Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo ambalo linaguswa kwa kiwango kidogo sana na Wizara ya Ujenzi na TANROADS ni pamoja na Jimbo la Arusha. Ukizungumzia Barabara ya Mianzini – Ngaramtoni kilometa 18, Jimbo la Arusha tuna meta 200 tu, nyingine zote ziko Wilaya ya Arumeru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla wake kwa miaka yote mitano toka mwaka 2020 mpaka sasa tumekuwa tunajenga hoja kwa Barabara yetu ya kutoka Arusha Airport kwenda Kilombero, inatakiwa ijengwe kwa njia nne. Kwa miaka yote mitano, Serikali imekuwa inafanya usanifu, na mpaka leo tumeona taarifa ya Mheshimiwa Waziri inatuambia usanifu umekamilika ndani ya miaka hiyo mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa kwenye bajeti hii Mheshimiwa Waziri atuambie sasa baada ya kukamilisha usanifu, ni lini watatangaza tender apatikane mkandarasi na hasa ukizingatia kwamba tunaenda kwenye masuala ya AFCON, na Mheshimiwa Dkt. Samia ameweka vizuri masuala ya utalii pale kwenye upande wa Royal Tour?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, hiyo barabara ikitengenezwa itasaidia pia kuondoa mafuriko. Kuna Kata kama ya Unga Limited, Sombetini, na Osunyai, mafuriko ni makubwa sana. Barabara ikijengwa, tunaamini kwamba mitaro itatengenezwa na changamoto kwa wananchi itaweza kuondoka. Pia, tunaomba wakalipe fidia angalau kwa kipindi hiki wakati tunasubiri na michakato mingine ya kujenga hiyo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusiana na Barabara ya Arusha – Kibaya – Kongwa, na yenyewe pia tumeipigia debe kwa miaka yote mitano. Mara ya kwanza mkataba ulisainiwa kupitia EPC+F, zikatokea changamoto. Umekuja tena mradi mwingine, mnasema sanifu na kujenga lakini mmeshasaini mkataba kwa kilometa 70 na hapa Bungeni wamejibu mara nyingi sana, lakini hadi leo tunavyozunguza, mkandarasi bado hajafika site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itatusaidia kupata barabara ya njia nne kutoka Kona ya Mbauda, kushuka mpaka kule chini Kwa Morombo ambako tunakwenda kujenga stendi ya kisasa. Itasaidia pia kuondoa na mafuriko kwenye eneo la Kata ya Sombetini pamoja na Kata ya Osunyai. Kwa hiyo, sasa tuambiwe huyo mkandarasi atakwenda lini site ili itusaidie kwenye masuala ya AFCON na kazi yote ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia anaifanya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kuhusiana na mafuriko. Tunajenga barabara nzuri. Mfano, Barabara ya Sakina – Tengeru, imejengwa vizuri, lakini maji yameelekezwa kwa wananchi. Ukiangalia Kata ya Ngarenaro, Kata ya Sakina, ukiangalia Kaloleni yenyewe, ukienda kule Baraa, na ukienda Kimandolu, kote mvua ikinyesha ni vurugu tupu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunategemea sasa wakafanye study ya kutosha ile yale maji yanayopita pale wayatafutie njia ya kupita yaende kwenye mitaro au kwenye mito kama Mto Nduruma ili tuweze kuwaondolea wananchi adha hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunashukuru kuona kwamba kuna baadhi ya jitihada zimeanza mfano kwenye Kata ya Terrat, kuna barabara ya Namba Sabini kule kwenye Mtaa wa Olkungu. Tumeona tayari mkandarasi amepatikana lakini alikwenda akachimba chimba, baadaye ameweka greda pembeni kazi haiendelei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba akasukumwe ile kazi ikafanyike ili wananchi wa Olkungu pale Namba Sabini wasipate changamoto hiyo. Pia, Mitaa kama ya Bondeni Kati, eneo la Mpambazuko pia lisipate changamoto hiyo ya mafuriko pamoja na Mtaa wa Laitayok kwenye Kata hiyo ya Terrat. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na malipo ya wakandarasi. Tunajua TANROADS na Wizara ya Ujenzi wangependa kujenga barabara zote nchi nzima, lakini ili wajenge barabara wanahitaji kuwa na fedha. Tumekuwa na taarifa kwamba wakandarasi wetu wana changamoto kubwa ya kupata malipo ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba Wizara ya Ujenzi ikae na Wizara ya Fedha ili itoe kipaumbele cha kutosha, maana najua wakipata fedha kusukumana na wakandarasi ili kazi ziende ni jambo ambalo wana uwezo nalo. Kama hamna fedha mkandarasi ameshafanya kazi, ametoa certificate kama fedha hakuna, kazi haiwezi kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kikubwa zaidi wakandarasi wetu wanapata hasara, wamekopa fedha kutoka benki, na nilikuwa nimejenga hoja kwenye Bunge hili, wakandarasi wa nje wakipewa kazi wanawekewa na riba. Serikali ikishindwa kulipa fedha kila baada ya muda riba inaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wakandarasi wa ndani na tumesema Serikali yetu inaangalia wazawa, kwa nini wao wakipewa kazi, Serikali ikichelewa kuwalipa, nao tusiwawekee riba ili mwisho wa siku zile riba wanazopata kwenye maeneo ya benki na maeneo mengine zisiendelee kuwaumiza? Wako baadhi ya wakandarasi ambao wameweza kuuza nyumba zao, mali zao na wamefilisiwa kwa sababu ya kucheleweshwa kulipwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu Mheshimiwa Dkt. Samia anawapenda Watanzania, anawapenda wananchi na anawajali wakandarasi wazawa. Sasa wanaomsaidia kwenye Wizara ya Fedha na Wizara ya Ujenzi, tumsaidie Mheshimiwa Rais kuweka mipango mizuri zaidi na tusitangaze tender kama hatuna fedha. Tusim-award kazi mkandarasi kama hatuna fedha. Kwa kufanya hivyo tunawarudisha nyuma badala ya kwenda kuwasogeza mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la kumalizia, kuna changamoto kwenye upande wa fidia. Barabara yetu ya Arusha Bypass ile kwenye Kata kama za Moshono na kata nyingine, wako wananchi ambao maeneo yao yamezuiliwa na Serikali kwa muda mrefu, wanaambiwa watalipwa fidia. Mwananchi anashindwa kuendeleza, kujenga na anashindwa kuuza na Serikali haimwambii ni lini itamlipa fidia. Naomba mtuambie ni lini mtalipa fidia na ikishindikana, basi wale wananchi wawe huru na maeneo yao na Serikali ikiyahitaji watakuja kule.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa sababu ya changamoto ya muda, nakushukuru sana na nitaunga mkono hoja baada ya kupata majibu ya kuniridhisha kulingana na masuala ambayo nimeyaelezea.