Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe shukurani nyingi kwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha alizowapelekea wananchi wa Ushetu. Vilevile, natoa shukurani kwa Mheshimiwa Waziri, na Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo wanatupa upendeleo wananchi wa Ushetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukurani nyingi kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wetu wa Shinyanga, Eng. Samweli Mwambumbu. Kijana anafanya kazi kwa kujitoa kwa kusimamia fedha na miradi mikubwa ambayo imeletwa kwa wananchi wa Ushetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa madaraja manne ya shilingi bilioni 18 kwa wananchi wa Ushetu. Kwa kweli umetutendea haki. Kazi inafanyika vizuri, wakandarasi wako kazini, Meneja wetu wa mkoa na timu yake na vijana wake wanawasimamia vizuri kabisa. Kwa hiyo, tuna uhakika yatakamilika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Mwabomba ambalo lilikuwa ni kero kwa wananchi lina mkandarasi, Daraja la Ubagwe lilikuwa kero kwa wananchi, lina mkandarasi, Daraja la Kasenga – Igombe River nalo lina mkandarasi, na Daraja la Uyogo – Ng’hwande na lenyewe tayari lina mkandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, nina barabara yangu ya kutoka Tulole - Chona - Chambo. Ni barabara ya zaidi ya kilometa 15, kutoka Kahama kwenda Tulole, ukiianza tu Ushetu imeondolewa TANROADS ikarudishwa TARURA; ukimaliza Chona ukaingia Tabora pale, inaingia TANROADS. Hiki kipande kimenichonganisha sana na wananchi. Nimelia sana, lakini pia RCC imesema sana, hebu kirudishwe TANROADS kiendelee kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pale namshukuru sana Meneja wangu, anaendelea kujitolea kukitengeneza, lakini ni kipande ambacho kinatuumiza sana na kutuchonganisha na wananchi. Naomba kirudishwe TANROADS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nina barabara yangu nimeiomba sana na RCC imepitisha zaidi ya mara mbili. Barabara inayotoka Nyankende pale Mwadui – Nyambeshi – Bunanda – Imalabupina – Kalo (Bulungwa) – Sabasabini - Mpunze mpaka Nyandekwa, ni kilometa kama 76. Hii barabara nimeiombea sana kwenda TANROADS. Ni barabara ambayo inajenga na kusimamia uchumi wa Halmashauri ya Ushetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa barabara yangu ya kutoka Mwabomba inayokuja Nyankende mpaka Ulowa, mpaka Igombe River, wamenipandishia TANROADS inaendelea kutengenezwa. Sasa naomba na hii barabara waichukue pia, kwa sababu ndiyo mhimili mkubwa wa Halmashauri ya Ushetu na yenyewe waipeleke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nina barabara yangu ya kilometa 54 ambayo ipo kwenye Ilani na pia, kila mwaka ipo. Naibu Waziri, Mheshimiwa Kasekenya anaijua na ameshakuja kuteimbelea. Nimeiombea lami na kwenye Ilani ipo. Leo ni mwaka wa tano, mwaka jana waliingiza, wakatenga kama shilingi bilioni tatu, lakini hakuna kilichofanyika. Basi nipewe na mimi, unajua Ushetu ni eneo ambalo lina uzalishaji mkubwa, lakini hatuna hata ile lami ya kupigia picha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2024 Mheshimiwa Naibu Waziri amenipa mita 500 tu pale Uyogo, lakini sasa hebu nisaidiwe, kuitengeneza angalau hata kidogo kidogo waitengee fedha. Naridhika na fedha wanazonipatia na ninawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, lakini basi hebu nitendeeni haki kwa hizi kilometa 54 za barabara inayotoka hapa Kahama – Nyandekwa, inapita Ukune inaenda Kisuke – Nyamilangano mpaka Uyogo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi angalau waanze kuijenga taratibu kwa kiwango cha lami kwa sababu waliahidi wenyewe. Mheshimiwa Rais ameahidi mwenyewe, amepita pale akaona umuhimu wake na kwenye Taarifa ya Itifaki ya Mwenge wameiona, wananchi walilalamika sana. Naomba tutendewe haki angalau ianze kujengwa kidogo kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niliomba taa za barabarani pale Nyamilangano. Mheshimiwa Naibu Waziri aliniahidi mwaka 2024, na kwenye swali langu la msingi alisema ataweka. Naomba nipewe basi hizo taa pale Uyogo na pia zile taa za barabarani pale Nyamilangano, angalau wananchi wangu pia waone sasa kazi ni kubwa. Pamoja na fedha wanazonipatia, na zile taa waniwekee pale barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa barabara yangu ya kilometa 30 ya kutoka Uyogo kwenda Ulowa imepandishwa na yenyewe kwenda TANROADS na imeanza kutengenezwa, lakini shida iliyopo, barabara ile bado ni finyu na ni ndogo. Naomba sasa ipanuliwe kwa sababu wananchi wangu wanapata ajali sana katika eneo hilo. Ipanuliwe iingie kwenye kiwango cha barabara ya TANROADS. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nawaomba, pale Kahama kuna barabara ya kwenda...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Cherehani.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)