Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026


WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha Wizara yangu kwa bajeti ya kutekeleza majukumu ambayo yamepangwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, hususan maandalizi ya AFCON ambayo yatapelekea uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya michezo hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji huu ni mbegu na chachu ya mabadiliko makubwa kuelekea kujenga uchumi, ajira na mapato kupitia sekta hii bunifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru wewe binafsi kwa kunipatia nafasi ya kuwasilisha hotuba yangu katika Bunge lako Tukufu. Pia nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuhitimisha hotuba yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Husna Sekiboko, kwa ushauri, maoni na maelekezo kuhusu utekelezaji wa shughuli za Sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Aidha, nawashukuru na Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza na kuchangia hotuba yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba yangu imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge 15 ambapo kati ya hao 14 wamechangia kwa kuzungumza na Mheshimiwa mmoja amechangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu nitoe ufafanuzi kwa baadhi ya hoja zilizotolewa na kuchangiwa na Waheshimiwa Wabunge. Aidha, majibu ya hoja zote kwa kina yatawasilishwa kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika upande wa Sekta ya Habari, nieleze kwamba, kwa kushirikiana na wadau wa habari Wizara imeendelea kulinda na kuuenzi uhuru wa habari na hii imefanya Tanzania kuendelea kutambulika na dunia katika kuuenzi uhuru huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka mitatu, Tanzania imepanda kwa nafasi 48 katika viwango wa uhuru wa habari duniani kutoka nafasi ya 143 mwaka 2023 hadi kufikia nafasi ya 95 mwaka 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Reporters Without Boulders, ambapo katika ripoti ya mwaka 2024 Tanzania ilipanda kutoka nafasi ya 143 hadi nafasi ya 97 na katika ripoti ya mwaka huu iliyotoka wiki jana tarehe 2 Mei, 2025, Tanzania imepanda nafasi mbili kutoka 97 hadi 95. Hii ni ishara kwamba uhuru wa habari hapa Tanzania unazidi kuimarika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia pamoja na hayo yote, Tanzania imeendelea kuwa kinara wa waandishi wake nguli wa habari wanaoshikilia nafasi za juu katika Vyama vya Kihabari Kikanda. Waandishi hao ni Deodatus Balile ambaye ni Rais wa Jukwaa la Wahariri Afrika Mashariki, Ndugu Kajubi Mkangaja ni Mwenyekiti wa Baraza la Habari Afrika Mashariki na Ndugu Ernest Sungura, ni Mwenyekiti wa Mabaraza Huru ya Habari Barani Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu tunategemea kuwa na Mkutano wa Kimataifa wa Mabara Huru ya Habari Duniani, unaotarajiwa kufanyika Mkoani Arusha mwezi Julai mwaka huu. Ninawashukuru wote waliochangia katika hotuba yetu, na kama nilivyosema, majibu mengine mtayapata kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na hili la TSN (Shirika la Magazeti ya Serikali). Hali hiyo imeanza kubadilika kwa sababu ya mtiririko wa fedha kwa mwaka 2023/2024 zilitengwa shilingi bilioni 10, lakini zilitoka shilingi milioni 270 pekee, katika mwaka 2024/2025 zilitengwa shilingi bilioni tano na zilitoka zote shilingi bilioni tano. Katika mapitio ya bajeti, kulionekana umuhimu wa kuongezewa fedha shilingi 4,800,000,000 katika mradi huu. Tayari kwa miezi minne iliyopita Serikali imetoa shilingi bilioni 2.3, hivyo kufanya jumla ya fedha zilizotolewa mwaka huu 2024/2025 kuwa shilingi bilioni 7.3.