Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Kwa sababu ya muda, Mheshimiwa Waziri na timu yenu, wote hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nazungumzia barabara mbili; barabara ya Handeni – Kiberashi – Kijungu - Kibaya – Njoro - Chemba mpaka Singida, na barabara hii ina sifa nyingi sana. Kwanza barabara ilikuwa kwenye mradi wa EPC+F na tumesaini mikataba tangu miaka miwili iliyopita, lakini nakushukuru kwa sababu bajeti yao hapa ukurasa wa 19 wamesema, hizi barabara zote za EPC mpango wa kujenga uko pale pale na wameshabadilisha mikataba. Ushauri wa kisheria tu ni kwamba unaposaini mikataba ni lazima barabara hizi zijengwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu kwa sababu kwanza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia ametoa agizo hapa wakati wa ziara ya Tanga na kwenye bajeti yenu hapa wamesema tayari TANROADS na TPA wameanza majadiliano kuhusu namna bora ya utekelezaji wa agizo hili la Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, agizo la Rais lazima liwe na timeframe. Kwa hiyo, tunategemea baadaye Mheshimiwa Waziri anapokuja kwenye mjadala atuambie sasa hao TPA na TANROADS wanafanya majadiliano kwa muda gani? Kwa sababu wananchi wanataka kusikia barabara hii inajengwa. Barabara hii ni muhimu sana, kwani Mradi wa Bomba la mafuta unapita kwenye barabara hii, Bandari ya Tanga imejengwa, magari zaidi ya 533,995 yanapita kwenye barabara hii kwa mwaka. Barabara hii itawapunguzia watu wa Tanga kuja Dodoma kwa zaidi ya kilometa 110. Kwa hiyo, ni barabara muhimu sana, lakini barabara hii ni ya wakulima, wafugaji na wananchi wa vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni barabara inayounganisha mikoa minne, Tanga, Dodoma, Manyara na Singida. Barabara hii itapita pia Manyara ambayo iko kwenye mikoa ambayo ina kiwango kidogo cha lami zaidi ya kilometa 200 hivi. Kwa hiyo, ni barabara muhimu sana. Kwa hiyo, rafiki yangu Mheshimiwa Ulega akija atuambie hayo majadiliano yanachukua muda gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunashukuru kwa sababu kwenye ukurasa wa 119 wamesema watajenga kilometa 50 kutoka Kibaya kwenda Kisima, na kwa kweli hii itatusaidia sana, lakini ushauri wetu tu wa kisheria ni kwamba, kama majadiliano yanaendelea kati ya TPA na TANROADS kuhusu barabara na agizo la Mheshimiwa Rais kujengwa barabara hii yote mpaka Singida, basi wafanye haraka ili tu-negotiate hizi kilometa 50 tuzihamishe kutoka Kibaya zije Kongwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba waanze kujenga barabara hii ya Kongwa kutoka Kibaya kilometa 50. Mheshimiwa Spika Mstaafu, naye atapata kilometa kumi pale. Unajua, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tutahamisha tu, kama barabara hii watasaini na wataji-commit kwamba hii barabara itajengwa na ushauri mwingine, kwa kuwa hii barabara ni ndefu sana, kwenye negotiation, wahakikishe inajengwa kilometa mia mia na wahakikishe wanakuwepo wakandarasi wengi kwa sababu mradi wa kwanza sijui kutoka Tanga hadi ifike Singida itachukua muda mrefu sana. Huu ni ushauri mwingine wa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Kongwa – Kiteto - Simanjiro, tumeona wanajenga kilometa 70 hapa, tunashukuru sana, lakini tunataka tusikie kauli hii vizuri kwa sababu tulikuwa tunaambiwa ikitoka Arusha ikifika Losinyai sijui inarudi tena Arusha. Tunataka hizi kilometa 70 zianze kujengwa ili tujue kwamba hii barabara ambayo ni nzuri sana inajengwa. Inapitisha magari 583,270 zinapita kwenye barabara hii kwa mwaka. Ni barabara ambayo inaunganisha mikoa mitatu; ni barabara muhimu sana, na kwa sababu zilikuwa kwenye mkataba wa EPC+F, wamesema hapa kwamba wameshahuisha mikataba na kwamba barabara hizi zitajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi barabara zitawanufaisha sana wananchi wa Kiteto, na unajua Kiteto ni breadbasket. Hii barabara itasaidia sana kufungua uchumi wa Manyara na wananchi wa Kiteto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri aliniahidi taa 50 za barabarani, hizo tunataka tupate majibu leo. Tunataka ule mji wetu wa Kibaya upendeze. Tunashukuru kwenye ukurasa wa 263 tumeona ametutengea shilingi milioni 300 kwenye ile barabara ya Kibaya - Chemichemi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Edward.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kuna barabara mbili tunataka tuzipandishe ziende TANROADS, barabara ya Dosidosi - Dongo kilometa 56 na barabara ya Kiperesa kilometa 45, hiyo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)