Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka ya uhai na kutuwezesha kukutana hapa jioni hii ya leo kujadili Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya mwaka 2025/2026.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati kabisa ya moyo wangu, namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini mimi na wenzangu kwenye Wizara hii ambao tunaongozwa na Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi kwa sasa na kuendelea kutuunga mkono na kuonesha kwamba yeye ni mwanamichezo namba moja kwa kuhakikisha tunayafanyia kazi maono yake kwa kuwezeshwa na mkono wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais na ninamwahidi kwamba nitaendelea kuwa mtiifu kwake na kwa nchi hii na nitaendelea kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na akili zangu zote ili kuhakikisha tunayatekeleza maono yake kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nawashukuru wenzangu kwenye Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakiongozwa na Prof. Kabudi kwa ualimu na maelekezo ya mara kwa mara ambayo yanafanya tuendelee kuifanya kazi hii ya wananchi wa Tanzania ambao walikiamini Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi wa 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika nakushukuru wewe kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo chini ya dada yangu Mheshimiwa Husna Sekiboko kwa miongozo na maelekezo yanayofanya tuweze kuifanya kazi yetu kwa ushirikiano mkubwa ambao wanatupa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru familia yangu, mke wangu na watoto wangu pamoja na wananchi wenzangu wa Muheza kwa kuendelea kuniunga mkono, kuni-support, kunivumilia na kunitia moyo hata pale mambo yanapokuwa magumu. Nawashukuru sana na ninawaahidi sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutolea ufafanuzi hoja kadhaa za Waheshimiwa Wabunge ambazo zimetolewa toka asubuhi ya leo kabla sijamwacha Mheshimiwa Prof. Kabudi kuja kuhitimisha hoja yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninazo hoja kadhaa, na sina uhakika kama muda utanitosha, lakini nitakapoishia ndiyo hapo nitakapokuwa nimejaaliwa. Jambo la kwanza, ni ile hoja kuhusiana na Muziki wa Singeli.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge kadhaa hapa wameongea toka asubuhi na wameonesha hisia nyingi kuelezea jinsi ambavyo kuna sintofahamu kati ya Singeli kuwa mziki wa Taifa, lakini hali kadhalika maudhui ambayo yanabebwa kwenye aina hii ya muziki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema ni kwamba, hakuna mtu yeyote aliyesema mahali popote kwamba tunataka kuufanya Singeli kuwa muziki wa Taifa. Kilichotokea ni kwamba Singeli kama muziki ambao umetoka mtaani, umejipigania wenyewe na umejipambania wenyewe, ukifanywa na vijana wadogo ambao wametengeneza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Kwa muda mrefu tuliona kwamba muziki huu umeshika na unakubalika katika maeneo mengi ikiwemo nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi nimewahi kwenda kwenye Maonesho ya Singeli nje ya nchi na muziki huu umekuwa unafanya vizuri sana. Sasa ukweli ni kwamba hakuna mtu yeyote kutoka sehemu nyingine yoyote duniani anayeweza kuja kudai kwamba Singeli ina asili ya kutoka nchini kwao. Kwa hiyo, kimsingi Singeli ina asili ya kutoka Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulichofanya tulikuwa tunajaribu kuwasaidia hawa vijana ambao wamejitengenezea ajira na wamejitoa mtaani kwenye kufanya mambo ya ovyo ili kuhakikisha tunawasaidia kuu-brand, kuu-package na kuu-promote muziki huu. Pia, wakati tunafanya hivyo tuwasaidie pia kuu-sanitize (kuusafisha) muziki wa Singeli. Hiyo ndiyo ajenda yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, uhuni ambao unasemwa uko katika Singeli, ninaamini nikiongea kama mwanamuziki; najua kwamba uhuni uko katika miziki yote na vijana hawa wanahitaji maelekezo na siyo kususwa kama ambavyo tumekuwa tunasema kwa ukali.
Mheshimiwa Naibu Spika, siamini kama kuna Mheshimiwa Mbunge yeyote anataka tuwatelekeze vijana hawa au anataka kuua Muziki wa Singeli, lakini ninachojua ni kwamba wanataka tujaribu kuusafisha muziki huu ili uweze kuwa utambulisho mzuri kwa Taifa letu huku ukiwa unabeba maudhui yanayoweza kuuzika ndani na nje ya mipaka yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wote walioongea kwa hisia sana akiwemo dada yangu Mheshimiwa Esther Malleko kwamba, watupe nafasi tuwasaidie vijana hawa kusafisha muziki huu na muziki huu utakuwa wenye matumaini makubwa hapo mbeleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sasa hivi muziki wa Singeli ndiyo unafanya vizuri hata kwenye mikutano yetu ya kampeni. Kwa hiyo, unafurahiwa na watu wengi na ni jukumu letu kuuelekeza badala ya kuususa na kuunyoshea vidole.