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kwa usimamizi na mtiririko wa fedha unaondelea sasa, mradi umefikia asilimia 57.9 na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2025. Wizara inapokea ushauri wote unaotolewa na Wabunge lakini ninawahakikishia kwamba hali ya TSN inazidi kubadilika na tunaamini kutokana na huu mtiririko wa fedha hali itakuwa bora zaidi, lakini lolote ambalo litatusaidia kufanya hali hiyo ikamilike kwa haraka sisi tutaliunga mkono na tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye mkakati wa ajira za Kiswahili kwa vijana wetu, Mheshimiwa Khadija Hassan Aboud, alilieleza vizuri. Nieleze tu kwamba, Wizara inaendelea kutekeleza fursa za ajira za Kiswahili kwa vijana ikiwemo, ujenzi wa shule ya Kiswahili na Stadi za Kiafrika itakayotoa fursa za ajira kwa vijana, kufungua vituo mbalimbali vya kufundishia Kiswahili kwa wageni kupitia Balozi za Tanzania nje ya nchi na vituo nje ya Balozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia BAKITA imeendelea kuendesha mafunzo ya msasa kwa taaluma mbalimbali za Kiswahili mfano, ukalimani, tafsiri, uhariri na ufundishaji Kiswahili kwa wageni hasa vijana ili waweze kutumia fursa za ukalimani katika mikutano ya Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mchango wa Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi kuhusu kuwaenzi wazee na waandishi wa mashairi ambao wamesaidia kukuza na kuendeleza Kiswahili na miongoni mwao ni Ndugu Shaaban Robert, Prof. Penina Muhando na Ndugu Nyambari Nyangwine, tunapokea maoni yake ya kuwaenzi wataalam wa mashairi na watu wenye mchango katika kukuza na kuendeleza Kiswahili. Ni jambo lenye tija ambalo limekuwa likifanywa na BAKITA na imeshatoa tuzo mbalimbali kwa Waandishi wakiwemo hayati Shaaban Robert, Prof. Penina Muhando, Prof. Massamba, Mzee Amiri Soud Andanenga na wengineo wengi. Tuzo zinaendelea kutolewa na Mheshimiwa Nyambari Nyangwine naye atafikiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai kwa shule zetu pia kurudisha kwa kasi kabisa ushairi wetu wa ngonjera, ambazo zilikuwa zinahamasisha vijana kuwa wabobevu katika lugha ya Kiswahili fasihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu ametoa ushauri mzuri, kwamba BAKITA iepuke kutengeneza maneno magumu mathalani Kishikwambi, Akili Mnemba ambayo yanahusisha vitu na hali halisi. Maoni yakeo yamepokelewa, ni vyema mchakato wa kuunda maneno uwe wa maneno ya kueleweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza maneno hutafutwa kwenye lahaja za Kiswahili na tunazo nyingi tu. Napenda kuwapongeza BAKIZA kwa kutoa Kamusi ya Kiswahili cha lahaja ya Kimakunduchi, Kitumbatu na Kipemba, na tumewahimiza waendelee kutoa Kiswahili katika lahaja ya Kimvita, lahaja ya Kipate, lahaja ya Kiamu, lahaja ya Kiungwana ambayo inazungumzwa Congo, lahaja ya Kiswahili ambacho kinazungumzwa Madagascar na lahaja ya Kiswahili ambacho kinazungumzwa Comoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kufanya maneno ya utohozi na yapo mengi tu katika Kiswahili kutoka kwenye Kiarabu, Kiajemi, Kireno na Kijerumani. Nataka kusema kwamba utohozi tu unaweza pia ukakifanya Kiswahili kupoteza uhalisia wake, lakini pia tunachukua ushauri wa Prof. Wole Soyinka, ambaye kwa mara ya kwanza mwaka 1976 ndiye aliyesema Kiswahili kiwe Lugha ya Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Prof. Wole Soyinka naye alishauri kwamba