Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Shabani Hamisi Taletale

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nampongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kile anachokifanya kwenye Wizara hii ya Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona juzi ameongeza pia bajeti kuwapa watu ambao wana changamoto, maana Mkoa wetu unaongoza kwa mafuriko. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuletea kaka yangu huyu wa Kizaramo Mheshimiwa Ulega. Mheshimiwa Ulega ni Waziri ambaye anaingia site na sasa hivi wakandarasi wanapungua vitambi, maana ukiwa unanenepa hutakiwi kudaiwa. Kwa hiyo, kwa kifupi Mheshimiwa Ulega, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Morogoro Kusini Mashariki tunaendelea kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kile alichokifanya katika barabara yetu ya Ubena - Zomozi. Mkandarasi yupo site, pesa imetoka, tunashukuru Mungu Alhamdulillah. Hili ambalo tunaweza kulisema kwa kuisemea Wizara, leo hii tunaona wenzetu wakifurahia barabara, lakini sisi wana Morogoro Kusini Mashariki, huu upande wetu wa Bigwa – Kisaki; mimi ninakaa kiti karibu na Mheshimiwa Spika, nilibahatika kuona namba yangu amei-save vipi? Ameni-save Bigwa - Kisaki, kwa sababu miaka mitano nalilia barabara tu. Kaka yangu Mheshimiwa Ulega wewe ni mtu wa vitendo, tayari kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kitendo cha wewe kuelekeza pesa zije pale, barabara ianze ndugu yangu. Kaka Ubunge naupenda huu; kazi naitaka hii; wananchi wa Morogoro Kusini Mashariki wanataka barabara ya Bigwa – Kisaki. Haiwezekani miaka mitano naongea neno moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi ina Rais msikivu, ametupa kilometa 78 na ameruhusu pesa ije. Mheshimiwa Ulega shida ipo wapi? Unanasa wapi? Mimi nakuona mwamba, jembe kabisa, lakini hapa unakwama wapi Mheshimiwa Ulega? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba, leo naondoka na shilingi ya Mheshimiwa Waziri, nakwenda nayo Kusini Mashariki, watanirudisha kama akisema analeta barabara. Maana kuna vitu unaongea mwishowe; mimi kuna siku nakaa na Spika hapa nilivyojiona ameni-save Bigwa - Kisaki nikajiuliza, hivi ni kero au anavutiwa na ninavyochangia kila siku?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kitu kimoja kwa kaka yangu Mheshimiwa Ulega, anionee huruma. Sijaja humu ndani hata siku moja kuchangia chochote. Wanamorogoro Kusini Mashariki wanataka barabara ya Bigwa - Kisaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza kwenye hii Wizara kaka yangu Mheshimiwa Ulega; upande wa Mkurugenzi wa TANROADS, brother mtu poa sana. Kaka siyo kama nakujaza, Mkurugenzi wa TANROADS mwambie Waziri wako Bigwa - Kisaki wanataka barabara. Mkandarasi anataka 75 percent tu ili aingie site. Twendeni site jamani, shida ipo wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najua Mheshimiwa Waziri ana Mkurugenzi mzuri na mambo yataenda, kama alivyokuwa na Mkurugenzi mzuri baba yangu Kondoro wa TBA, ukimtazama mvi na anavyoongea ni vitu viwili tofauti. Ana Mkurugenzi Mnyawezi. Sisemi kwa sababu ni baba mwenye nyumba wangu wa TBA, lakini nasema kwa sababu he has a good heart. Alishawahi kuniita siku ya kwanza akaniambia, uongozi ni kuweka rekodi, kapambane uweke rekodi. Rekodi yangu mimi ni kuhakikisha Bigwa - Kisaki inakuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nikishindwa kuchukua neno la baba yangu Kondoro la kuweka rekodi ni kwa sababu ya Mheshimiwa Ulega na Mkurugenzi wake wa TANROADS. Nawaomba, leo hii mimi nipo kwenye orodha ya wale ambao watakaoshika shilingi yake mpaka nijue hatima ya barabara yetu ya Bigwa – Kisaki, kwa sababu haiwezekani over five years mimi niko hapa Bigwa – Kisaki. Mtu mwingine wa nje anashangaa yule hajui kuongea au! Nitaomba nini hatuna barabara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Rais ametuletea barabara za ndani zote, kwetu sisi vitu vilivyoletwa kwetu kwenye Jimbo la Kusini Mashariki natembea kifua mbele, mimi ndio Mbunge na nitaapa pale mwezi wa 11, na ninatembea nikiamini Chama cha Mapinduzi kitashinda kwa kishindo na Mheshimiwa Rais atashinda kwa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe, hili ni ombi langu mimi na wana Morogoro Kusini Mashariki.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Taletale.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Taletale, nakushukuru sana.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.