Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Maimuna Ahmad Pathan

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia hoja iliyopo Mezani leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mungu kwa kutupa pumzi yake ya uhai, na pia napeleka pongezi kuu kwa Kiongozi wetu Mkuu wa nchi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi zake nzuri ambazo anazifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Ujenzi kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Tumeona maelezo yenu ni mazuri, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu yaweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze na barabara ya kutoka Liwale kwenda Morogoro. Hii ni barabara ya kuunganisha mikoa miwili, ni ya muhimu sana. Tunaiomba Serikali kuna kipindi barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara iliharibika, wananchi wanaotoka Liwale – Nachingwea walikuwa wanazunguruka sana mpaka kufika Dodoma. Wanatoka Liwale wanapita Nachingwea, wanaenda Masasi, wanaenda Ruvuma – Njombe – Makambako – Iringa mpaka warudi Dar es Salaam au waje Morogoro ni safari ndefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba sana Serikali watutengenezee barabara ya kutoka Liwale kwenda Morogoro, itawasaidia sana wananchi wa kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali kwa mapitio na ujenzi wa barabara ya Kibiti - Lindi. Hii barabara inakatisha tamaa, kwani ni mbovu sana. Kama alivyoongea jana Mbunge wa Dar es Salaam, Mama Kisangi alisema kuna maeneo ni korofi, yanakatisha tamaa. Vilevile kuna Mbunge wa Songea aliongea, Mheshimiwa Mama Msongozi akasema kuna vidungurushi, yaani kuna yale mashimo ya hatari, barabara hizi zinakatisha tamaa. Serikali imechukua jitihada ya kuitengeneza, imeanza na madaraja, tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe angalizo kidogo, pale Somanga, maji kila siku yanavuka daraja yanapanda juu. Ombi kwa wakandarasi ambao wanaitengeneza barabara ile, waangalie eneo lile, kama hawana uwezo wa kuweka flyover, basi hilo daraja wahakikishe wanaliinua, kwa sababu wakiweka daraja bila kuinua eneo lile, yale maji yatavuka juu ya daraja, na itakuwa ni kazi bure, bado tutaendelea kupata shida wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kupitia barabara ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pamoja na utengenezaji wa madaraja, tuendelee kuwasisitiza na kuwaomba kwamba ile barabara kiukweli ilitengenezwa chini ya kiwango, ni mbovu, mbovu, mbovu sana. Bado tuendelee kuwasisitiza Serikali waendelee kutengeneza kipande kwa kipande mpaka wakamilishe barabara ile, kwa sababu barabara ile siyo ya kutengeneza sehemu moja, ni ya kuibomoa yote, haifai kabisa. Tunaomba Serikali na tunasisitiza kwenye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuiongelea pia barabara ya kutoka Masasi kwenda Nachingwea - Liwale. Barabara hii ni ya muhimu sana, kama inavyoonekana kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, imekuwa ikijirudia kila siku. Naiomba Serikali na tunajua inao mpango huo wa kuianza hiyo barabara lakini bado nisisitize kwamba barabara hii ni ya kimkakati, kuna mambo mengi sana ya msingi ambayo yanatakiwa yatumike kwenye barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa unaenda Liwale kutoka Nachingwea, mvua ikinyesha ya dakika tano tu ile barabara huwezi kwenda, inateleza, inajaa maji, inakatisha tamaa. Tunaiomba Serikali na kuwasisitiza, tunajua mna hilo lengo, tunaomba mtutengenezee barabara ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile tangu tumepata uhuru mpaka leo haijawahi kuonja lami. Wananchi waliopo kule ambao hawajawahi kufika mjini Dar es Salaam wala wapi, hawaijui lami. Nawaomba, ile barabara bado ni mpya japokuwa ni barabara kongwe ya miaka mingi na ni barabara inayotoka kwenye mkoa mwingine kwenda mkoa mwingine. Tunaiomba Serikali na kuwasisitiza, tutengenezewe barabara ile kwa kiwango cha lami ili wananchi waweze kuona faida za kodi zao ambazo wanazilipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia barabara hiyo ya Masasi kwenda Liwale kuna waathirika ambao nyumba zao zimebomolewa, wamechukuliwa maeneo yao, na ni miaka mingi zaidi ya 15. Kwa kweli hii inakatisha sana tamaa wananchi. Naiomba Serikali tufanye juu chini ili tuweze kuwalipa wale waathirika wa barabara hiyo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Kicheko)