Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 116 paragraph 321kwenye bajeti yako Mheshimiwa Waziri, umeongelea baadhi ya barabara za Singida, lakini sijui ni kwa bahati mbaya au ni kwa vyovyote, sijaona barabara ya kutoka Iguguno kupita Makao Makuu ya Wilaya pale Mkalama kwenda Sibiti na hatimaye kuunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu. Barabara ambayo kwa kipindi changu chote cha miaka minne Bungeni nimekuwa nikiisemea kwenye maswali na kwenye mchango, lakini mpaka sasa hatuna barabara ya lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana, barabara hii ni ya kiinchi. Barabara za Mkoa wa Singida ni barabara za nchi kwa sababu zinagawa nchi katika pande zote nne. Ukitoka mashariki mwa nchi, Dar es Salaam kwenda Mwanza Magharibi mwa nchi, ni lazima upite Mkoa wa Singida, ukitoka Kaskazini mwa nchi kwenda Kusini ni lazima upite Mkoa wa Sigida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii barabara ya Iguguno, kupita Mkalama kwenda Sibiti mpaka Mkoa wa Simiyu inaunganisha Mikoa ya Mara, Simiyu na sehemu ya Mkoa wa Mwanza. Nashauri kwamba hata Wabunge wote wa mikoa hii kwa pamoja kabisa tungeungana kusema kwamba bajeti hii haipiti bila kuweka fedha kwenye hii barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka wenzetu wa Dodoma na Manyara mpaka Arusha, mimi nikiwa bado mdogo, nasikia wale akina Mheshimiwa Kwang’u waliungana wakasema bajeti haipiti; ndiyo hii barabara leo ina lami. Mimi nadhani kuna kila haja, Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Simiyu, Mkoa wa Mara hebu tuungane kwa pamoja kwamba bajeti hii isipite bila barabara hii kuwekewa fedha, kwa sababu ni barabara muhimu inaunganisha Mkoa, ina uchumi, pamba inapita. Watu wa Simiyu leo mkiwa mnaenda Simiyu mnapita Mwanza, mkipita hapo Singida mnaenda karibu kilometa 200 tu, sasa sijui hii barabara itajengwa lini, na upembuzi yakinifu tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kilometa kumi ziko pale nimepewa pale Makao Makuu kwenye hii barabara pamoja na taa zake kwa bajeti inayoisha, lakini hata mkandarasi bado hajafika pale. Hili jambo jamani, Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu, Mwenyekiti mwenzangu wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Pwani mimi nikiwa Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Singida, Mjumbe wangu wa Baraza, tafadhali bwana, mimi Ubunge bado naupenda kaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkalama wameniambia wanahitaji tu barabara, basi nikae vipindi vingine vitatu. Kwa hiyo, nakuomba sana, hii barabara ni mfupa, hebu wewe utafune huu mfupa. Kama wenzako waliopita wameushindwa, hebu wewe utafune, maana upembuzi tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni ya muhimu sana, Iguguno, Mkalama, Simiyu kupita daraja la Sibiti ambalo limejengwa kwa mabilioni ya fedha ili tu barabara za lami ziweze kupitika na kuchukua uchumi wa upande ule kuleta huku Dar es Salaam na sehemu nyingine. Tafadhali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitika sana, baada ya kuiangalia kwenye kitabu sijaona sehemu ambako barabara hii imetajwa kwa umuhimu kabisa, sijaona hata zile kilometa kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, angalieni hii barabara, mnapita wote mkienda kwenye Kamati, wote lazima mpite kwenye barabara hii ya vumbi. Kwa hiyo, kila mmoja ajue hii ni barabara ya nchi. Ukitoka Dar es Salaam unaenda Simiyu, unatembea kwa lami, ukifika pale unaingia kwenye vumbi, kuna maana gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani unaweza kuvaa suti halafu chini ukavaa suruali ya jeans, haijaungana! Unatoka Mwanza unapita kwenye vumbi, halafu baadaye unaanza lami tena. Hebu kwa pamoja kabisa tuone kwamba hii barabara ni ya kitaifa, na siyo barabara ya Mkoa wa Singida kabisa. Hii barabara ni ya kitaifa kwa sababu huwezi kwenda upande wowote wa nchi bila kupita Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, Rais wetu ametutendea mambo mengi makubwa, na hii barabara ameshaipitisha, amenipa kilometa kumi, kilichobaki ni utekelezaji tu ambao unatakiwa uanze kwenye bajeti inayoisha na hii inayoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi angalau hizi kilometa kumi ambazo nimepewa, waongezee na hii bajeti hata kilometa nyingine 30 angalau basi kilometa 42 kutoka Makao Makuu ya Mkoa mpaka pale Makao Makuu ya Wilaya angalau na sisi tuione lami. Katika Jimbo la Mkalama, kilometa mbili tu, ile sehemu inayopita Iguguno ndiyo kuna lami tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhalini sana, sijui nifanyeje nipige magoti tena hapa, labda mbele ya hili Bunge ili niweze kusikilizwa. Mimi bado kijana sana, bado nautamani Ubunge, nimekaa miaka mitano, bado wananchi wangu wananihitaji.

Mheshimiwa Waziri, hii barabara nakuomba, niko chini ya miguu yako, natamani kulia kabisa machozi, na haya ni machozi ya wananchi wa Mkalama kwa miaka mitano mfululizo tunaomba hii barabara. Zaidi ya miaka kumi, alianza Mheshimiwa Msindai, ameomba ikashindikana; akaja Marehemu Mheshimiwa Mwambu ameomba, amekuja Mheshimiwa Allan; na mimi sasa, angalau nimepewa mengi, basi hili la barabara limaliziwe ili angalau niwe na uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. Tafadhali sana, namwomba Mheshimiwa Waziri, barabara hii ni ya muhimu sana, ahsante. (Makofi)