Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Michael Constantino Mwakamo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kama kawaida ya kila mmoja kushukuru. Naishukuru Serikali na Mheshimiwa Waziri na Watendaji wake wote wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda ni mchache naomba nimweleze Mheshimiwa Waziri kwamba leo nitachangia katika sura ya kumpa salamu nilizopewa nimpe. Pale Mlandizi baada ya jana kuwasilisha hotuba yake, wapo walionipigia simu, wapo waliompongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais, nami mwakilishi wao nafanya hivyo kwake na kwa Mheshimiwa Rais. Hongereni sana kwa kazi inayofanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia nachukua nafasi ya kushukuru sana kwa sababu nilipoingia hapa nilizungumza habari ya barabara ya Makofia – Mlandizi, Mlandizi – Mzenga mpaka Mwanalumango kwa kila hotuba ya bajeti iliyokuwa mbele yangu kwa kipindi ambacho nimeishi hapa na niliuliza maswali mengi sana juu ya barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maswali na michango hiyo niliyoitoa, na kutokana na hotuba ya jana, baadhi ya watu walinipigia simu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri. Pia, wameniambia nimpe salamu, tena wamenilazimisha nimpe salamu hiyo kwa lugha ya Kizaramo. Kwa kuwa yeye ni Mzaramo, wamenipa methali mbili kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, wameniambia nimwambie kwamba, “Mkulwa nyamale kalimanduage.” Naye anajua salamu hii amenipa Mzee Matambo, na kwa sababu Bunge hili linasikilizwa na wengi, “Mkulwa nyamale kalimanduage”, ina kwa maana kwamba, “ukiona mtu mzima amenyamaza, ananyamaza tu kwa kukataa kelele, lakini yapo mambo mengine yanawezekana akabaki na mashaka nayo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mzee Matambo ameniambia nimwambie methali hii. Pamoja na kumpongeza, anataka kujua fidia ya watu wa Makofia - Mlandizi – Mzenga – Vikumbulu. Pia, pongezi wanayompa, tarehe 4/5/2025 kwenye hotuba yake jana walisikia akisema barabara ya kilometa 23 kutoka pale Mlandizi kwenda Ruvu Stesheni kwenye Stesheni ya SGR itasainiwa. Kwenye hotuba, Mheshimiwa Waziri alitumia lugha hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameomba nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba wanamshukuru kwa sababu juzi tarehe 4/5/2025 mkandarasi ameshasaini barabara hii na wamemwona Mlandizi akitembea kutafuta sehemu ya kuweka kambi. Wameniambia nimshukuru sana, ila nimwombe amwambie awahi kuweka kambi wamwone kwa sababu ujenzi wa barabara ni kukuza Uchumi, lakini ujenzi wa barabara kwa Jimbo langu la Mlandizi na hata Waziri nafikiri anafahamu kwamba ujenzi wa barabara ni siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi tulichonacho wanatarajia wasione kuishia kusaini, wanatarajia waone kazi zikiwa zinaendelea. Mheshimiwa Waziri, niendelee kumpongeza kwa sababu kwenye hotuba hii nimeona amezitaja barabara ambazo zinakatiza Mlandizi kwa maana ya Jimbo la Kibaha Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ametaja Barabara ya Makofia -Mlandizi kwamba ipo kwenye hizo hatua, ametaja Barabara ya Chalinze – Utete, ametaja barabara hiyo ya kilometa 23 ya Mlandizi kwenda Ruvu, lakini imetajwa Barabara ya Kisarawe – Mlandizi ambayo ndiyo hii hii ya Kisarawe – Mwanalumango ambayo inapita Mzenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, imetajwa Barabara ya Kibaha – Mlandizi - Chalinze hadi Dodoma ambayo itajengwa kwa PPP kwa maana ya barabara ya mwendokasi. Hizi barabara kwa kweli zikifunguka ni uchumi mkubwa sana wa maeneo yetu. Kwa hiyo, naomba sana atakaposimama hapo baadaye, kwa kweli katika lugha yoyote atakayoitumia, ajaribu kuifafanua namna ya watu hawa watakapopata fidia yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ya barabara zote alizozitaja ndiyo msingi wa kupata nguvu ya kuona barabara zinakwenda kutekelezwa. Kwa hiyo, wangeomba sana atakaposimama atuelezee vizuri namna ya barabara hii mojawapo iliyotiwa saini ya kwenda SGR, lakini pia hiyo ya Makofia – Mlandizi namna ya watu ambavyo wamesimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, methali ya pili walioniambia nimwambie Mheshimiwa Waziri kwa lugha hiyo hiyo wameniambia nimwambie, “ngwengwe mdisolo jaki.” Yeye ndio yupo Wizarani leo, hizi barabara zilizotajwa anazijua vizuri. Kwa hiyo, muda wa kukaa Wizarani, asiishie kuzitaja. Wanamwomba sana azisimamie ziende kwenye utekelezaji ili baada ya kutekelezwa, basi zifunguke na wananchi waendelee kutumia barabara hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine najua Wizara hii inasimamia kuzifungua hizi barabara zinazokwenda kwenye Stesheni za SGR na Serikali imeweka fedha nyingi sana. Kwenye Jimbo la Kibaha Vijijini ipo barabara inaitwa Kongowe – Soga ina urefu wa kilometa 15. Barabara hii kule mbele ina Stesheni ya SGR na ina uwekezaji mkubwa sana wa viwanda.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, barabara hii aichukue nayo aiingize kwenye utekelezaji kwa sababu ni barabara inayotekelezwa na inatarajiwa sana na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)