Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nichukue nafasi hii awali ya yote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kaliua. Nianze kwa kuipongeza Wizara hii ya Ujenzi chini ya Waziri, Mheshimiwa Ulega, kwa kazi nzuri zinazoendelea katika nchi yetu. Pili, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa miradi mikubwa sana aliyoileta katika nchi yetu na anayoendelea kuitekeleza, hususan katika Jimbo langu la Kaliua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Kaliua napongeza kwa sababu zifuatazo: Moja, Kaliua tumekamilisha ile barabara ya kwenda Kigoma kilometa 38 ambazo zina thamani ya shilingi bilioni 38. Pili, Kaliua tulikuwa tuna ujenzi wa barabara ya kutoka Uganza ambapo Mheshimiwa Waziri alikuja kama Waziri wa Mifugo kipindi kile; akija sasa hivi inawezekana akapotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uganza kwenda Usinge tumekamilisha kilometa 7.5 zenye thamani ya shilingi bilioni 11.6. Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana wewe kwa usimamizi mzuri, kwa sababu, tayari taa za barabarani zimeshawaka hivi tunavyoongea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mtendaji Mkuu wa Mkoa, Mlimaji anafanya kazi nzuri sana. Hii ni awamu yangu ya pili kwa sababu, mwaka 2024 nilisema hivi hivi kwenye bajeti hii na wakati nasema zile kilometa 7.5 zilikuwa hazijajengwa. Sasa nasema kwa sababu zimekwisha, taa zimewekwa na nina kila sababu ya kusema vijana kama hawa mwaangalie kwa macho mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Kaliua Mjini kuna by pass pale, kilometa nne zimekwisha, taa za barabarani zimewekwa na kilometa 1.5 iliyokuwa imebaki tayari, Mkandarasi Samota General Construction, kilometa 1.5 mkataba umeshasainiwa. Ninaamini ndani ya wiki hizi mbili ndugu zangu wa Ushokola kwenda Relini kazi itakwenda kama inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maombi kwa Mheshimiwa Waziri. Kwanza wananchi wa Usinge, Uganza, Kaliua, wanahitaji kumwona akienda kuzindua ile barabara ya kilometa 7.5, kwa hiyo, namkaribisha. Alikuja kama Waziri wa Mifugo, sasa aje tuchinje ng’ombe tule na wananchi wa Usinge kwa ajili ya ukamilishaji wa ile barabara. Ila ombi lao wananchi wa Usinge, wanasema taa za barabarani zimewekwa mbali, kuna upungufu kidogo. Naomba tuongezewe angalau taa 20 pale ili Mji wetu wa Uganza, Usinge, ukae vizuri zaidi, nami namwamini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo nilikuwa nataka kuliomba, kama ombi maalum, ni barabara yetu ya kutoka Mpanda, Kaliua mpaka Kahama. Barabara ile ni ya kiuchumi. Leo nimekuja na ushauri huu, najua wanaendelea na upembuzi yakinifu, kwamba, kwa sababu ule mji tumejikuta vinabaki vile viraka vya TANROADS, hasa kutoka pale Ushokola kama unaenda Zugimlole, TARURA tunapiga lami zetu huku tunakutana na kile kipande ambacho kinakuwa bado kwa upande wa Ushokola. Nawaomba zile kilometa mbili tuwekewe ili kuwe na muunganiko mzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, barabara hiyo hiyo ya kuelekea Kahama siyo lazima tuanze kwa kasi. Kwa sasa, ninashauri, twendeni taratibu kama inawezekana. Kwa mfano, tuanze na kilometa 10 kwenye Bajeti ya 2025/2026 kuanzia pale Kasungu kwenda Kazaroho kwenda Igwisi tukiwa tunaelekea Ulyankulu. Tutakapomaliza upembuzi yakinifu, mambo yakakaa vizuri, ninaamini mambo mazuri yatakuja, ninaamini Serikali yangu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kaliua ahadi yao ni kumpigia kura za kutosha, nyingi sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na wana imani na mimi Mbunge wao, Mbunge wa vitendo. Wanaamini kazi nzuri na kuwasemea na Madiwani wangu wa Chama cha Mapinduzi kule mambo ni bambam. Huyu ndio Mheshimiwa Dkt. Samisa Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa ambalo mimi nashauri ni kuhusiana na malipo ya wakandarasi, yanatukwaza kwa sababu, wale tuna mahusiano nao, ni ndugu zetu, ni jamaa zetu. Wanapokuwa hawajalipwa na wamekopa benki, interest inakuwa kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, katika eneo ambalo ataonekana ame-perform pia, ni kuwasaidia wazawa wetu. Naomba kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja, ahsante sana. (Makofi)