Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nichangie Bajeti ya Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamesimama hapa wakimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara hii kwa kazi nzuri ambazo zimefanyika kwenye majimbo yao. Kwa upande wangu ninapata kigugumizi kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata kigugumizi kwa sababu maalum. Kuna mchezo unaofanyika katika Jimbo la Same Mashariki kuhusiana na barabara hii ambayo imepangwa kwenye bajeti 2025/2026. Mchezo huu umeanza muda mrefu sana, kiasi inaonesha kwamba Jimbo la Same Mashariki, barabara zake zinafanyiwa hujuma ya makusudi, kwa maana zimeshapangwa kwenye bajeti, hii ni mara ya tatu, lakini utekelezaji wake hauonekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niwape scenario inayoweza kufanya tuone kwa kweli kuna mchezo mchafu unafanyika katika barabara hii. Kwa hiyo, mchango wangu uko kwenye sura ya tatu; Mpango wa Bajeti ya mwaka 2025/2026 na unazungumzia kuendelea na ujenzi wa barabara ya Same – Kisiwani – Mkomazi kilomita 97. Ndungu – Mkomazi wameweka vipande viwili kilomita 36, Same – Kisiwani kilomita 56.8, jumla wanazungumzia kilomita 92.83 na bajeti yake ni shilingi bilioni sita kama nimesoma vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika barabara tajwa hapo juu tarehe 18 Agosti, 2021, Serikali ilisaini mkataba wa kutengeneza kipande cha Mroyo – Ndungu. Katika kujibu swali langu la msingi Na. 22, hapo tarehe 31 Februari, 2024, majibu ya Naibu Waziri wa Ujenzi kwa wakati huo alisema kwamba, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi milioni 860 zilizotumika kwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara ya Same – Kisiwani – Ndungo – Mkomazi, ambapo aliweka kilometa 96.46 na alisema kazi ilikamilika mwezi Septemba, 2022, ilichukua miaka mitatu kufanya kazi hiyo. Miaka mitatu na shilingi milioni 860. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Naibu Waziri ambaye ninamheshimu na ninampenda sana, aliendelea kusema kuwa, katika mwaka wa fedha 2021, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 6.3 ambazo zilitumika kwa kazi ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa kipande cha kilometa 5.2, nacho hicho kilikuwa Gonja – Ndungu. Aliendelea kusema kwamba, ujenzi ulikuwa umefikia 25% na barabara hii ilikuwa inategemewa ikamilike Juni, 2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza hivi, kama kilometa 5.2 zimechukua huu mwaka wa nne hazijakamilika, kweli tunafikiria kilometa 92.85 zilizowekwa kwenye bajeti hii zitakamilika? Ni barabara hiyo hiyo, kipande kidogo tu, na hicho kipande kidogo cha kilometa tano kilitengewa shilingi bilioni 6.3, hii kilometa 92.83 kimetengewa shilingi bilioni sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa akili ya kawaida, unasema huu ni usanii. Kama kilomita tano, kwanza imechukua huu mwaka wa nne hazijaweza kutengenezwa, na Mkandarasi bado analipwa. Maana nitawasomea jinsi ambavyo Mkandarasi amelipwa na kazi ilisimama tangu mwaka 2024 Waziri akibu swali hili, na kazi imesimama mpaka leo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo tunaletewa usanii wa kusema kilometa 92 zitatengenezwa kwa hela ambayo ni ndogo kuliko ile iliyopangiwa kilometa tano. Kwenye zile kilometa tano, hata kitone cha lami hakuna. Kasehemu kalikotengenezwa ni kujaza mawe, na sehemu hiyo walisema kwamba mkataba ambao ulikuwa uishe baada ya mwaka mmoja umechukua mwaka wa nne, wanasema kwamba walikuwa hawajui kwamba kuna maji chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza, sehemu hiyo walisema imechaguliwa kwa vile ni mbovu. Kwa hiyo, ilitakiwa itengenezwe kwa maana ina matatizo. Sasa ikatengewa shilingi bilioni 6.2. Moja, upembuzi yakinifu haukuwa umefanywa kwenye kipande hicho? Kama ulifanywa, haukuonyesha kama chini kuna maji? Pili, kwa nini mkataba huu ulitolewa kabla ya hata upembuzi yakinifu wa barabara yote haujaisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile kuambiwa shilingi bilioni 5.2 zitatumika kwenye kilometa 5.2, hiyo fedha sasa imekwenda wapi? Ukiangalia huu mradi, ulianza tarehe 1 Septemba, 2021 na ulitegemewa kukamilika Septemba, 2022, lakini mkataba uliongezwa hadi Juni, 2024. Sasa mpaka leo hivi tunavyozungumza hakuna kazi, ilisimama pale pale na gharama ya ujenzi ndiyo hivyo kama nilivyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa kazi hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri akijibu swali ilikuwa 55%. Malipo ya awali (tusikilize hapo vizuri) kwa Mkandarasi yalikuwa shilingi milioni 783, malipo ya hati ya pili ni shilingi milioni 896, malipo ya tatu ni shilingi 1,139,150,000, na deni la Mkandarasi ambalo anadai hati ya nne ni shilingi 1,489,000,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajiuliza, hivi kakipande hako ambako hata pale palipowekwa mawe hapafiki hata nusu kilometa, kama imezidi ni nusu kilometa, huku kwingine kote hakujatengenezwa, na bilioni hizi zimetumika; na hizo bilioni kwenye bilioni sita zilizobaki ziko wapi? Kwa maana Mkandarasi hajalipwa tangu mwaka 2024 mwezi wa Februari, Mheshimiwa Naibu Waziri akilizungumzia pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita nilikuwa kule kuhakiki kwamba Mkandarasi ameanza kazi, hakuwa ameanza. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema hapa kuna uchafu unaofanyika. Kilomita 92 uweke shilingi bilioni sita, kilometa tano uweke shilingi bilioni 6.3, kazi mpaka leo mwaka wa nne 55%, hiyo fedha nyingine imeenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo jana alivyokuwa akichangia Mheshimiwa Halima Mdee alisema, au kuna mfuko mwingine hela inatoka huku, inaingia huku? Kwa hiyo, ina maana barabara hii inatumika kama shamba la bibi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili hiyo, nasema hakuna haja ya kuiweka kwenye bajeti kwa maana mnatuchezea. Malizeni kile kipande, na ionekane hiyo shilingi bilioni 6.3 imetumika kwa sehemu hiyo. Kwa maana mpaka leo hakuna hata kilomita moja ya lami. Hii ni kuonyesha kwamba kwa kweli kuna mchezo mchafu, na haya ndiyo yanasababisha kuomba Special Audit kwa CAG. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia, ahsante sana. (Makofi)