Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango katika Wizara hii ya Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nami niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo nchi yetu imeendelea kupiga hatua kubwa sana kimaendeleo katika sekta mbalimbali, na jitihada kubwa kwa kweli anayoifanya kuhakikisha kwamba Wizara hii inaongezewa bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miundombinu katika Taifa letu ambao ni uti wa mgongo wa maendeleo wa nchi, inapewa kipaumbele mwaka hadi mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi kwa kazi kubwa kweli wanayoifanya, pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Wizara hii. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana, japokuwa changamoto bado zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunawapongeza sana, na kwa namna ambavyo kwa kweli wamekuwa na ushirikiano mkubwa na Wabunge na kwa vyovyote vile tumekuwa tukiwasiliana pale palipo na changamoto na wakati wote wamekuwa wakisaidia kuchukua hatua za haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie fursa hii kwa kweli kumpongeza Meneja wangu wa TANROADS Mkoa Ndugu Joel Mwambungu, kwa kazi nzuri anavyosimamia barabara za Mkoa wa Shinyanga, lakini na ushirikiano mkubwa anaouonyesha kwetu sisi Wabunge na hususan mimi Mbunge wa Jimbo la Kishapu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Katibu Mkuu kwa namna ambavyo amefikia maamuzi ya kumthibitisha sasa kuwa Meneja wa Mkoa, kwa sababu amekaimu kwa kipindi kadhaa, lakini kazi yake nzuri, ushirikiano na umoja anaouonesha baina yetu sisi Wabunge, kwa kweli maendeleo ni makubwa na barabara zetu sasa zimekuwa katika kiwango kizuri katika Mkoa wa Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nianzie mchango wangu kwa barabara ya Kolandoto – Kishapu. Barabara hii ipo kwenye Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi, na sote tunafahamu Ilani ni mkataba baina ya wananchi na chama. Kimsingi Chama Cha Mapinduzi ndicho kilichoshinda na kikaweka ilani mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa barabara hii ipo kwenye ilani tangu mwaka 2015 – 2020 na 2020 – 2025, lakini barabara hii haijaanza kutengenezwa. Huu mwaka wa fedha 2024/2025 tunaoumalizia ilitengewa jumla ya shilingi bilioni moja kama fedha za kuanzia utekelezaji wa mradi huu. Sasa tumekwenda hatua, barabara hii haijatekelezwa, na hii tunakwenda hatua za mwisho, lakini kwenye hii bajeti mmeongeza shilingi milioni 900. Hizi fedha sielewi, ni ndogo sana. Sijajua labda ni kwa ajili ya mobilization na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nipate majibu sahihi, kwamba barabara hii itakwenda kutekelezwa katika kipindi hiki cha mwaka huu unaoanza 2025/2026? Ama hizi shilingi milioni 900 zilizoongezwa ni kwa ajili ya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, barabara hii ni moja kati ya zile trunk road, ni barabara inayotoka Kolandoto – Kishapu – Lalago – Meatu na hii barabara inaunganisha Arusha – Manyara – Singida. Ni barabara muhimu sana, na barabara hii ikijengwa ikakamilika, itaharakisha sana jitihada za kiuchumi katika mikoa hii yote minne. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ione umuhimu wa kuanza kujenga hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi imejitabanaisha wazi kabisa kwamba, mkakati mkubwa ni kuhakikisha kwamba wilaya na mikoa zinaunganishwa. Sasa barabara hii ndiyo inayounganisha mkoa na wilaya, Wilaya ya Kishapu ina miaka mingi tunahangaika na vumbi. Kwa nini Serikali isifike mahali ikatekeleza takwa la Chama cha Mapinduzi kwa maana ya Ilani, kuhakikisha kwamba barabara hii inapelekewa lami na tutawasaidia wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri atuambie tu, sijajua wanafanya utaratibu gani, lakini trafficking ya barabara hii ni kubwa sana. Kuna magari mengi, kuna malori mengi ambayo yanasafirisha pamba, yanasafirisha kunde; na Mkoa wa Shinyanga tunalima pamba na Kishapu ndiyo inaongoza kwa kulima pamba. Kwa hiyo, kwa kipindi hiki ni vurugumechi, malori yote yanayotoka Singida, yanayotoka Simiyu yanapitia barabara hii, lakini hatuwezi tukaelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka mmoja tumekuwa tukitumia zaidi ya shilingi milioni 600, kufanya matengenezo ya mara kwa mara kwa barabara hii. Kwa hiyo, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuweka lami ili tuondokane na gharama za matengenezo ya mara kwa mara, isiwe tunatengeneza mara nne kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwahurumie wananchi, kwa sababu inafika mahali wazazi wanajifungua barabarani, kwa sababu barabara hii inaharibika mara kwa mara na inakuwa na mashimo makubwa. Sasa kwa nini tusitengeneze barabara hii? Tunahujumu Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, tunakwenda kwenye uchaguzi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Butondo, ahsante, nakushukuru.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini naomba sana Mheshimiwa Waziri kwenye majumuisho, atoe majibu ya matumaini, ahsante sana.