Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, Naibu wake Mheshimiwa Hamis Mwinjuma, Katibu Mkuu Ndugu Gerson Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Methusela Mtonda, wataalamu wa Wizara na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kazi nzuri wanayofanya kuboresha utendaji katika sekta hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita kwenye umuhimu wa kuwekeza katika tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza nchini Tanzania. Filamu na michezo ya kuigiza huweza kutumika katika jamii kuelezea tamaduni zetu, kuibua hisia fulani kwenye jamii, kutoa elimu za kimaadili, burudani na kujiingizia kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu huo, tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza kama zitachukuliwa kwa umakini mkubwa, zinaweza kuwa chanzo bora na muhimu katika kulijenga Taifa letu na zinaweza kutumika kama jukwaa la mafunzo la kuchochea mijadala nchini kote.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii inaweza kuwa kichocheo kikubwa kwenye kukuza uchumi wa Taifa letu na mtu mmoja mmoja. Kwa mfano, filamu ya The Royal Tour iliyotengenezwa kuonesha vivutio vya utalii katika Taifa letu imekuwa mkombozi katika sekta ya utalii hapa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na umuhimu wa tasnia hii, miaka ya hivi karibuni tumekumbana na wimbi kubwa la kushuka kwa tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza hapa nchini Tanzania ukilinganisha na nchi kama Nigeria na South Africa ambao wapo vizuri sana kwenye tasnia hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kudidimia kwa tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza hapa nchini, wananchi wengi wa Tanzania wameishia kupata burudani kutoka kwa wasanii wa nchi nyingine kama Nigeria na Afrika Kusini. Kwa mfano, Watanzania wengi hupenda kufuatilia kipindi cha tamthilia cha wasanii wa Afrika Kusini kinachorushwa na Azam TV. Upenzi wao unatokana na umakini wao na kuigiza mambo ya misisimko, mafunzo na ya kipekee katika jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiuhalisia, tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza hapa nchini bado ipo nyuma sana na Serikali yetu ni kama imeipa kisogo na kugeukia michezo wa mpira wa miguu ambao hauhitaji sana teknolojia za kisasa. Hivyo basi, kutokana na ukosefu wa ajira hapa nchini, ni vyema Serikali ikaja na mkakati wa kuhamasisha vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi wa wasanii waliong’ara hapa nchini ni pamoja na Stephen Kanumba, Ramadhani Mkieti (Sharo Milionea) na wengine wengi. Taifa letu likiwa na mipango madhubuti, tunaweza kukuza tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza na kufikia kiwango kizuri na kuzalisha wasanii wakubwa na maarufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hili kwa sababu katika nchi yetu, tumebarikiwa kuwa na wahitimu wengi waliosomea tasnia ya sanaa na utamaduni ikiwepo masuala ya filamu na michezo. Kama wasomi wetu hawa watatumika vizuri, baada ya kumaliza masomo yao, watasaidia sana kuendeleza hii sanaa waliyosomea na kulipatia faida Taifa na wao wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla na kiwango kikubwa, waigizaji wetu wengi wamekuwa wanatumia lugha ya Kiswahili kwenye kutengenezea filamu na kuigiza hapa nchini. Filamu hizi zinapendwa sana katika nchi za Afrika Mashariki kutokana na kuwa zinatumia lugha adhimu ya Kiswahili. Nje ya jumuiya ya Kiswahili, filamu hizi hazina soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wakati muafaka sasa kujiongeza na kuzalisha filamu kwa kutumia lugha za Kiingereza kama wanavyofanya nchini nyingine za Afrika zikiwemo Kenya na Nigeria ambapo kwenye tasnia zao za filamu na michezo ya kuigiza hutumia lugha ya Kiingereza na kuchanganya na Kiswahili au lugha ya kienyeji kidogo na kufanya filamu hizo kupata soko la ndani na la Kimataifa. Kwenye haya Mataifa, Kiingereza kinatumika kama lugha ya biashara Kimataifa ili kupata soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu, napendekeza yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Serikali iwekeze kikamilifu kwenye Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Tanzania ili waweze kuandaa, kuratibu na kuendesha warsha, vikao, mijadala na mafunzo ya kujenga uwezo kwa wadau wa filamu hapa Tanzania. Pia uwezeshaji huo utawasaidia kutafuta fursa katika sekta na kuziwekeza kwa wadau na kuratibu uibuaji vipaji kupitia michezo ya kuigiza na filamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ili kuiendeleza sekta ya filamu, Serikali kwa kushirikiana na wadau wanapaswa kulisaidia Shirikisho la Filamu Tanzania ili kuwawezesha watayarishaji na wasanii kupata mafunzo ya kitaalamu kwa njia ya warsha na semina ili kuongeza uwezo wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, Serikali ifanye uwekezaji wa kimkakati katika tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza. Hii ni pamoja na kujenga studio za kisasa za uzalishaji wa filamu na zenye ubora. Miundombinu ya filamu hapa ni duni sana. Wasanii wetu wapewe fursa ya kutumia studio hizi hata kwa kuchangia gharama kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, Serikali ije na ajenda mahsusi ya Kitaifa kuhusu tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza itakayowahusisha wadau wote ikilenga kujenga uzalendo na kuifufua tasnia hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tano, Serikali iwekeze nguvu kuingiza nchini teknolojia mpya kwenye tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza kwa kuweka mazingira rafiki ya kikodi. Teknolojia hizi ziletwe kutoka kwenye Mataifa yaliyo mbele zaidi kimaendeleo katika tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sita, Serikali iwekeze kimkakati kwenye kuandaa wataalamu mahiri wa kutayarishaji na kuunda filamu na michezo ya kuigiza. Wataalamu hawa wawe na ubobezi katika ubunifu, matumizi ya lugha (Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu) na matumizi ya vifaa vya kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya upungufu wa wataalamu hasa katika lugha ni changamoto inayoturudisha nyuma zaidi katika tasnia ya filamu nchini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wadau wa ndani au Kimataifa hutazama zaidi lugha ili kupata ujumbe ulioko kwenye filamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, saba, Serikali iendelee kuboresha sera, sheria pamoja na kanuni za kusimamia filamu na michezo ya kuigiza Tanzania Ili ziwanufaishe wasanii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kushauri kwamba ni vyema wasanii wetu wakajikita zaidi katika kuzalisha filamu zinazotoa elimu kwenye changamoto zinazosumbua Taifa na ulimwengu kwa ujumla kama zile zinazogusa hisia za watu. Kwa mfano, filamu zinazohusu utekaji wa watoto, ubaguzi wa rangi na jinsia, udhalilishaji wa akina mama, watoto na akina baba, na fursa mbalimbali zilizopo hapa nchini. Ni vyema filamu na michezo ya kuigiza kutoka kwa wasanii wetu ziwe na maudhui ya heshima na ya kuijenga jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.