Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MWENYEKITI: Samahani kidogo. Wajiandae Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mheshimiwa Flatei Massay, Mheshimiwa Francis Isack Mtinga na Mheshimiwa Edward Olelekaita Kisau.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wananchi wa Mlimba wameniagiza leo hii nizungumze kwa habari ya barabara inayounganisha Mikoa ya Pwani na Nyanda za Juu Kusini inayopita Mlimba – Njombe. Wameniagiza nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa utashi wake wa kuelekeza fedha shilingi bilioni 167 ziende zikajenge kilometa 100 kipande cha kutoka Ifakara – Miale – Igima kilometa 62.5 na kipande cha kutoka Miale – Igima – Chita JKT pale makutano kilometa 37.5. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina furaha ya kusema tu kwamba tayari vipande hivi vina Wakandarasi, na Mkandarasi mmoja huyo wa kwanza kutoka Ifakara – Miale – Igima, ameshaenda eneo la kazi kwa maana ya kwamba, ameshaandaa camp site na hivi sasa mitambo iko pale na nina taarifa ya kwamba anajenga nyumba kwa ajili ya wataalamu wanaokwenda kusimamia ujenzi wa barabara hiyo. Hivyo, nina kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kipande kingine cha kutoka Kihansi - Madeke tangu mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022 kulikuwa na habari ya kwamba tuna fedha kutoka Benki ya Mendeleo ya Afrika (AfDB). Sasa mpaka leo Waziri ingefaa atueleze wananchi wa Mlimba, kile kipande cha kutoka Kihansi – Mlimba kwenda Mpanga, pale Masagati mpaka Madeke kilometa 93 hali ikoje sasa, kwa maana mkandarasi anayekwenda kufanya usanifu na upembuzi yakinifu wa mradi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mlimba pia wameniagiza, na kwa kuwa kaka yangu Mheshimiwa Ulega, yeye ni kaka yangu, nami ni Mjumbe, na Mjumbe hauawi, wananchi wa Mlimba wameniagiza, wamesema leo hii niondoke na shilingi ya mshahara wake. Wameniagiza, nami ni Mjumbe, nasema tu niondoke na Shilingi ya mshahara wake. Kwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema nia njema ya Mheshimiwa Rais alielekeza barabara hii ijengwe ndani ya miaka mitatu na mkandarasi amesaini mkataba miaka miwili sasa. Je, kazi hii itakamilika kwa miaka mitatu, na hajaanza kazi? Wangependa kupata majibu ya uhakika, maana majibu kila siku wamekuwa wakipata kwamba hatua ikoje na kwa nini sasa miaka miwili wakandarasi wote wawili hawajaanza kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakipata majibu ya uhakika wameniruhusu niondoe shilingi, lakini bila majibu ya uhakika wamesema niondoke na shilingi ya mshahara wa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni kaka yangu, lakini mimi ni Mjumbe, na mjumbe hauawi. Anapofanya majumuisho, wananchi wa Mlimba sasa leo wapo wanafuatilia TBC live, wanataka kusikia kauli yake, unakwenda kusema nini kwa habari ya mkandarasi huyu kuanza kazi sasa? Huyo wa kwanza kipande cha kutoka Ifakara kuja Miale - Igima na wa pili kutoka Miale - Igima kwenda Chita wataanza kazi lini? Wakishapata majibu ya uhakika, wameniruhusu niondoe Shilingi ya mshahara wa Mheshimiwa Waziri, na apate mshahara kaka yangu na maisha yaendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine namshukuru Mheshimiwa Waziri, amefanya ziara kwenye Jimbo langu kujionea hali halisi. Sasa nimpe taarifa, lile eneo la Mpanga ambalo sasa barabara imekatika na kuna bwawa hivi, tayari mama mmoja amefariki pale mjamzito. Alikuwa anakuja kupata huduma ya afya kwenye hospitali ya Wilaya ya Mlimba hapa Mngeta, amefika pale barabara haipitiki, na amefariki. Mimi ninamwombea huko aendako Mungu ailaze roho yake mahali pepa Peponi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hizi ni kadhia ambazo wananchi wanazipata. Mheshimiwa Waziri you can feel. Sasa tangu utoke hamna kilichofanyika. Ninavyozungumza na wewe mpaka sasa ulikwenda kushuhudia, lakini mpaka sasa hali ipo vile. Magari ya kule yamebaki kule na hata eneo lile la Ngwasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Ngwasi alipoenda Mheshimiwa Waziri, mpaka sasa kuna magari yaliyotoka Njombe – Mlimba yamebaki. Kwa hiyo, hakuna mwananchi anayefika Ifakara, hakuna mwananchi anayesafiri kwenda Dar es Salaam. Kwa hiyo, hiyo ndiyo hali halisi ya sasa, na Waziri akisema neno moja, nadhani wananchi wa Mlimba watafarijika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili tulikuwa na miradi hapa ya fedha za Benki ya Dunia. Eneo lile la Mpanga lingepaswa kupata fedha zile, lakini nashangaa kwa nini zilikwenda maeneo mengine, lakini Mpanga hawakupata pale bajeti ya daraja la kudumu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende eneo lingine. Nimeyataja maeneo korofi, Ngwasi na Mpanga, lakini niende kwenye eneo la fedha za maendeleo. Mheshimiwa Waziri labda atueleze wapi tunakwama? Kwa nini karibu mikoa yote hawapelekewi fedha za maendeleo? Kwa mfano Mkoa wa Morogoro, mimi pale nina mradi wa fedha za maendeleo, barabara ya lami kipande cha mita 400 kata ya Mchombe. Hivi sasa mkandarasi alikuja akasembua barabara, ameacha matope barabara haipitiki, na taarifa niliyonayo, mpaka leo pale kwenye ile njia haipitiki sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe kwa kusema kwamba niombe na nishauri Wizara...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda umeisha, ahsante sana.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu kuwa na miradi michache ambayo itakamilika kwa wakati kuliko kuwa na miradi mingi ambayo kimsingi haiwezi kukamilika.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba kuwasilisha na naomba niunge hoja mkono kwa sababu ninaamini wewe ni mtu rahimu sana. Utaenda kutupa majibu ya faraja wananchi wa Mlimba leo hii, nami nitasikiliza hapa kwa sababu nitashika Shilingi baadaye. (Makofi)