Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya ya kuweza kusimama na kuchangia katika bajeti hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa nzuri ambayo anaifanya kuhakikisha kwamba nchi yote inapitika. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wasaidizi wake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nitakuwa na mchango katika maeneo mawili au matatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza, ni ukweli usiopingika, na Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri analijua, juu ya umuhimu wa ujenzi wa barabara ya lami kuanzia Kasesha Boda – Matai. Barabara hii ni ya jumla ya kilometa 60 yenye thamani ya bilioni 37.353. Fedha ambayo imeshalipwa ni shilingi bilioni 6.943, fedha ambayo inadaiwa kwa maana ya certificate ambayo inasubiriwa kulipwa ni shilingi bilioni 13.027. Hivi ninavyoongea, mkandarasi hayupo site kwa sababu anadai fedha hii ili aweze kurudi site. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii umuhimu wake hakuna mtu ambaye anatilia mashaka. Ili kuondokana na msongamano wa malori ambayo yapo mengi sana Tunduma. Ufumbuzi wa haraka ni kuhakikisha kwamba barabara hii inakamilika. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri katika certificate ambazo ni za kuhakikisha kwamba zinafuatiliwa na zinalipwa ni pamoja na hiki kiasi cha shilingi bilioni 13.027. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa barabara hii naomba tu nitoe takwimu jinsi ambavyo imekuwa ikileta mapato kwa TRA, kwa maana ya customs. Mwaka 2021/2022 barabara hii tuliweza kukusanya kiasi cha shilingi bilioni tu, lakini baada ya ujenzi kuanza, mwaka 2022/2023 TRA wamekusanya jumla ya shilingi bilioni nne; mwaka 2023/2024 wamekusanya shilingi bilioni 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Barabara hii ikikamilika kwa ujenzi wa kiwango cha lami, maana yake ni kwamba, yale malori yote ambayo yanatakiwa kwenda Rwanda, Burundi, Mwanza, Uganda, yale ambayo yanatoka Zambia, South Africa, hawatapita Tunduma. Makusanyo yatakuwa makubwa sana na watakuwa wamepunguza umbali mrefu badala ya kuzunguka Tunduma, na msongamano ambao upo Tunduma itabaki ni historia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha pili ambacho ni kilometa 30 tayari mkandarasi ameshasaini, lakini hawezi kuingia kwa sababu hajalipwa certificate ya kwanza. Thamani ya project ni shilingi bilioni 36.365, advance payment ili aingie kazini ni shilingi bilioni 3.525.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu wa barabara hii ikiwa inaunganisha nchi hizo ambazo nimezitaja na ili kupunguza umbali huo ambao watu wanalazimika kupita, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, barabara hii ipewe kipaumbele ili kama Taifa tuanze kuchuma fedha ambayo obvious iko, inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba nieleze juu ya namna bora ya kuhakikisha kwamba msongamano wa malori unapungua Tunduma. Mheshimiwa Rais alivyokuwa kwenye ziara mwezi wa Saba mwaka 2024, aliridhia umuhimu wa kuunganisha kipande cha kutoka Laela. Mheshimiwa Sangu anajua, wameshaanza upande wa kwake, ni jumla ya kilometa 90 ili barabara hii ianze kujengwa kwa kiwango cha lami, tuunganishe ili tupunguze msongamano ambao uko Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ikiunganishwa, tafsiri yake ni kwamba tunaenda kuunganisha pamoja na Kasanga Port. Tafsiri yake, kile alichokuwa anakisema Mheshimiwa Conchesta, ukiwa unataka kwenda Lugumbashi hulazimiki kwenda Kalemie. Kalemie ni kilometa 1,000 na ushee, lakini huku tunaongelea kilometa 480. Hivi tufanyeje ili tuweze kufika DRC bila kupita Zambia? Ni kuhakikisha kipande hiki kinajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tuhakikishe bandari ya asili kwa tafsiri aliyokuwa amefanya Mbelgiji, ni port iliyoko eneo linaitwa Mulilo na wala siyo Kalemie. Kalemie ni mbali sana. Mnaitafuta Congo ipi ambayo haina mazao ambayo tunahitaji kama Taifa? Njia ya shortcut ni kupita Kasanga Port. Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi analijua, na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi naomba kwa kushirikiana wahakikishe zile kilometa chache ndani ya DRC tunazijenga kwa sababu wanufaika wa kwanza ni sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi barabara ambazo nimezitaja zina manufaa makubwa sana kiuchumi. Mheshimiwa Waziri. Katika hiki kipande cha pili, wananchi wa Vijiji vya Tatanda, Kaluko, Kasesha pamoja na Katete, wameahidiwa fidia ili ujenzi uanze. Naomba hili lifanyike na wananchi wako tayari kupisha ili kazi nzuri ya kuunganisha kwenda Zambia, lakini wakati huo kwenda upande wa pili wa DRC, inafanyika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nadhani itoshe ili yatiliwe uzito mkubwa katika bajeti hii. Mheshimiwa Waziri, uhakikishe yanaenda kufanyiwa kazi. Nakushukuru. (Makofi)