Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye anaendelea kutustahilisha sisi wote humu ndani miongoni mwa Watanzania walio wengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anafanya kazi kubwa na nzuri kwenye sekta zote ikiwemo kwenye sekta hii ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nampongeza kaka yangu Mheshimiwa Ustaadhi Abdallah Ulega kwa kuendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais na kuteuliwa kwenye nafasi hii ya kuwa Waziri wa Wizara hii. Mheshimiwa Ulega ni mtu mzuri, mtu rahimu, mchapakazi, hatuna shida naye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tu Mwenyezi Mungu amsaidie dude hili linaloitwa ujenzi lisimbadilishe, aendelee kufanya kazi yake vizuri. Pia tuipongeze timu yote ya Wizara ya Ujenzi, kwa maana ya Naibu Waziri, Katibu Mkuu na pia Mtendaji Mkuu wa TANROADS kwa kazi nzuri na kazi kubwa ambayo anafanya kwenye maeneo yote ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango kwenye maeneo machache. Eneo la kwanza niongeze na kukoleza sauti kwenye maeneo ambayo Mheshimiwa Shangazi aliyasema jana na Mheshimiwa Ummy ameyasema leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Handeni – Kiberashi – Mtoro ni barabara ambayo sisi watu wa Tanga tunaamini ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa mkoa wetu na kwa uchumi wa nchi yetu. Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa kwenye bandari. Bila kuwa na uhakika wa barabara hii, kazi kubwa ya kwenye bandari haitakuwa na matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kazi inayoendelea kufanywa kwenye baadhi ya vipande kwenye barabara hii kwa sasa. Pia natambua maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Rais na ameyarejea jana vizuri sana kwenye hotuba yake. Tunaomba yafanyiwe kazi aliyosema Mheshimiwa Rais, yafanikiwe ili ndoto za watu wa Tanga na manufaa ya kazi kubwa ya uwekezaji inayofanyika kwenye bandari yaweze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni kuhusu Barabara ya Tanga – Pangani – Makurunge. Barabara hii ni muhimu sana kwa ajili ya kuufungua Mkoa wa Tanga, kufungua uchumi wa Tanga, hasa hifadhi yetu ya Saadan kwenye kukuza utalii. Tunatambua kazi inaendelea kufanyika, tunaomba mwendelee kumsimamia mkandarasi, kazi hii ifanyike vizuri kwa manufaa ya mkoa wetu na ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa barabara ya Soni – Bumburi – Dindira – Korogwe, hii barabara tumeipigia kelele sana. Tunafurahi leo ninachangia tofauti kidogo na mchango wangu wa mwaka 2024, kwa sababu nimeona kazi iliyoanza kufanyika kwa sababu Serikali tayari ilishatangaza zabuni ya kumpata mkandarasi wa kufanya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba nisisitize hapa, Mheshimiwa Waziri aongeze spidi ya kazi, anakwenda pole pole. Wiki iliyopita niliuliza swali hapa Bungeni kuhusu barabara hii, Naibu Waziri alinijibu kwamba ipo kwenye hatua za manunuzi. Sasa hii kesi sisi watu wa Tanga, watu wa Korogwe na Bumbuli tulishaiacha, tumemkabidhi mwenyewe, mwenye Wanakorogwe wake, mwenye Bumbuli wake ambaye sio mwingine ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 24 ya mwezi wa Pili Mheshimiwa Rais akiwa Lushoto, Mheshimiwa Waziri alikuwepo, akawaambia watu wa Korogwe na watu wa Bumbuli juu ya barabara hii. Naomba ninukuu maneno ya Mheshimiwa Rais, “Nataka niwaambie, tarehe 6 ya mwezi ujao wa Juni, 2025 tunafungua tenda kutafuta mkandarasi na barabara itaanza kujengwa; na tunaanza kujenga kilometa 22 kuanzia Soni – Bumbuli na kilometa 9.3 kwa Meta – Shemshi, tutakwenda pole pole. Tutaanza hapo na polepole tutakwenda.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni maneno ya Mheshimiwa Rais. Sisi humu ndani tumeacha hii kesi kwa Mheshimiwa Rais, ametoa ahadi na aliwaahidi watu wa Korogwe na watu wa Bumbuli. Mheshimiwa Waziri bado kasi kwenye kazi hii sioni kama ni ya kuridhisha, tunaomba waongeze kazi ili jambo hili liweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, tunayo barabara ya kutoka Old Korogwe – Magoma – Mashewa – Bombomtoni – Mabokweni. Barabara hii ni muhimu sana, na kaka yangu Mheshimiwa Kitandula amesema hapa kwa zaidi ya miaka 13 kabla hajaingia Serikalini. Mimi nimeisema kwa takribani miaka saba, au sita sasa hivi, lakini pia ilikuwa na ahadi za viongozi wetu wa dini; Shehe Mkuu wa Tanzania ameisemea sana barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ulega, tukiwa na Mheshimiwa Rais, Tanga, tulifanya vikao mimi, yeye na Shehe Mkuu kuhusu barabara hii. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, nimeona kwenye hotuba yake ukurasa wa 84 ameeleza kwamba kwenye mwaka wa fedha unaokuja tunakwenda kuanza ujenzi wa barabara hii kilometa 10 za kutoka Old Korogwe mpaka Kwa Mndolwa na Kilometa 10 za kutoka Mabokweni – Maramba. Jambo hili ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mmoja tulifikiri tukasema, tumesema sisi Wabunge hawakutusikia, Marais wameahidi hawakufanya, na viongozi wa dini wakasema. Tukajiuliza, wenzetu hawa wanataka aseme nani ili wamsikie? Leo tumeona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Ulega, tunaomba ahadi hii ikatekelezwe kwa sababu barabara hii ni barabara muhimu sana. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naiomba Serikali iongeze kasi ya barabara ya kutoka Ndungu – Mkomazi. Kwenye hotuba yake…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: …amesema imefika asilimia 2.4 tuongeze kasi, barabara hii ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)