Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi uliyonipa. Nami niungane na Wabunge wenzangu wengine wote, kwanza kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani yake kwa Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii ya Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega amekuwa ni Waziri ambaye anafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Godfrey Kasekenya Msongwe ambaye amekuwa Naibu Waziri kwa miaka mitano hapa. Hii ni ishara kwamba anafanya kazi nzuri, tunampongeza sana. Pia nampongeza sana Katibu Mkuu Balozi Eng. Aisha pamoja na Naibu Katibu Mkuu, ndugu yetu Dkt. Charles Msonde. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetumwa na wananchi wa Jimbo la Lupembe kuchangia mambo mawili katika bajeti hii ya Ujenzi. Jambo la kwanza, wananchi wa Jimbo la Lupembe wamekuwa na kilio cha muda mrefu sana kwa ajili ya hii barabara ya Kibena – Madeke. Barabara hii imeahidiwa tangu mwaka 2000 Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne, na Awamu ya Tano kulikuwa na ahadi ya maneno tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nina faraja kuzungumza ndani ya Bunge lako Tukufu, kwamba nimesoma kwenye hii hotuba ya Wizara ya Ujenzi ukurasa wa 31 Waziri amesema mambo yafuatayo na ninaomba kuyanukuu. Mheshimiwa Waziri anasema, “katika barabara ya Njombe – Kibena – Lupembe – Madeke kilometa 126, sehemu ya Kibena – Kidegembye kilometa 42, taratibu za manunuzi ya Mkandarasi na Mhandisi Mshauri kwa ajili ya ujenzi, zipo katika hatua ya mwisho.” Mheshimiwa Rais ahsante na hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wahenga walisema, moyo usiokuwa na shukrani, hukausha mema yote. Nasi wananchi wa Lupembe tuna imani kubwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwamba hii barabara iliyokwama kwa muda mrefu yeye katika Awamu yake ya Sita atakwenda kuijenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna imani na Mheshimiwa Rais, kwa sababu alituahidi kujenga Makao Makuu ya Halmashauri, amejenga, ameshamaliza. Aliahidi kujenga vituo vya afya, amejenga, ameshamaliza. Aliahidi kupeleka umeme, amepeleka Jimbo zima la Lupembe. Tuna imani na Mheshimiwa Rais, barabara hii atakwenda kuikamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, wananchi wa Lupembe wamenituma pia, pamoja na kutangaza hiki kipande cha kilomita 42, wanashauri pia kutangaza sehemu nyingine ya pili ya kuanzia kule Lupembe ili waje wakutane pale katikati kwa ajili ya ujenzi wa hii barabara iweze kwisha mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, wananchi wangu wa Kijiji cha Nyombo, Kidegembye penyewe, Matembwe, Wanginyi, Lupembe Barazani, Mfiriga mpaka Madeke wanahitaji fidia kwa ajili ya maeneo yao. Juzi nilikuwa kwenye Mwenge kule Njombe, nimekuta kazi ya uthamini wa mali unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la wananchi wa Lupembe, wanaomba maeneo haya yalipwe fidia mapema ili nyumba zao na mali zao ziweze kuwa na thamani sasa. Namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hotuba yake baadaye jioni awapatie matumaini wananchi wa Lupembe, hii fidia yao italipwa lini? Kwa sababu uthamini unaendelea kule sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nakumbuka Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja Lupembe pamoja na Waziri aliyepita, Mheshimiwa Ulega ndiyo bado hajafika Lupembe. Barabara hii ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaombe, barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Mkoa wa Njombe na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Hii barabara inaunganisha mpaka Ifakara kule Mlimba kwa ndugu yangu Mheshimiwa Kunambi mpaka Morogoro kuja hadi Kilosa. Ni barabara muhimu kwa uchumi wa Taifa, ni barabara ya kimkoa. Naomba ipewe uzito kama walivyoahidi kwenye bajeti hii, ujenzi uanze mara moja, wana Lupembe wapate hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ahsante na Mungu awabariki sana. (Makofi)