Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee naomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa maendeleo makubwa ya michezo na sanaa ikiwemo ongezeko kubwa katika ukuaji uchumi na mchango katika pato la Taifa na pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Mbunge na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa Kimataifa (national competitiveness).
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na majirani zetu Kenya na Uganda, kwa maandalizi ya kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) ambayo yataanza Juni, 2027. Mafanikio mazuri yamefikiwa katika ujenzi na uboreshaji wa viwanja, viwanja vipya vilivyopangwa kujengwa Arusha na Dodoma na pia viwanja vya Zanzibar na Mwanza ikiwemo kuboresha viwanja vya Benjamin Mkapa, Uhuru vya Dar es Salaam na Aman Stadium na Gombani vya Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna maandalizi mazuri ya kuboresha viwanja vya kufanyia mazoezi na kuna maandalizi mazuri ya mahoteli, hospitali na miundombinu ya barabara na mawasiliano na vifaa vingine kwa ajili ya kuandaa michuano ya CHAN 2025 na AFCON 2027.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali kuchukulia michuano ya CHAN 2025 na AFCON 2027, kuwa ni fursa muhimu za kuijenga Tanzania vizuri zaidi katika ramani ya dunia na hususan fursa za kiuchumi ikiwemo utalii. Ninapendekeza taasisi hasa za utalii, kuchangamkia fursa hii kwa kuwekeza vivutio zaidi na kuhakikisha tunakuwa na sehemu kubwa ya soko na biashara zitakazozalishwa na michuano hii ya CHAN 2025 na AFCON 2027.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yote panapojengwa na kuboresha viwanja vitavyotumiwa na mashindano haya, iendane na kuboresha miundombinu ya barabara, maji, umeme, mawasiliano na hata huduma za mahoteli, migahawa, biashara mbalimbali na hata sehemu za burudani.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwapongeza wanamichezo wote kwa kufanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa. Kwa namna ya pekee napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hamasa na msukumo alioweka katika michezo yote na hasa mafanikio makubwa ya timu zetu za Yanga na Simba katika mashindano ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup).
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuwapongeza Klabu ya Simba kwa kujiwekea rekodi ya kuingia fainali za ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup). Kutokana na hamasa ya Mheshimiwa Rais, Klabu za Yanga na Simba zimeandika historia na kuipa nchi yetu heshima kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inastahili pongezi kwa mkakati wake katika kuimarisha, kuziwezesha na kufanikisha ushiriki wa timu za Taifa na vilabu katika michezo na michuano mbalimbali ya Kimataifa na kikanda. Kama sehemu ya mkakati huo, Wizara iweke msukumo zaidi wa kuhamasisha kujenga, kukarabati na kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo hususan vya mpira wa miguu.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanja vingi vya mikoani vipo katika hali mbaya na kwa kiasi kikubwa ni sehemu ya changamoto katika maendeleo ya michezo nchini. Michezo na sanaa ni muhimu sana katika kujenga sura na sifa ya Taifa letu (Nation brand). Hivyo ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha inaweka umuhimu mkubwa wa ushiriki wa timu zetu za Taifa na kuwepo kwa mkakati wa Kitaifa wa kuhakikisha timu zetu za Taifa na vilabu zinafanya vizuri kwenye mashindano ya kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati huu katika michezo na sanaa ni nguzo muhimu katika kutekeleza Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026. Serikali itenge bajeti ya kutosha kuhakisha tija katika ushiriki wetu katika mashindano ya Kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na kuboresha miundombinu ya viwanja, Wizara ijikite katika kuibua vipaji mbalimbali vya michezo na sanaa kwa kuimarisha ushirikiano na Wizara nyingine hususan Elimu na TAMISEMI. Pamoja na kutokuwepo kwa miundombinu rafiki, mikoa mingi imekuwa inatoa wachezaji wenye vipaji vikubwa katika mpira wa miguu, riadha na hata sanaa mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, umefika muda sasa wa kuwepo kwa mkakati wa kuibua na kuendeleza vipaji hivyo ambavyo vimekuwa vinaonekana kikanda zaidi kama vile riadha kwa Mikoa ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Mikoa ya Kati. Pia kwa upande wa mpira wa miguu kumekuwepo na mikoa kadhaa ya vipaji vikubwa, na huko ndiyo Serikali iweke msukumo zaidi wa kuibua na kuendeleza hivyo vipaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata kwa wasanii, kuna mikoa imekuwa inatoa idadi kubwa ya vipaji kwenye uigizaji, uimbaji ikiwemo nyimbo za Injili ambazo zinapata umaarufu sana duniani. Kutokana na vipaji vingi vya michezo hususan mpira wa miguu na riadha, napendekeza Shule ya Sekondari Santilya ya Wilaya ya Mbeya iongezwe kwenye orodha ya shule teule za michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa Kiswahili, kuwa lugha rasmi Kimataifa, napendekeza uwekezaji zaidi katika kuitangaza na pia kuwezesha ulimwengu kujua kuwa mizizi na ustawi wa Kiswahili ni Tanzania pekee na wengine wanaigiza kwetu. Serikali iendelee kuchukua hatua zaidi ya kukistawisha Kiswahili katika Mataifa mengine Barani Afrika na kwingineko kwa kushirikisha vyuo vikuu hapa nchini na vyuo vikuu mbalimbali duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.