Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake mbalimbali katika Taifa letu, hususan ustawi wa kijamii kisiasa, kiuchumi, amani, kidiplomasia na mshikamano. Hali hii imetuweka nchi yetu kuwa kisima cha amani mbele ya Mataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuungana na wananchi wote wa Jimbo la Mbulu Mjini kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoliongoza Taifa letu na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025, Mwenyezi Mungu ambariki pamoja na Serikali yake nzima ya Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Prof. John Mwaluko Kabudi, Waziri wa Wizara, Naibu Waziri Mwinjuma na watendaji wote wa Wizara hii kupitia hotuba ya mapendekezo ya maombi ya mapato na matumizi 2025/2026 kama ilivyowasilishwa mbele ya Bunge letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wajumbe wote wa Kamati kupitia taarifa yao waliyowasilisha mbele ya Bunge letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mapendekezo hayo mawili ya Wizara na Kamati. Kwanza, Serikali iandae kalenda/ratiba ya michezo kupitia Kamati za michezo ambazo Mwenyekiti wa Wilaya ni Katibu Tawala na Mkoa ni Katibu Tawala wa Mkoa kuunganisha na ngazi ya Taifa ili kubaini na kutangaza vipaji kwa vijana wetu walioko ngazi za kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Kamati za Michezo za Wilaya na Mikoa hazina majukumu kabisa na mipango kazi inayoonesha muundo wake, majukumu, hali inayopelekea wanamichezo wengi vijijini kucheza kama burudani wakati kuna vipaji vingi vya michezo katika makundi hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendeleza miundombinu ya viwanja vya michezo kwa ajili ya mashindano ya AFCON. Hatua hiyo ni kubwa sana kwa Taifa letu, hivyo basi, tuendelee kujenga miundombinu hiyo ya michezo katika ngazi za mikoa na wilaya kama vile uwanja wa michezo wa Mwalimu Nyerere Stadium ulioko Wilaya ya Mbulu, Mkoani Manyara ambao ulitumiwa na timu kutoka mikoa ya Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa huko nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, basi tunaiomba Serikali yetu itafute fedha za kukarabati uwanja ule. Kwa kweli hali ya hewa ya Wilaya ya Mbulu ni nzuri sana kwa michezo, na tuna hazina nyingi za vijana wenye vipaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba sana Serikali yetu ijitahidi kupeleka fedha zinazoombwa kwenye bajeti ya Wizara hii muhimu sana kwa kuwa sekta ya michezo nchini itachochea ajira kwa kundi kubwa la vijana wengi walioko mitaaani ambao Mwenyezi Mungu amewajalia vipaji vingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, na ninaomba kuwasilisha.