Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara ya Ujenzi bajeti ya mwaka 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana na kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambazo anaendelea kuzifanya ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba nijikite ndani ya Mkoa ninaotoka, Mkoa wa Manyara katika Wizara hii ya Ujenzi. Kwanza tuendelee kupongeza kazi kubwa ambazo zinafanywa na Wizara hii ya kuendelea kuhakikisha kwamba barabara zetu zinaendelea kupitika, licha ya changamoto kubwa ya mvua inayoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara una jumla ya takribani barabara za TANROADS kilometa 1,657, lakini kilometa ambazo zina lami ni kilometa 257; kilometa ambazo hazina lami, ambazo ni changarawe ni kilometa 1,400. Utaona ni kwa kiwango gani bado tuna uhitaji mkubwa wa kuunganishwa na mtandao wa barabara, licha ya barabara kuu ambazo zinazounganisha nchi yetu ya Tanzania kati ya Mkoa wa Manyara na Mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu wananchi wa Manyara ni kwamba tuna barabara ndani ya Mkoa ya kuufungua Mkoa ili kuondoa kupita Wilaya, kutoka Simanjiro kuja kupitia Arusha kwa ajili ya kuja Manyara. Tunaomba sana tuzingatiwe, kwani upembuzi yakinifu umeshafanyika. Tunaomba tuwekwe kwenye bajeti ili sasa tusipite mkoa mwingine kwa ajili ya kuja kupata huduma ndani ya Mkoa wa Manyara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ambazo tunaomba zifunguliwe sasa ni barabara ya kutoka Babati kuja Kiteto kwenda Simanjiro kwa maana ya Orkesumet. Hii itakuwa imesaidia sana kuufungua Mkoa wa Manyara na kuendelea kuhakikisha kwamba kilometa hizi 1,400 tunaanza kuzipata kwa ajili ya kutengenezewa barabara ya lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuendelee kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ya ujenzi wa madaraja ambayo imefanyika; daraja la Katesh, daraja la Dabili, daraja la Msasani, daraja la Minjingu na daraja la Losinyai kule Simanjiro. Kazi hizi zinaendelea, lakini tunachokiomba ni fedha ili kazi hizi zilizosimama kwa sasa ziweze kuendelea. Fedha itolewe ili madaraja haya yaweze kupitika na wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kilometa 257 ambazo nimezisema za lami ndani ya Mkoa wetu wa Manyara, bahati mbaya sana miongoni mwa lami hiyo ni lami inayotoka Singida kuja Arusha, ambacho kimsingi kama umepita njia hiyo ni njia muhimu sana kwa wakazi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, kwa sababu wanatumia barabara hiyo kutoka Arusha kwa maana ya kuja kupita Manyara kuelekea Singida na kwingineko kwa Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitokea Dar es Salaam kuja Arusha, sehemu korofi iliyoharibika ni kipande cha Mkoa wa Manyara ambacho kinaanzia Dareda kinakuja Masakta – Masqaroda – Endagau - Endasak – Nangwa - Measkron, kinakuja mpaka Katesh, tunakwenda Mogitu - Gehandu ndani ya Wilaya ya Hanang ndicho kipande kikubwa ambacho kimeweza kuharibika na kukatika sana, na wakati wote imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba ukarabati ufanyike walau wa dharura ili kuweza kunusuru ajali ambazo kwa sasa zinapatikana kwa sababu ya mashimo makubwa ambayo yamejitengeneza katika kipande hiki cha barabara nilichokitaja kutoka Dareda kwenda Gehandu mpaka Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuishukuru sana Serikali, kwani mwaka 2024 kwenye Bajeti ya 2024/2025 ulisainiwa mkataba wa kilometa saba za lami Kipande cha Dareda Center mpaka Dareda Mission. Kazi hiyo mpaka sasa hivi haijaweza kuanza na barabara ilishasainiwa mwaka 2024 katika Bajeti ya 2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sasa kazi hiyo iweze kuanza ili kile ambacho kilisainiwa na kilikusudiwa kiweze kwenda kufanya kazi na kuleta tija kwa wakazi wa Manyara kwa sababu, tunachokiamini ni barabara kubwa ambayo inatumika kufungua uchumi wa maeneo mengine kwa sababu, malori na bidhaa nyingi zinapitia pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, tunaomba Barabara ya Mogitu – Haydom iweze kujengwa kwa kipande cha lami, lakini pia, Barabara ya Nagwa kuja Kondoa iweze sasa kutengewa fedha kwa ajili ya lami, kwa sababu upembuzi yakinifu umeshafanyika na kazi hii kubwa ndani ya Mkoa wa Manyara, hususan Wilaya ya Hanang, kama ambavyo nimeitaja, iweze kwenda kufanyiwa kazi kwa sababu, wananchi wana imani kubwa sana na Serikali yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. (Makofi)