ili Kiswahili kiwe lugha ya Afrika, kianze kuchukua maneno kutoka lugha nyingine za Afrika ili baada ya hapo Waafrika wote wawe na lugha ambayo inawaunganisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tutajitahidi kutumia maneno kutoka kwenye lugha zetu na lahaja zetu badala ya kuunda maneno kwenye maabara za lugha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la singeli. Kwanza nashukuru sana mjadala huu ambao umekuwepo kwa muda mrefu, tuliamua kukaa kimya ili Watanzania waseme. Watanzania tunasahau sisi ndio Taifa katika Bara la Afrika lenye tofauti kubwa za utamaduni, tofauti kubwa za lugha kuliko Taifa lolote katika Bara la Afrika. Sisi tuna utofauti mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao utamaduni wa Wabantu, Wakushi, Wakhoisan na Afroasiatic, lakini kinachotufanya Watanzania tujione ni wamoja ni juhudi za Baba wa Taifa kutuunganisha kuwa Taifa moja. Nje ya hapo, sisi tuna tofauti kubwa kuliko nchi yoyote ya Bara la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ndiyo pekee yetu tuna makundi matano ya lugha, pamoja na lugha za watu waliokuja baadaye wa Afroasiatic ambao ni Wairaqw, Wambugu, lakini tuna watu wenye lugha ya asili ya kale katika Bara la Afrika Wahdzabe. Kwa hiyo, tuna tofauti kubwa sana ya Utamaduni. Ukitaka kulijua hilo, leta jambo lolote la utamaduni, hapo ndipo utakapojua tofauti ya Watanzania na tutahangaika na hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hiyo, Serikali haiwezi kuja na wimbo mmoja, haiwezi kuja na chakula kimoja, haiwezi kuja na nguo moja ikijua kuna uanuai (diversity) huo. Wakati mwingine imetufanya tukimbilie nyimbo za Kwaito, kwa sababu haina mwenyewe, kuliko nyimbo zetu wenyewe kwa sababu tunaona ni tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Baba wa Taifa, kwani asingefanya hivyo, Tanzania hii ingekuwa haikaliki. Kwa sababu tuna tofauti kubwa katika mavazi, katika chakula, katika vionjo na pia vinachochewa na imani za dini. Kwa hiyo, tushukuru tuko Taifa moja. Maana yake ni nini? Ni lazima tutekeleze 4R katika kujadili muziki wa Singeli, 4R za Rais Samia Suluhu Hassan za ustahimilivu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Singeli kwa sasa imekuwa ni moja kati ya Miziki ya Tanzania kama ilivyo kwa miziki ya dansi, taarabu, kwaya, Bongo Fleva na miziki mingine. Tunachokifanya kwenye Singeli, wala siyo kuipeleka duniani. Singeli tayari imeshakwenda duniani kwenye matamasha ya Ubelgiji na haichezwi kama hizo ambazo mnaziona, ambazo Naibu Spika amenisaidia, imekwenda kwenye Tamasha la Primavera, Spain; Tamasha la CORA Festival, Ufaransa; Tamasha la Munich; Tamasha la Dusseldorf; na tamasha ambalo ashakum siyo matusi Nyegenyege, Uganda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tarehe 26 Aprili, 2025, kwenye Tamasha la Samia Serengeti Music Festival ambalo mgeni wa Heshima alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dogo Paten pamoja na Zuchu, walicheza Singeli ambayo iliwafanya watu wachangamke.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, yako mambo ambayo ni ya upotofu wa maadili na hiyo siyo kwa Singeli tu, iwe ni muziki wa Injili, iwe ni muziki wa dansi, iwe ni muziki wowote, utakapokuwa na mambo ambayo siyo ya maadili, Wizara itachukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama muziki wa Injili utakuwa ni wa kunengua utachukuliwa hatua; kama muziki wa kawaida utakuwa hauendi na maadili utachukuliwa hatua; kwa hiyo, tusichanganye vionjo vya wachezaji na aina ya muziki.

