Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuweza kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara ya Michezo. Kwanza, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye sekta hii ya michezo. Hongera sana Mheshimiwa Rais. Kazi kubwa imeonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa uteuzi wa nafasi ya hii Wizara, maana yake ni Mheshimiwa Waziri ambaye ni mbobevu kwenye masuala ya kisheria.

Hongera sana Mheshimiwa Prof. Palamagamba Kabudi kwa kuteuliwa na kuongoza. Watanzania wanakutegemea na wanakuona kwamba upo kwenye nafasi sahihi kwa sababu umeingia, unafahamu sheria na kanuni, huwezi kuburuzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, napenda kuipongeza Serikali kwa uwekezaji kwenye viwanja. Kuna ujenzi kule wa Kiwanja cha Arusha, ujenzi wa Kiwanja Dodoma na ujenzi wa viwanja mbalimbali na maboresho kwenye Kiwanja cha Taifa cha Dar es Salaam. Hongera sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sasa Mheshimiwa Waziri akikumbuke na Kiwanja cha Ali Hassan Mwinyi pale Tabora, tupate kiwanja bora cha kisasa. Wazungumze na partnership CCM ili kuona ni namna gani wanaweza kukiboresha, kwani kuna fedha nyingi. Kama unavyotambua, Tabora ni Mkoa wa kimkakati na Tabora tunahitaji kukuza viwango vya wanamichezo wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalopenda kuzungumza, kama ambavyo unafahamu, tumeweza kuona namna gani ambavyo tunashiriki michezo yetu. Ligi yetu inakua na inavutia sehemu mbalimbali duniani. Leo natumia nafasi hii kuwapongeza Azam kwa uwekezaji mkubwa katika ligi ya Tanzania. Hongera sana kwa Azam, wamefanya kazi kubwa na amewekeza fedha nyingi. Watanzania wanaona, dunia inaona, na wachezaji wanavutika kutokana na fedha alizowekeza kwenye ligi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nishauri. Tumeweza kuona Ligi Kuu ya Uingereza inayoongozwa na bodi ya ligi ambayo inaitwa EPL. Pia Federation ya Uingereza ina Ligi yao ya FA. Hizi ni ligi mbili na bodi ya ligi ya Uingereza inasimamia kila kitu na masuala mazima ya Ligi Kuu ya Uingereza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Ligi Kuu ya Spain inaongozwa na bodi ya ligi. Pale Spain kuna bodi ya ligi inaitwa LaLiga inasimamia masuala mazima ya michezo katika Ligi ya Spain. Pia, federation ina ligi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Tanzania, nampongeza Mheshimiwa Leodegar Chila Tenga kwa kuanzisha bodi ya ligi ndani ya Idara ya TFF na imekuwa nzuri. Toka ilivyoanzishwa mwaka 2008 ilikuwa imeanzishwa ikiwa chini ya Idara ya TFF lakini malengo yalikuwa baadaye ije ijitegemee kama zilivyo Bodi ya Ligi ya Uingereza na Bodi ya Ligi ya Spain. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa bodi yetu bado iko chini ya TFF. Tunaomba Mheshimiwa Waziri aiboreshe bodi hii, iwe independent na ijitegemee. Tumeona bodi ambayo haijisimamii; asubuhi inatoa matamko haya, jioni inatoa matamko haya. Hii inaonesha nyuma ya pazia bodi inasukumwa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri bodi hii ijisimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu Ligi Kuu ya Uingereza inasimamiwa na Bodi ya Ligi Kuu ya...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali…

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Naam!

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali, wewe ni Mbunge mzoefu. Usiliingize Bunge kujadili vitu ambavyo bado havijafika rasmi…

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, vitu gani?

NAIBU SPIKA: Kanuni ya 81 inakataza kujadili au kutuhumu mtu au chombo ambacho hakina nafasi ya kuja kujitetea wakati wewe unasema… (Makofi)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali!

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa.

NAIBU SPIKA: Kanuni ya 84. Ukikataa maelekezo ya Kiti au Spika, unashtakiwa kwa kanuni kwa kosa la kukosa nidhamu…(Makofi/Kicheko)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika…

NAIBU SPIKA: Ukipinga Kanuni ya 84 unakwenda 85, ndiyo mbaya kabisa, hata Ubunge hutagombea. Usituhumu chombo chochote… (Kicheko)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika…

NAIBU SPIKA: Ninakuomba, mimi nakusaidia tu. Kuna kesi ilitokea hapa ya Mheshimiwa mmoja mkubwa na Mbunge humu ndani kuzungumza vitu ambavyo unatoa maamuzi na unalalamikia maamuzi yaliyofanywa. Wewe hukuwa sehemu ya hicho kikao, na mimi kwa kukaa hapa naweza nikaingizwa kwenye kesi yako. Punguza munkari, changia mambo ambayo una uhakika nayo. Endelea.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba muda wangu ulindwe. Nazungumzia muundo wa bodi zetu za ligi zilivyoanzishwa. Ukienda Uingereza kuna bodi ya ligi inayojitegemea inaitwa EPL… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali!

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Spain kuna bodi ya ligi inayojitegemea… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali, haya makofi hayatakusaidia… (Kicheko)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sizungumzii huko. Nazungumzia jinsi…

NAIBU SPIKA: Utakapopelekwa kwenye kikao cha nidhamu haya makofi hayatakusaidia. Hawa wote watakutazama tu. Unapuuza maelekezo ya Kiti, unalalamikia maamuzi ambayo siyo sehemu yetu hapa. Endelea. (Makofi)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea maelekezo, lakini silalamiki. Nazungumzia muundo wa bodi za ligi duniani… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Umezungumzia bodi hii inatoa…

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninazungumzia Bodi ya Ligi ya Uingereza.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali, umezungumzia bodi hii asubuhi inasema hivi, jioni inasema hivi. Ndiyo ulivyosema. It is recorded.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Ligi ya Uingereza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)