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Esther Malleko na wengine wote ambao walisema kwa ukali kuhusiana na muziki wa Singeli, watupatie nafasi ya kufanya hili na sisi tunawahakikishia tutawaongoza vijana hawa na muziki huu utakuwa safi, unaoburudisha badala ya kupotosha maudhui na kupotosha jamii yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili alilisema Mheshimiwa Hamisi Taletale, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki. Lenyewe lilikuwa linahusiana na kadhia ambayo Kampuni ya Azam imeingia baada ya kusimamishwa kuonesha kipindi chake cha vitasa, kipindi ambacho kilikuwa kinaonesha mchezo wa ngumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kusema ukweli mimi binafsi ni mpenzi mkubwa wa mchezo wa ngumi, nami nimecheza ngumi. Azam baada ya kuingia na kufanya udhamini, kwenye mchezo wa ngumi walikuwa wanabadilisha maisha ya vijana wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchezo wa ngumi unachezwa sana uswahilini, unachezwa na vijana wenye hali duni za maisha na ni mchezo hatari kusema ukweli. Baada ya Azam kuingia, wakaubadilishia hadhi. Maeneo ambayo mchezo huu ulikuwa unafanyika yakawa yenye hadhi kubwa, lakini pia mapato ambayo mabondia (wapiganaji) walikuwa wanayaingiza yakawa yameongezeka sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichotokea ni kwamba, kuna bondia mmoja wa zamani akaenda Mahakamani akashtaki kwamba Azam wamechukua idea yake ya kuonesha kipindi cha aina hii na akaiomba Mahakama kwanza alipwe fidia na Azam wazuiwe kuonesha mchezo huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninafikiri proceedings za kesi wengine tuliziona na hazikuwa nzuri sana kwa upande wa Azam kiasi kwamba Azam kweli wakazuiwa kuonesha mchezo ule japokuwa wamekata rufaa na kesi yao sasa iko kwenye Mahakama Kuu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri pamoja Naibu Waziri, usizungumze jambo ambalo liko Mahakamani, zungumza topic, maudhui unaweza, lakini usizungumzie kesi ambayo iko wapi, wamefikia hatua gani? Ndiyo kanuni zetu, na Kanuni ya 84 ukikataa maelekezo ya Spika, ina adhabu yake. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea. Jambo lingine lilisemwa na Mheshimiwa Malembeka kuhusiana na msaada ambao wasanii wanaupata kupitia Baraza la Sanaa la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Malembeka, ule upolisi ambao Baraza la Sanaa la Taifa lilikuwa likiufanya huko nyuma umesimama sasa hivi. Baraza la Sanaa la Taifa linafanya shughuli yake kama walezi wa wasanii badala ya kuwa Polisi. Sasa hivi tumekuwa tukifanya mijadala mingi na wasanii na hata wasanii hawajisikii vibaya na hawapati uwoga wanapopata wito wa kuitwa BASATA, kwa sababu wanajua ni majadiliano na maelekezano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampa shukrani za dhati Dkt. Kedmon Mapana kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye Baraza la Sanaa la Taifa. Kimsingi BASATA haiwezi kuwalipia wasanii, kuwatengenezea nyimbo zao na kuwatengenezea video, lakini linachofanya ni mambo mbalimbali ikiwemo kuwapa msaada wa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwaka 2024 pekee yake wasanii zaidi ya 20 wamepata msaada wa kisheria kutoka BASATA, wasanii zaidi ya 100 wamepata kazi, matamasha na maonesho mbalimbali ndani ya nchi kupitia BASATA. Maonyesho zaidi ya 200 ya nje ya nchi yamepatikana kwa wasanii wa nchi hii kwenda kutumbuiza kupitia BASATA, hili la upolisi limekwisha kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ada ambazo wasanii wanatakiwa kulipwa zimeshushwa kutoka shilingi 40,000 mpaka shilingi 20,000 kwa mwaka mzima kuanzia mwezi Julai, mwaka huu 2025. Hata zile za kutozwa mara mbili, kwamba kuna tozo ya Halmashauri na tozo ya BASATA na zenyewe zinakwenda kukoma mwezi Julai, mwaka huu, 2025 kwa sababu BASATA imeanzisha Mfumo wake unaitwa AMIS ambao unakwenda kusomana na Mfumo wa TAUSI, na tozo hizi zitakuwa zinakatwa mara moja ili kuwapunguzia kadhia na usumbufu mwingi wasanii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwelezee Mheshimiwa Malembeka ya kwamba, BASATA inafanya kazi yake ya ulezi kama inavyotakiwa kuwa, na mahali popote ambapo wasanii wanakuwa na mkwamo wa aina yoyote BASATA imekuwa ni kimbilio lao kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni la Mheshimiwa Babu Tale ambaye alilisema kuhusiana na fedha za Mfuko wa Utamaduni, mikopo yake kutolewa kupitia benki. Mwanzoni wakati Mfuko wa Sanaa na Utamaduni unaanza, fedha hizi zilikuwa zinatolewa na mfuko moja kwa moja. Idadi ya mikopo ambayo ili-default, ambayo haikurudishwa ilikuwa ni zaidi ya 80% ya fedha zilizotolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Mfuko huu kufanyiwa marekebisho na kupelekwa benki, mikopo hii ikaanza kutolewa benki. Sasa hivi hakuna mkopo hata mmoja ambao haujarudishwa. Hii inaonekana kabisa jinsi ambavyo mfuko huu umekuwa na ufanisi wa hali ya juu baada ya kupelekwa kutolewa mikopo hii kwenye mabenki kinyume na ilivyokuwa hapo awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili jambo halijafanywa kwa ajili ya kuwakomoa wasanii, limefanywa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba fedha hizi zinatolewa na zinarudi ili kuwanufaisha wasanii wengi zaidi. Halikadhalika, ni fursa ya wasanii kujirasimisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukilifanya jambo hili kwa juhudi kuwa zaidi, kwa sababu miongoni mwa kazi za Mfuko huu pamoja na kukopesha, hali kadhalika ni mafunzo na ruzuku. Tumekuwa tukihakikisha wasanii wengi zaidi wananufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Swalle, hata wale wasanii wake wa Lupembe aliowataja hapa, wana nafasi ya kunufaika na Mfuko huu. Ni kufanya maombi na maombi hayafanywi, siyo lazima hata aende kwenye mfuko, yanafanywa kwa njia ya mtandao, na sisi tutaangalia namna ambavyo tunaweza kuwafikia na wasanii wa Lupembe. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia kengele ya pili, naunga mkono hoja. (Makofi)