Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja iliyoko Mezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hoja hii kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna alivyoinua michezo nchini kwa uhamasishaji wake uliokwenda sambamba na utoaji wa fedha zilizoleta mabadiliko chanya katika sekta ya michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na management nzima ya Wizara kwa kazi kubwa na nzuri ambayo Wizara imefanya katika kuinua michezo na kuleta hamasa kubwa kwa wasanii, hongereni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua nchi yetu itakuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027. Mpango wa Wizara ni kuwa na viwanja vitano vitakavyotumika katika mashindano ya AFCON. Mbali na ujenzi wa viwanja vipya hivyo vitano, moja ya viwanja ambavyo vilikusudiwa kutumika katika michezo hiyo, ni pamoja na uwanja wa CCM Kirumba ambao ulitakiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa ili utumike aidha, kwa mazoezi au kwenye mashindano.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa Wizara iko kimya kuhusiana na ukarabati wa uwanja huo. Napenda kujua suala hili limefikia wapi? Naomba utekelezaji wa suala la ukarabati ufanyike mapema ili uwanja huo utumike katika mashindano hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naunga mkono uanzishwaji wa mamlaka/taasisi itakayosimamia viwanja vya michezo nchini. Nashauri taasisi hiyo itakapoundwa isihusishe viongozi wa michezo, bali ijitegemee kabisa ili kuepuka mwingiliano wa kiutendaji ili kuleta tija katika utendaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu ni kutaka kujua suala la maandalizi ya kuwa na vazi la Taifa imefikia wapi? Kama imeshindikana tufahamishwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho japo siyo kwa umuhimu Serikali iangalie kwa mapana tamaduni zetu. Kumekuwepo na utamaduni usiokidhi au unaokiuka maadili ya Kitanzania. Ngoma zinazochezwa sasa hususan Ukanda wa Pwani zaidi sana Dar es Salaam, wanakiuka sana maadili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, Wizara itupie macho tamaduni hizi ambazo zinaaibisha sana na kukiuka maadili ya Mtanzania. Hivi karibuni baadhi ya wasanii hao walikwenda Kenya na kujinasibu kuwa huo ulikuwa ndiyo utamaduni wa Mtanzania. Yaliyojiri baada ya onyesho lao, ni aibu kwetu kama Watanzaniaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.