Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ya pekee, ambavyo ameendelea kutusaidia kutupa fedha nyingi kwa ajili ya madaraja hasa Daraja la Sukuma pamoja na Daraja la Simiyu, jumla ya shilingi bilioni 57 zimekuja kwenye madaraja, haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri, ameshika nafasi kwa muda mfupi. Hongera sana, tumeanza kuona na tunaamini kwamba, atafanya kazi kubwa pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu na wengine, Wakurugenzi wa Taasisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nilikuwa ninaomba kushauri Mheshimiwa Waziri, haipingiki sasa kutoka Mwanza mpaka Nyanguge kupanua barabara, kwa sababu, huko ndiko sasa hivi uwekezaji wa viwanda unaendelea; Kisesa, Nyanguge, yote ile ina viwanda vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi foleni kutoka Mwanza mpaka Kisesa ni dakika 40 ndipo unaanza kukimbia. Kwa hiyo, watu wanapoteza muda mrefu kwenda kufanya kazi za kiuchumi. Naomba sana, barabara kutoka Mwanza mpaka Nyanguge upembuzi yakinifu umeshakamilika. Sasa ipanuliwe, kwa ajili ya kuondoa msongamano wa magari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Barabara ya Nyanguge kwenda Lamadi Border, ni barabara ambayo imeharibika kabisa, viraka vinawekwa juu ya kiraka, gharama kubwa inatumika kwa Serikali kuziba viraka na ajali nyingi zinatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba, Mheshimiwa Waziri Ulega yupo hapa na Katibu Mkuu, kwa kweli, hebu waweke fedha kwa ajili ya ujenzi mpya wa barabara hiyo ambayo ni zaidi ya kilometa 100 itakuwa imekamilika. Kwa sababu, wameweka shilingi bilioni 48 za Daraja la Simiyu, sasa kama barabara hiyo kila siku inazibwa viraka na daraja jipya wamejenga, haitaleta maana. Hebu ijengwe vizuri hiyo barabara ili iweze kuendelea. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, naomba mniruhusu nisiruhusu taarifa kwa sababu nina dakika tano. (Makofi)

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Barabara ya kutoka Magu kwenda Bukwimba kwenda Hungumalwa, ambayo mwaka 2024 mlitutengea fedha na mkandarasi yupo kazini, nimpongeze. Aliwapongeza jana wakandarasi wazawa, lakini wapo hoi tabaani, naomba walipeni fedha ili waweze kuendeleza miradi hii kwa sababu, wameanza kusimama. Barabara ya Bukwimba – Hungumalwa imesimama, kilometa 10, mkandarasi yupo kazini. Toeni fedha ili aweze kuendelea na barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Barabara ya Airport – Nyanguge, ili kupungzua jam ambayo ina watu wanaotoka Musoma, na wanaotoka Simiyu kwenda Airport, barabara hii imeanza na kilometa 10 kule Airport. Tungeomba sasa, mwaka huu wa fedha ziwekewe za kutosha ili kuhakikisha kwamba barabara hii inakamilika kutoka Airport mpaka Nyanguge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara ya kutoka Magu – Mahaha ambayo usanifu unaendelea. Tunaomba baada ya kukamilika usanifu, ziwekwe fedha kwa ajili ya ujenzi wa lami. Barabara hii inafungua uchumi wa Wilaya ya Magu kutokea Simiyu. Kuna kipande ambacho tayari usanifu umekamilika, kwenda Bariadi ambako kwa kweli nako uchumi unafunguka kwa ajili ya Mkoa wa Mwanza. Naomba fedha ziwekwe kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo barabara ambazo zina sifa ya kwenda TANROADS, na tumemwandikia na kumpelekea Mheshimiwa Waziri. Tunaomba sasa atume watu wake waje waangalie. Barabara ya Kisesa – Kayenzi ambayo inatoka trunk road kwenda barabara ya TANROADS; ina sifa zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayotoka Matela – Nyakasenge inatoka trunk road inakutana kule na barabara ya TANROADS; hizo zina sifa zote. Barabara ya kutoka Nyanguge – Kisesa B – Kwimba Boda – Barabara Kuu – Barabara ya TANROADS, nayo iingizwe kwenye TANROADS. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara inayotoka Ilungu kwenda Kwimba, ni barabara ambazo zinatoka barabara kuu zinaunganishwa na barabara ya TANROADS. Kuna barabara inatoka Kisamba – Simiyu ni barabara inayotoka barabara kuu kwenda Barabara ya TANROADS. Barabara hizi zina sifa zote. Hata barabara ya kutokea Magu Buhumbi – Kwimba – Lumeji ni barabara ambazo zina sifa ya kuingia TANROADS. Tumeshampelekea Mheshimiwa Waziri, atume watu wake waje wakague kwa sababu zina sifa ya kuingia TANROADS.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakuona unaniangalia, naunga mkono hoja. Dakika tano ni chache lakini Mheshimiwa Waziri ameeshayaelewa haya mambo. (Makofi)