Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Newala Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Pia namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya pamoja na wasaidizi wake wote wakiwemo Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na timu yake yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukienda ukurasa wa 48 wa hotuba kipengele (b) kinazungumzia miradi ambayo ipo wenye upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Katika kipengele hiki, ipo pia Barabara ya Mtama – Mkwiti – Kitangani – Newala ambayo urefu wake ni kilometa 74. Barabara hii ilishatengewa fedha kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 shilingi milioni 145 kwa ajili ya zoezi la upembuzi yakinifu. Nimeangalia kwenye hotuba hapa, barabara hii sasa ipo kwenye upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu fedha imetengwa mwaka 2023/2024 na leo ni 2024/2025 bado ipo kwenye upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Naomba wakati wa kuhitimisha bajeti Serikali ituambie ni lini usanifu wa kina utakamilika ili barabara hii iende kwenye hatua ya ujenzi kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimesoma hotuba ya Bajeti ukurasa wa 36. Naishukuru Serikali imezungumzia barabara ya kutoka Kongowe – Kibiti hadi Lindi. Katika kipengele hiki au katika sehemu hii nimeangalia Serikali inasema inatafuta fedha kwa ajili ya ukarabati wa sehemu mbalimbali. Sasa kwenye sehemu mbalimbali hizo, nimeishika ile ya Kongowe mpaka Marendeko kilometa 160 na Nangurukuru – Mbwemkuru kilometa 95. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba Serikali inatambua umuhimu wa hii barabara, lakini pia niishukuru kwa sababu ilikuwa haipitiki katika baadhi ya maeneo. Serikali ilikesha pale kutafuta namna ili wananchi waweze kuvuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuishauri Serikali kwamba ile barabara inapita kando kando ya bahari na ardhi yake ni oevu. Leo tunaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati. Nilikuwa naomba, kwa sababu hii barabara ni mbovu kuendelea kukarabati kila wakati ni sawa na kumpa panadol mgonjwa ambaye yupo mahututi, kila siku unampa tu panadol unamwongezea shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, Serikali badala ya kujikita kutafauta fedha kwa ajili ya ukarabati, sasa itafute fedha kwa ajili ya kujenga upya hii barabara ili kuondoa changamoto iliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kama unaenda jimboni ukitumia hii barabara, unapofika kule, lazima gari yako baadhi ya vipuli viwe vimeharibika kwa sababu ya ubovu wa barabara uliyopo. Kwa hiyo, naomba na kuishauri Serikali kwamba sasa ifike wakati itafute fedha kwa ajili ya ujenzi na siyo kuendelea kukarabati kila wakati suala ambalo linaiingizia Taifa fedha nyingi zinatumika lakini kila siku tunaenda kukarabati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo pia Barabara ya Mtwara – Mnivata - Tandahimba – Newala – Masasi. Tunaishukuru Serikali kwamba ilitenga fedha, wakandarasi wapo site. Tunashukuru kwa hizo jitihada kwa sababu ni barabara ya muda mrefu na imekaa kwenye ilani kwa muda mrefu pia. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali, tunamshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye barabara hii, sitaki kuingilia utaratibu ambao wakandarasi wamejipangia, ila nilitaka kushauri, kwa sababu matengenezo yanaendelea, wametengeneza matuta kwa kiasi kirefu hasa kutoka Mnivata – Tandahimba kwenda Newala, kuna tuta refu sana. Sasa nilitaka kushauri kwamba tumeshuhudia mvua zilizopita hapa katikati barabara hii ilikuwa haipitiki kwa maana ya zile diversion ambazo mkandarasi ameziweka, zilikuwa hazipitiki, magari yanakwama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unatoka Newala zaidi ya kilometa 174. Utoke Newala – Kitangali uzunguke Mtama kwenda Mtwara wakati kutoka Newala mpaka Mtwara ni kilometa 140. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri, mkandarasi ni jukumu lake kuhakikisha diversion zake zinapitika muda wote, lakini magari yalikuwa yanakwama, mkandarasi haangalii wala hashughulikii ili wananchi au wale watumiaji wa barabara hii waweze kupita kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwamba ahakikishe wakati wote zile diversion zake zinapitika ili kuwaondolea adha na gharama kubwa watumiaji wa barabara hii wanaotoka Newala kwenda Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru tena kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)