Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa wasaa huu kuchangia Bajeti ya Wizara ya Ujenzi. Cha kwanza, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ametekeleza kutuletea fedha zetu katika miradi ya maendeleo katika Jimbo la Songwe, siyo barabara, lakini katika miradi yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima, naomba leo nichangie kwa upole mkubwa sana na ninaomba Mheshimiwa Ulega anisikilize, ni juu ya barabara yangu ya lami. Toka nimeingia Ubunge mwaka 2010 nimekuwa nikiililia barabara hii ya kutoka Mbalizi – Mkwajuni mpaka Makongorosi. Tumekuwa tukiongea kila mwaka na kila mwaka kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ipo, zaidi ya miaka saba sasa, lakini hakuna kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 2023 tuliiingiza kwenye bajeti wakasema ingefanyika, lakini hewa. Mwaka 2024 tumeiingiza kwenye bajeti, lakini mpaka sasa tunaenda kumalizia muhula bado sijapata chochote. Mheshimiwa Ulega, angalia Wabunge wenzangu wanavyochangia, wanavyoshukuru, kwa ajili ya barabara zao za lami, lakini katika nchi nzima unaweza ukasema nimebaki peke yangu. Ni barabara ya kutoka Mbalizi kwenda Wilaya ya Songwe. Wilaya ya Songwe ni mpya, lakini sina lami. Mheshimiwa Ulega wewe ni rafiki yangu, tumeingia Ubunge pamoja, hebu naomba uliangalie kwa umakini sana jambo hili, sina barabara ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara mwaka 2024 kwenye Jimbo langu akaahidi kwamba, angeweza kunipa lami lakini…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi?

TAARIFA

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampa Taarifa mzungumzaji, asiseme kwamba ni yeye tu. Mimi pia Nyang'hwale; kutoka Kahama – Nyang'hwale – Busisi, barabara hii zaidi ya miaka 15.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa unapokea Taarifa?

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwomba Mheshimiwa Waziri. Naomba sana jambo hili liangaliwe kwa mapana marefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni madaraja kwenye jimbo langu. Ninalo Daraja la Muheza kwenda Isanzu. Ni barabara ya TANROADS, limeharibika kabisa. Hiki kipindi cha mvua barabara hii haipitiki na vijana wanalala pale mtoni siku tatu wanasubiri kwa ajili ya kwenda kupeleka mifugo yao kwenye masoko huko Isanzu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo Daraja la Magamba kwenda Mpona na lenyewe ni hatari tupu. Mwaka 2025, kwenye Road Board tumejaribu kuingiza kwenye bajeti, itakapofika huko kwenye bajeti itakayokuwa inaendelea leo naomba nisikie kwamba, na yenyewe ipo. Otherwise, Mheshimiwa Ulega, nisingependa nishike shilingi yako. Wewe ni kijana, lazima uwe unasikia haya mambo, na unafanya ziara kwenye majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimemsikia Mheshimiwa Waziri alikuwa Mbeya, nikajua labda angenitembelea na pale Songwe, lakini sikumwona. Naomba afike Mkoa wa Songwe na aje Wilaya ya Songwe. Wale wenzetu wa Ileje wana lami, wenzetu wa Mbozi wana lami, kule Momba unapoenda Sumbawanga kuna lami, lakini kwangu kuchepuka hapa Mbalizi kwenda kijijini kule Songwe hakuna lami. Mheshimiwa Ulega, nakuomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho, toka nimekuwa Mbunge tumekuwa tukipitisha barabara zetu ziingie kwenye TANROADS, lakini mpaka leo. Yaani kila siku wanasema kuna hiyo sera ya kuomba maombi barabara zile za TARURA zinazokuwa ni ndefu ziingie kwenye TANROADS, lakini sijawahi kuona hata barabara moja imekubalika ili siku moja na sisi tufanye sherehe ya kusema kwamba, barabara hii ya kutoka Kapalala kwenda Gua angalau imekubalika, kwamba, imeingia kwenye TANROADS au hii karabara ya kutoka Kininga kwenda Ngwala, kwenye mgodi mkubwa, kwenye madini adimu duniani, rare earth, hakuna barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wale wa rare earth na Kampuni ya Mamba, wanahangaika kweli kupeleka mitambo yao kule. Ni madini ambayo Tanzania hapa hayapo, ni madini ambayo Afrika hayapo, yapo China peke yake, lakini yapo kule Ngwala porini. Kwa nini, msitulee barabara ili madini haya tuweze kuyachimba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Eng. Kasekenya anajua na alishafika mpaka kule Ngwala, atakwambia. Tuleteeni barabara basi jamani tujenge uchumi wa nchi yetu. Ni madini makubwa na yana hadhi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki leo dakika ziishe. Ombi kubwa ni hayo mambo mawili; madaraja yangu na barabara ya lami. Wenzangu wanafurahia, amesema Mheshimiwa wa Nyang’hwale hapa, labda kama Wilaya yake ni mpya, lakini mimi kule kwangu ni kwa siku nyingi. Naomba uniletee lami zile kilometa 91 kutoka Mbalizi – Mkwajuni – Saza mpaka Makongorosi. Ahsante sana Mheshimiwa Ulega, nimechangia kwa sauti ya upole, sauti ya Kimungu, najua utakuwa umenisikia. Tumsifu Yesu Kristu. (Makofi/Kicheko)