Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Ulega, kwenye nafasi yake, kwa kweli amefanya kazi kubwa kwa kipindi kifupi, lakini mimi na yeye tuna jambo letu. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, atukumbuke kwenye kipande changu cha lami cha kilometa 20 kutoka Nkome. Najua kuna changamoto ya fedha, lakini Mungu akijaalia akipata advance naomba atukumbuke, kwa sababu wakandarasi wako site tunasubiri hiyo fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nashauri, najua tunaenda kufungua Daraja la Busisi. Hili daraja wafaidika wakubwa ni watu wa ng’ambo, maana yake Sengerema, Geita, Bukoba, na Kigoma. Sisi kwetu hili ni jambo la kihistoria, siyo jambo la mzaha, na siyo jambo la kawaida kama unavyofikiria. Ni jambo kubwa sana na tunahitaji kuhudhuria sherehe hizi ambazo Mheshimiwa Rais atakuwa mgeni rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ufunguzi wa ujenzi wa daraja ulifanyika Misungwi upande wa Mwanza na sisi tumejipanga kupeleka watu kwenda kumshangilia Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya. Mpaka sasa mimi jimboni kwangu kuna mabasi zaidi ya 30, wanasubiri tu tarehe ya Mheshimiwa Waziri, watatangulia hapo siku tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba, ili tuwe fair, sherehe hizi zifanyike upande wa Busisi Sengerema ili iwe rahisi watu wa Kigoma, Kagera, Geita na Mwanza nao wavuke tukutane, siyo kila mara mnatuvusha kwenda Mwanza. Kwa hiyo, naomba sana wanapoandaa sherehe hizi, zifanyike upande wa Busisi Sengerema. Eneo linatosha, basi tufanyie hapo ili na sisi tuweze kupata nafasi ya kumwona Mheshimiwa Rais wetu na kumpongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kale Kakiingereza kake kale alikokafanya kwa Wachina Dar es Salaam. Safi sana Mheshimiwa, kamefanya kazi. Naona Wachina sasa waliogopa kile Kiingereza, wamekimbia kwa kweli, lakini nina ushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wote tunapita kwenye hiyo barabara. Hebu fikiria mtu anayetoka Airport ya Dar es Salaam anakaa Mbweni, kama itaisha hiyo barabara mpaka Mbweni na Tegeta, nataka uniambie ukipita kuanzia Airport, unazionaje zile kona? Maana ninaona kama tunarudishwa kucheza twist; unakata kulia, unakata kushoto, unakata kulia mpaka unafika Mbweni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukishuka usiku, huwezi hata kulala. Ukipitiwa usingizi kidogo tu imekata kona, imekata kulia. Mheshimiwa Waziri ukipita tena ninaomba uangalie hata ule uwekaji wa zile kingo za Barabara, zimeshagongwa karibia zote kuanzia mwanzo huku walikomaliza mpaka unafika mjini. Kila angle imegongwa. Sasa nadhani tuna ma-engineer wazuri na Besta yuko hapa, oneni namna ya kuzipunguza zile kona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajaribu kulinganisha na nchi nyingine. Sioni mahali ambapo kuna hiyo barabara ya design hiyo, kuzunguka kuanzia mwanzo mpaka mwisho, unakata kona tu. Sasa naona nishauri kwamba, kule upande wa kulia na kushoto, zile kingo wajaribu kuzipunguza kwa kweli, zinatusababishia ajali. Ninyi wenyewe ni mashahidi, aidha mmeweka makubwa sana au imekuwaje, sijui. Mtaona jinsi gani mtakavyofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, ni kweli kama Waheshimiwa Wabunge tunavyosema, mimi binafsi kwenye jimbo langu pamoja na kwamba sina lami, ndiyo nakuomba nisaidiwe, lakini tunaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa fedha nilizopokea, kwa barabara zangu zilivyo nzuri muda wote wa mvua za masika. Tunaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo, unafahamu tunaye mkandarasi kuanzia Sungusila – Nzera – Nkome, barabara hiyo tayari ina Mkandarasi wa Kichina kilometa 30 kutoka Geita kuja Sungusila zenyewe zimefanyiwa maintenance. Kule aliko Mchina, hakuna maintenance, barabara ni mbaya kwa kweli. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aone namna ya kutusaidia kuweza kumsimamia Mchina ili aweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, sisi tunaungana na Buchosa na Sengerema. Barabara ya Buchosa – Sengerema – Nkome ni barabara ya kimkakati sana. Yaani haya maeneo ndiyo yanailisha Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naomba tutakapoenda kufungua daraja letu, tusiende sana kwenye bure. Hili nalisema kwa uzalendo tu. Tumefanya kazi kubwa sana kwenye lile daraja. Ni daraja kubwa la kihistoria. Mimi ninapitisha gari zangu pale kama 30 au 35 kwa siku. Tunalipa shilingi 10,000, shilingi 15,000 mpaka shilingi 80,000 hadi shilingi 100,000 kwa malori. Sasa naomba tusidekeze sana kwenye bure. Tuweke tozo hata shilingi 5,000. Watu wasilipe, lakini magari yale yanayofanya biashara tulipe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunahitaji madaraja mengine. Kuna daraja la kutoka Mwanza kwenda Kamanga. Tunahitaji nako tuwekewe daraja kubwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, ahsante sana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)