Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza naunga mkono hoja; pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Wataalam wote katika Wizara hii. Kipekee hapa nampongeza Engineer wa Mkoa wetu, Eng. Salehe, anafanya kazi nzuri, ana-respond kwa haraka sana kwenye matukio. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru sana Serikali kwa mradi wa barabara ya Kitai - Rwanda kilometa 35. Mradi huu ulikuwa ukamilike mwezi Disemba, 2023 lakini mpaka hivi leo mradi huu bado uko nyuma sana. Sasa leo nataka nipate majibu hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana, yanapita magari makubwa yanayosafirisha makaa ya mawe. Makaa ya mawe yote yanayouzwa nchi hii, kwa kiasi kikubwa yanatokea katika njia hii, na imekuwa kero kubwa kwa wananchi wanaokaa sambamba na barabara hii, kuanzia Ruanda, Paradiso, Amani Makoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili lote wakati wa kiangazi linakuwa na vumbi jingi sana. Sasa hivi wakati wa masika hii kwa sababu magari yanayobeba makaa ya mawe ni mazito mazito, ile barabara sasa hivi haipitiki, na ikipitika basi wananchi wale kipande kidogo cha kilometa 20 wanatumia masaa mpaka sita. Kwa kweli haileti afya kwa eneo linalotoa rasilimali kubwa kama hizi halafu hatuoni umuhimu na hatutoi kipaumbele kutengeneza hizi barabara.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri mtani wangu naomba utakapokuja kutoa hitimisho hapa, utueleze wananchi wa Mbinga ile barabara ambayo ilipaswa kwisha mwaka 2023 itaisha lini? Pengine usiposema vizuri, leo kwa mara ya kwanza nami nitashika Shilingi kwa sababu sioni sababu kwa nini barabara inayopitisha rasilimali nyingi isijengwe mpaka leo na kukamilika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha pili kuanzia Rwanda hadi Lituhi tunashukuru mkandarasi tayari wameshampata, bado hajapewa fedha za awali kuanza kazi. Sasa na yeye lini anapewa fedha kuanza kazi? Kwa sababu ile barabara inatoka pale Ruanda mpaka Lituhi, na Ndumbi, tumejenga bandari nzuri ya kisasa, lakini ile bandari haitumiki kwa sababu mzigo hauwezi kupita kutoka hapa Ruanda kwenda hadi pale Ndumbi. Kwa hiyo, huyu mkandarasi tuliyempata, ni lini anapewa fedha na anaanza kujenga? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, namshukuru sana, barabara ya Kigonsera, Matiri mpaka Mbaha. Barabara hii Mheshimiwa Rais alipita akatoa ahadi ya kutujengea kwa kiwango cha lami, sasa hivi tayari nimeona upembuzi yakinifu umeanza, sasa ni lini unakamilika na lini barabara ile inaenda kujengwa? Kwa sababu Mbaha tuna jambo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa barabara hii umeongezeka sana kwa sababu inatoka Kigonsera inaenda Matiri halafu inafika Mbaha na barabara yenyewe siyo ndefu, ni kilometa 55 tu. Kwa nini tusiijenge, kwa sababu tuna jambo letu pale Mbaha? Naomba sana, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kusimama hapa, atueleze sisi Wanambinga na wananchi wa Mbaha Jimbo la Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni barabara ya kutoka Mbinga kwenda Litembo kupitia Kindimba, lakini na ile ya Ndengu kuelekea Litembo na yenyewe inafika hadi Nyasa. Barabara hizi ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kujengwa kwa kiwango cha lami. Nashukuru sana upembuzi yakinifu wa barabara hii umefanyika. Sasa lini tunapeleka fedha na kuzijenga hizi barabara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kadhaa nimesema hapa, pale Litembo kuna hospitali teule, wananchi wa Mbinga pale ndipo tunapotibiwa toka enzi na enzi, lakini tunafika kwa shida sana. Kwa hiyo, tunaomba, Mheshimiwa Rais aliona haja ya kupeleka lami pale. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, mtani wangu atekeleze hilo kwa kupeleka hiyo lami, kwani tayari upembuzi yakinifu umefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni ya kutoka Nyoni kuelekea Maguu hadi Kipapa na yenyewe inafika hadi Ziwa Nyasa. Barabara hii iko kwenye Ilani ya Chama hiki ambayo sasa tunaenda kuikamilisha. Tayari upembuzi yakinifu umekamilika. Nashukuru inajengwa kipande kipande, sasa ni lini tutaijenga yote kuanzia mwanzo hadi mwisho ili wananchi wa Bonde la Gati wapite na wanufaike na maendeleo ya Chama hiki cha Mapinduzi?
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa mara nyingine naunga mkono hoja hii. (Makofi)