Mheshimiwa Naibu Spika, yakumbukeni maneno ya Yesu Kristo katika Biblia walipompelekea kahaba akasema, “yule ambaye hajawahi kufanya hayo, awe wa kwanza wa kumtupia huyo jiwe.” Wote waliangalia chini na kuchora chini ya miguu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwasaidie vijana hawa kuusafisha muziki huo ambao tayari umeshakwenda duniani. Hatutavumilia aina yoyote ya muziki unaotweza wanawake, wala kuwashushia hadhi, uwe ni wa aina yoyote ile, lakini Singeli imepiga hatua,

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyosemwa, Singeli tunayoizungumza ya kwenye video na nimeletewa hiyo sijui ya Nairobi, ya wapi, hao ni vijana waendelee kuombewa, waendelee kuaswa, waendelee kuonywa. Kama alivyosema Yesu, nimekuja kwa wagonjwa, mimi ni tabibu, na siyo kwa walio wazima. Ninyi wote ambao mmeokoka endeleeni kuwaombea hao watu, na imbeni tabibu wa kweli ni Yesu Kristo au Mtume Mohamadi (S.A.W.) ili wawe na heshima katika aina zote za miziki na aina yoyote ya michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la mustakabali wa mchezo wa kati ya Simba na Yanga. Umeeleza wazi, kwa mujibu wa Sheria za FIFA, Wizara au Serikali haiwezi kuingilia suala hilo. Suala la Ligi inasimamiwa na TFF, linasimamiwa na bodi ya ligi na Kanuni haziruhusu Serikali kuingilia mambo hayo, kwa sababu ukifanya hivyo, FIFA itaifungia Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa ndugu yangu Mheshimiwa Swalle na Wanasheria wengine, hilo jambo ni sub judice na kwa sababu ni sub judice siwezi kulisema. Nikilisema nitakuwa nimefanya makosa ya Padri kutoa maungamo. Kwa hiyo, tunaendelea na juhudi mbalimbali na mazungumzo yetu yaligusa kuhusu kuboresha mchezo wa mpira katika nyanja mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii tena kuwashukuru Wabunge wote waliotoa maoni ya kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan apewe tuzo kwa kufanya maendeleo ya michezo. Hakika Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa ni hidaya ya Taifa letu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa ni hiba ya Taifa letu katika eneo la Sanaa na Michezo, nami naunga mkono kabisa wazo hilo la Wabunge la kuwa na aina maalumu ya tuzo kwa Mheshimiwa Rais kwa kutambua mchango wake mkubwa katika Sekta hii ya Michezo, Sanaa, Utamaduni na Habari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala ya viwanja, niwahakikishie kabisa ndugu yangu Mheshimiwa Priscus Tarimo wa Moshi Mjini kwamba tutatuma wataalam kuja kuangalia suala la Kiwanja cha Moshi. Ndugu yangu alikuwa hapa Mheshimiwa Joseph Tadayo, ninaona ametoka Mbunge wa Mwanga na ninajua ni kwa nini ametoka. Kama mlivyosikia tangazo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumefikwa na msiba mkubwa wa kuondokewa na Mzee Cleopa David Msuya, aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia alikuwa Waziri Mkuu wakati wa Mwalimu, alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Fedha. Ni mzee ambaye ametoa mchango mkubwa wa Taifa. Kwa hiyo, ndiyo maana yeye hayupo hapa, naye namhakikishia nitakwenda Mwanga kwa ajili hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimhakikishie ndugu yangu Mheshimiwa Edwin Swalle, nitafika Lupembe, Njombe ili kuona eneo hilo na tuone na wataalam ni jinsi gani pia tutaboresha Uwanja wa Lupembe, Njombe. Ipo sababu kubwa sana ya mimi kufika Lupembe, Njombe, kwa sababu Mama yangu mkubwa nilikokulia aliolewa na Luchangiro kutoka Lupembe. Kwa hiyo nitakwenda huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuhitimisha kwa kueleza kwamba baada ya mafanikio makubwa ya timu ya Simba na sasa inaingia kwenye mchezo wa kwanza wa Fainali ya Kombe la Shirikisho linaloandaliwa na CAF ambapo Klabu ya Simba inakwenda Morocco kupambana na Klabu ya RS Berkane, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya maamuzi ya kutoa ndege itakayoipeleka Klabu ya Simba nchini Morocco kwa ajili ya mchezo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutoa hoja. (Makofi)