Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pia kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja muhimu sana iliyopo mbele yetu asubuhi hii. Kwa namna ya kipekee kabisa, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazozifanya maeneo yote ya Kusini ikiwemo pamoja na Jimbo la Ndanda. Awamu hii tumeweza kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa zaidi ya 85%. Hii ni kazi kubwa sana ambayo imefanyika katika kipindi kifupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niungane na kumpongeza ndugu yetu Mzee Ebenezer Mwapapo, contractor ambaye ni mzalendo mkubwa sana. Kwa taarifa tu, ni mlipa kodi mkubwa kati ya walipa kodi waliopo Mkoa wa Mtwara na anafanya kazi nzuri. Tumeona barabara nyingi Mkoa wa Mtwara, Mkoa wa Lindi na maeneo mengine amekuwa akizitengeneza yeye, na tunatambua kazi yake kubwa, lakini ni kiongozi mkubwa ndani ya chama na ndiyo msaada mkubwa sana kwenye eneo letu la kazi na tumeshirikiana vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo machache ya kusema hapa. Jambo la kwanza kabisa ni masikitiko yetu baada ya kuondolewa ule mradi wa EPC+F, kwa maana ya ujenzi wa barabara kati ya Masasi – Nachingwea – Liwale, hali imekuwa ni mbaya sana. Sasa hivi kutoka Masasi mpaka kufika Nachingwea kilometa 42 tunatumia zaidi ya saa tatu au nne. Tunaiomba sana Serikali iangalie namna bora ya kufanya ili hii barabara sasa ijengwe. Wananchi walikuwa na matumaini makubwa lakini wameanza kukata tamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa karibuni barabara ya Dar es Salaam – Ngurukuru – Lindi ilikatika, jambo ambalo lilirudisha nyuma sana Mkoa wa Lindi kimaendeleo. Vilevile kulikuwa na hali mbaya sana kwa wakazi wa Mkoa wa Lindi pamoja na Mtwara. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha kwamba daraja lile linajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu tulikuwa tunasema kwamba barabara ile yote inayokuja mikoa ya kusini ni mbovu, inahitaji kujengwa tena upya, tena ijengwe iwe bora zaidi kwa sababu eneo linalojegwa barabara ni karibu sana na bahari. Kwa hiyo, barabara hii imekuwa inaharibika kila mara, tuweke pale tuta kubwa ikiwezekana lakini tutumie utaratibu wa kujenga kwa asphalt kama ilivyo barabara ya Iringa – Mbeya na maeneo mengine. Nadhani mnauona ule ubora unaotakiwa, ndiyo ubora hasa sisi tunaohitaji hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara nyingine ambayo tunajaribu kuishauri Serikali, lakini sioni kama wanaamua kuifanyia kazi kwa uhakika mkubwa sana. Ipo hii barabara inayoanzia Masasi – Nachingwea – Liwale – Mahenge, zaidi ya kilometa 120. Barabara hii pia inaweza kukufikisha Ifakara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kama barabara inayokuja Dar es Salaam inakuwa imekatika, na ni sera ya Chama Cha Mapinduzi ni kuhakikisha mikoa inaunganishwa, lakini Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Morogoro haijaunganishwa. Hii barabara tunayoisema ndiyo barabara bora kwa sababu kwanza ipo nje kabisa ya bahari na siyo rahisi kuharibika kwa sababu hata aina ya udongo ulioko kwenye maeneo yale ni mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo jambo lingine ambalo sisi tumeendelea kushauri kila mara. Serikali mfanye uwekezaji mkubwa sana kwenye Bandari ya Mtwara. Sasa ili Bandari ya Mtwara iweze kuwa na tija ya kutosha pamoja na kusafirisha korosho na mazao mengine ya kilimo, kulikuwa kuna haja sasa ya kukamilisha ujenzi wa reli ya kusini ambayo ina kilometa 1,000 zile zinazotakiwa pale kwa nia ya kupeleka mzigo Bandari ya Mtwara. Tunaweza tukapata chuma kutokea Ligangala na Mchuchuma na pia pamoja na makaa ya mawe kutokea Ngapa na maeneo mengine, ili kuleta tija zaidi pale bandarini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliishauri Serikali, kwa kweli reli ya kusini inatakiwa iwe ndiyo reli mama ya Tanzania. Kwa sababu, kuna malighafi inayopatikana yenye uwezo wa kutengeneza reli nyingine. Sasa tunatengeneza SGR, tunafanya importation ya chuma na vitu vingine, tunatengeneza na hizo reli nyingine, zote tunafanya importation ya chuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatumia vibaya forex, tunaagiza chuma kutoka nje wakati tunacho chuma cha Liganga na Mchuchuma. Naomba niseme kwamba chuma pamoja na makaa ya mawe ni masuala ya muda tu, itafika wakati fulani tena makaa ya mawe hayatakuwa yanatakiwa huko duniani. Kwa nini tusitumie nafasi hii tuliyonayo kuhakikisha kwamba tunatumia hiyo chuma vizuri, tuna-extract na kuitumia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri katika mikakati yake mirefu ahakikishe sasa kwamba Liganga na Mchuchuma, kwa maana ya reli ya kusini inaanza kujengwa mapema kwa sababu kuna watu wanasubiri kwa muda mrefu. Wengine walikuwa wanadai riba zao, lakini hicho kitu hakifanyiki. Ile sasa iwe kama ndiyo reli mama kwa sababu italeta chuma, tuta-extract chuma ambacho kitakwenda kujenga reli nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu madeni ya wakandarasi. Kote kule unapozunguka wakandarasi wanalalamika, hasa zaidi wakandarasi wazawa, wengine wanadai zaidi ya shilingi bilioni tatu na wanatozwa riba na benki…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipatia, lakini kwa msisitizo niseme tuiangalie kwa kina kabisa barabara ya Liwale – Masasi – Nachingwea kwa sababu zinarudisha sana nyuma uchumi wa Wilaya ya Nachingwea.