Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nampongeza Waziri wa Ujenzi ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, Naibu wake Mheshimiwa Kasekenya; Katibu Mkuu, Omary na Msonda na watumishi wote wa Wizara ya Ujenzi, wanafanya kazi nzuri sana. Mheshimiwa Ulega hajawahi kushindwa chochote. Tumemwona kwenye Wizara ya Mifugo, anafanya kazi vizuri sana. Sasa hivi anatembea kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais hasa kwa Jimbo langu la Bunda na kwa Mkoa wa Mara kwa ujumla. Tunampongeza kwa shilingi milioni 56 ya Barabara ya Makutano – Nyamswa – Sanzati ambayo mpaka sasa hivi tunavyozungumza imeshakamilika. Tunampongeza kwa shilingi milioni 67.2 ya barabara ya kutoka Nyamswa – Bunda – Bulamba ambayo imekamilika. Tunampongeza kwa barabara ya kutoka Bulamba – Kisolya, milioni 53, imekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi tunampongeza sana kwa kweli, hamna namna ya kusema zaidi ya kumpongeza kwa juhudi kubwa ambayo ameifanya kwenye barabara hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ya Barabara ya Sanzati – Nata. Kwa kweli hili ni tatizo kubwa, na Mheshimiwa Kasekenya ameshafika pale, na takribani Mawaziri wote, labda Mheshimiwa Ulega ndiye ambaye hajafika pale, lakini wote waliokuwepo wameshafika pale, lakini barabara ile imeshindwa kukamilika. Wale watu waliwapa thamani ya mradi ni shilingi bilioni 51 na sasa wamewapa shilingi bilioni 6.7. Maana yake ni kwamba bado wanadai shilingi bilioni 44 na point. Wale watu wanateseka, wametoka kwenye ile barabara, wameweka lami juu ya barabara kwenye mchanga, wala haifanyi kazi. Inasikitisha sana kutengeneza barabara nzuri kama ile halafu tumeshindwa kuimaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile barabara ndiyo barabara inayotoka Makutano – Sanzate – Nata – Mugumu, imeshindwa kukamilika. Tuelewe hapo wote, Mbuga ya Serengeti ni 80% ya Mkoa wa Mara, ndiyo wanaokaa pale ndani, lakini Mji wa Mugumu kuja Musoma hauna barabara ya lami. Kwa kweli kuna vitu vingine vinasikitisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hii barabara ya Nata – Sanzati, kwa kweli kama wanataka kutukwamisha kwenye Ubunge ni hii barabara. Tunaomba watuokoe kwa sababu hali ni mbaya. Huwezi kutengeneza barabara miaka yote hiyo na haikamiliki na tumetumia hela nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali sana, naomba Mheshimiwa Ulega atoe fedha. Nimesikia juzi kuwa wanawapa shilingi bilioni mbili, wapatie ili waendelee kufanya hiyo kazi. Kuna changamoto nyingine ya barabara ya kutoka Bukama – Salama Kati – Kulusanga – Mihingo, halafu inatoka Mgeta – Mhingo – Mikomalio. Tuliomba shilingi bilioni 1.4 hawajatoa mpaka sasa hivi, na ile barabara imekwenda TANROADS. Tunaomba hizo fedha ambazo TANROADS waliomba, wawape ili wafanye kazi ile, barabara iishe. Tafadhali sana Mheshimiwa Ulega, nakuamini kwenye hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kutoka Balili – Mgeta ambayo inafanyiwa tathmini kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami. Tunaomba hiyo tathmini ifanyike haraka ili barabara iingie kwenye lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mambo mengi hapa yanazungumzwa. Nilikuwa natazama wenzetu wa Shelisheli, wenzetu wa Mauritius, wenzetu wa Congo, wanafanyaje kwenye wakandarasi wazawa? Wana sheria inayosema hivi, “ili mkandarasi wa nje afanye kazi kwenye nchi, lazima awe na mkandarasi wa ndani.” Sisi hapa mnasema subcontract wawepo, lakini wanakwepwa. Hivi kweli inawezekanaje tukope shilingi bilioni 30, shilingi bilioni 300 au shilingi bilioni 400 kutoka nje, tuzilete ndani ya nchi yetu, halafu mtu huyu huyu kutoka nje aje afanye kazi arudi na hizo hela? Hivi inawezekanaje hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani tukope fedha kuja ndani, halafu tumpe mtu kwenda kukaa nazo, haiwezekani. Kwa hiyo, tuweke sheria kwamba kila mkandarasi wa nje sheria yake ni kwamba awe na mkandarasi wa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kufanya mradi wowote; hawa wakandarasi mnaosema wa shilingi bilioni 10, au shilingi bilioni 50, waungane wawe sasa kwenye viwango hivyo. Kila mkandarasi kutoka nje awe na mzawa kutoka ndani ili waweze kufanya kazi ili hela zikiletwa hapa, nyingine zibaki hapa kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)