gombani, uwanja ambao una hadhi ya kuchezwa AFCON.
Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo ikikupendeza hii ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na mashindano yanakuja Tanzania, ni vyema ule Uwanja wa Amani na Gombani ukatumika kikamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwenyewe anayesimamia michezo hapa TFF, Rais Karia, ambaye ‘r’ yake ni ndogo, alikwenda Zanzibar kushiriki kwenye yale mashindano na alikwenda kukagua baadhi ya viwanja. Kwa hiyo, namhakikishia kwamba kuna viwanja vingi vya timu kufanya mazoezi, viwanja standard na viwanja vinavyokubalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nashukuru kwa kunipatia muda huu na ninasema, naunga mkono hoja, ahsante sana.