Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuweka barabara yetu hii ya Mbulu – Haydom - Labay kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nina ombi kwa Mheshimiwa Ulega. Ipo Barabara ya Maretadu inaitwa Dongobesh – Maretadu kwenda Haydom. Barabara hii inafaa sasa kupandishwa hadhi kutoka kwenye wilaya zetu kuja kwenye TANROADS kwa sababu ina sifa zote. Kwa sasa hivi, nimwambie Mheshimiwa Waziri, haipitiki kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hali ni mbaya na siyo mbaya, ni mbaya zaidi lakini pia Bashay - Endamilay – Haydom nayo ni mbaya, mbaya zaidi. Kwa hiyo, ombi langu, najua Waziri ni mchapakazi, ninakufahamu tangu tukiwa vijana. Nakuomba sasa huu ndiyo wakati wake umefika wa barabara hiyo kuipandisha ije TANROADS ikafanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo barabara ambayo kimsingi nimekuwa nikiomba mara nyingi hapa, Barabara ya Karatu – Mbulu - Dongobesh – Haydom – Sibiti - Lalago River. Barabara hii inategemewa na Waheshimiwa Wabunge 12 wapo hapa ndani na wangetamani barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini namshukuru Mheshimiwa Rais? Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu amekubali kipande cha Haydom kuja Labay kijengwe kwa kiwango cha lami na walau ametoa 10% kwa mkandarasi ambaye anaendelea na taratibu zinaendelea. Sasa kuna barabara hii ya Mbulu – Garbabi kwa kweli mkandarasi hayupo site. Mimi ninavyoona ni hatari kwa sababu ameshajenga kiwango fulani kimefikia, bado tu kumwaga lami. (Makofi)
Sasa kaka yangu Mheshimiwa Ulega, wewe ni Waziri, umetoka kwenye Wizara ya Mifugo, umefanya vizuri. Nakumbuka tumekuwa kwenye jumuiya ya vijana wote katika mtindo ule wa Chama cha Mapinduzi. Sasa ndugu yangu wewe ukaingia ukawa mNEC, ukaja huku Bungeni, na mimi nikawa Bungeni.
Leo ndugu yangu naomba basi hebu njoo kwenye barabara ile ukawe mwarobaini wa ile barabara, kwa sababu kwanza barabara imesimama, mkandarasi hayupo site na balaa zaidi unajua tena barabara ikisimama haijawekewa fedha, haipitiki kabisa. Kwa hiyo, wananchi hawaitegemei barabara ile kuwa nzuri kwa sababu hakuna fedha inayotengwa kila mwaka kwa maintenance.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Ulega barabara ile haipitiki kabisa. Kwa hiyo, wananchi wanaona kuliko ile lami iliyoanza kuwekwa ni bora ungeweka changarawe ya kawaida kuliko hiyo lami inayoendelea kwa sababu yaliyofanyika ndani ya Bunge hili sitaki kusema. Nimeizungumzia barabara hii mara 25 kwenye hotuba kama hii, lakini nikuombe sasa wewe na kijana mwenzio Mheshimiwa Godfrey, najua ni Mawaziri ambao kwa kweli mnachapa kazi, Mheshimiwa Rais amewaamini amewaweka hapo; wamebadilishwa wengi kuja hapo.
Mimi ninajua kwa Mdengereko hakuna kinashoshindwa. Sasa ndugu yangu nikuombe nenda kaweke fedha pale ili mkandarasi awepo site wamalizie kujenga ile barabara. Kilometa 25 zinakushindaje ndugu yangu? Mimi ninaamini haziwezi kukushinda, nenda pale fanya hivyo. Ile Haydom kwa sababu mkandarasi ameshalipwa 10%, kwa mujibu wa sheria zetu hana haja ya kuacha kujenga barabara. Endelea, watumie ma-engineer wako wamsimamie mkandarasi aendelee kufanya kazi. Kwa sababu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mbulu Vijijini tuna imani na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu barabara ile tangu Mbulu imeundwa au imeanzishwa mwaka 1905 haijawahi kuwa na barabara. Tumemwambia Mama yetu ni msikivu, amekubali kuiweka na imeanza kazi, kilichobaki ni Mheshimiwa Waziri kuisimamia na ndio ana instrument ya kusimamia barabara hii. Wasimamie barabara hii ili ijengwe kwa kiwango cha lami na iweze kumalizika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini ya kwamba kwa kuwa Mheshimiwa Rais alishakuja, na kwa kuwa aliahidi barabara hii, asije akaonekana mwongo wakati ninyi mpo, kwa sababu imeshaanza, ni kiasi cha kusimamia tu barabara hii. Ombi langu ni kwamba wasimamie barabara hii ili ikamalizike kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani nasema hivyo? Ukiangalia kwenye hii bajeti, mimi nafurahi Mheshimiwa Ulega nimeona ameniweka kwenye bajeti yake, ameitengea fedha iendelee kujengwa, lakini kwa sasa kwa sababu hali yake ni mbaya, maana yake angeendelea kuijenga, ingeshamalizika kabisa. Yapo matatu pale ninaomba ayamalize, kwa sababu mkataba wa yule mkandarasi umekwisha, basi uhuishwe ule mkataba ili mambo haya yaendelee na mkandarasi awepo site aendelee kujenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nakuomba kwa sababu Waziri ni kijana mwenzangu, ndani ya mwezi huu atembelee ile barabara akawape matumaini wananchi wa Mbulu kwamba barabara inajengwa au iweje, naye akaone adha wanayoipata wananchi wa Mbulu Vijijini na hasa Mbulu Mjini na Karatu pia wananchi wa Singida na Meatu, awape matumaini, kwa sababu ukishaanza kuepeleka yale material site, juzi nimeona wamepeleka kule magreda yameanza kufanya kazi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Sasa wananchi wasije wakaona ndiyo kampeni, kumbe kazi inaanza. Mheshimiwa Waziri njoo uwathibitishie kabisa kwa sababu muda umefika wa barabara hiyo kujengwa.
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.