Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. UMMY A. MWALIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii. Nami nianze kwa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika kuijenga nchi yetu, lakini hususan kuboresha miundombinu ya barabara. Sisi watu wa Tanga Mjini ni moja ya mashahidi wa kazi kubwa nzuri ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri, Mheshimiwa Ulega, Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Kasekenya na timu yake kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya. Wakati naomba kuchangia, Wabunge wameona jina langu, Mheshimiwa Musukuma mtani wangu ananimbia Ummy, Tanga una hoja? Tanga kila sehemu kuna lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazo barabara nne ambazo leo nataka kuziongea hapa. Kwanza ni barabara ya Tanga – Pangani. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Ulega, nilipompigia mara tu baada ya kuteuliwa tulimpa kilio cha kusuasua kwa ujenzi wa Barabara ya Tanga – Pangani, akaja, na tunamshukuru Mheshimiwa Rais akatupatia shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Barabara ya Tanga – Pangani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Mheshimiwa Ulega, ni sasa wamsimamie kikamilifu mkandarasi ili aweze kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Tanga – Pangani kwa wakati, hususan kufidia muda wa takribani mwaka mmoja ambao ulipotea. Kwa nini, tunapigania kukamilika haraka Barabara ya Tanga – Pangani? Siyo tu itasaidia usafiri wa watu na mazao, lakini itaufungua Mkoa wa Tanga kwa upande wa utalii. Tunataka kama vile watu wanakwenda beach za Nyali, Beach za Diyani, tunataka watu waje Beach za Pangani, kwa mdogo wa Mheshimiwa Jumaa Aweso ili tuweze pia, kuvutia watalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara hii ya Tanga – Pangani, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, wakati tunasubiri hiyo lami, kuna kipande cha kutoka Mwahako barabarani mpaka Shule ya Istiqaama, hakipitiki wakati wa mvua. Kwa hiyo, tunaomba angalau wakamwage kifusi wakati ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni barabara ya kuanzia Junction ya Liemba – Kiomoni kwenda Pande - Mjesani hadi Mlingano - Muheza. Ninashukuru Mheshimiwa Shangazi jana aliomba, tunaomba barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami iwe ni bypass ili pia, kuweza kuchukua mizigo mikubwa inayotoka Bandari ya Tanga na Bandari ya Mombasa kwenda ndani na nje ya Tanga. Tatu, ni Barabara ya Mabokweni – Maramba – Bombo Mtoni hadi Kwamndolwa. Tunaomba barabara hii pia, ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba pia, nizungumzie Barabara ya Chalinze – Segera, Chalinze – Tanga. Barabara hii sasa hivi ni nyembamba. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia, amefanya kazi kubwa na nzuri ya kuboresha Bandari ya Tanga. Kwa hiyo, barabara ile haikidhi mizigo mikubwa inayotoka Bandari ya Tanga na Bandari ya jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba ipandishwe hadhi barabara hii iwe ni trunk road, ili sasa iwe na connectivity kutoka mizigo ya Bandari ya Tanga, Bandari ya Mombasa na Bandari ya Lamu ili kwenda kuunganisha na sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia, kuzungumzia kipande kidogo tu cha Barabara ya Mabokweni kwenda Mikweni, kilometa moja tu. Hatuombi lami, lakini basi, tunaomba Mheshimiwa Ulega na mimi nakuamini sana, najua uchapakazi wako, najua uchakarikaji wako, najua jinsi unavyojituma, angalau mkawekee hata kifusi, ili barabara hii ipitike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga ni Jiji, amesema ndugu yangu Mheshimiwa Shangazi. Uwanja wa Ndege wa Tanga siyo mkubwa, kwa hiyo, ndege kubwa hazitui katika Uwanja wetu wa Tanga. Sasa hivi ukitaka ku-book ndege ndogo, zinakuja ndege tano kwa siku na zote zinajaa. Watu wa Tanga pia wanataka kupata ndege hizi anazonunua Mheshimiwa Rais, za ATCL, waweze kurahisisha maisha yao, lakini kuna wawekezaji wa Bomba la Mafuta wanakwenda na kurudi kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Tanga tunaomba kukamilika au kuongezwa kwa urefu, kitaalamu mnasema runway ya Uwanja wa Ndege wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niomba, kwa sisi watu wa Mjini, wakati Mheshimiwa Musukuma ananiambia sihitaji lami, ni kwamba tunahitaji lami, na pia tunahitaji taa za barabarani. Naomba sana, kama vile tulivyofanikiwa kuletewa taa za barabarani kutoka Pongwe. Mheshimiwa Ulega nakushukuru sana mtani wangu Mzaramo, basi naomba zifike mpaka Airport ili sasa mtu akiingia aone kweli, sasa anaingia katika Jiji la Tanga, waja leo kuondoka majaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana Mheshimiwa Ulega, chapaka kazi. Wewe na timu yako, Naibu Waziri, mnafanya kazi nzuri, ahsante sana. (Makofi)