Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuchangia Wizara ya Ujenzi. Nami niungane na wachangiaji waliotangulia kupongeza sana juhudi za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nia njema ya kuhakikisha kwamba Wizara hii inatengewa bajeti ya kutosha kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ndani ya Majimbo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia njema ya Mheshimiwa Rais tunaiona kupitia bajeti ya Wizara ya Ujenzi ambapo mwaka 2024/2025 Wizara hii kwa upande wa maendeleo ilitengewa shilingi trilioni 1.6, lakini leo tunaona ongezeko la 30% ambayo imetengewa shilingi trilioni 2.189, ni pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, napongeza Wizara hii chini ya Comrade Abdallah Ulega, ambaye kwa kweli kwa speed ambayo ameenda nayo, tunaona ni speed and standard katika kusimamia barabara hizi ambazo katika kipindi chake ameingia kipindi cha changamoto, lakini aliweza kukabiliana nazo na kuhakikisha kwamba hali halisi ya miundombinu ndani ya Wizara yake inarudi katika mfumo wa kawaida, akisaidiwa na Mheshimiwa Engineer Godfrey Kasekenya ambaye pia amekuwa Mtendaji mzuri ndani ya Wizara hiyo bila kusahau Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa TANROADS, pamoja na Mameneja wetu wa Mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Engineer wangu wa Mkoa Eng. Ntuli pamoja na wasaidizi wake ambaye amefanya kazi nzuri ndani ya Mkoa wetu na Wilaya ya Misenyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hasa kwa upande wa Misenyi, na kwa niaba ya wananchi wa Misenyi kutoa pongezi kwa kazi kubwa ambayo kupitia Wizara hii TANROADS imefanya kazi kubwa na kazi za barabara zote ndani ya Wilaya yetu ambazo ziko katika hatua za ujenzi. Nyingine zimekamilika, lakini na nyingine ziko katika hatua mbalimbali, nami kwa niaba ya wananchi hao nashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimerejea katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri, ukiangalia ukurasa wa 292 kuna upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara ambayo nimekuwa nikiililia sana hapa Bungeni, barabara ya Katoma – Kanyigo – Bukwali kilometa 38.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara kwa kweli Serikali imekuwa ikitusaidia, tunajenga mita 400, mita 100, lakini imeweka katika utaratibu wa upembuzi ili sasa ikikamilika naamini Mheshimiwa Waziri hataniacha ili kuweza kuijenga kwa pamoja ili wananchi hao angalau waweze kufaidi lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, Serikali imeweza kututengea bajeti ya shilingi milioni 100 katika eneo hilo na imenipa mita 400 za lami ziendelee kujengwa. Naishukuru sana Serikali kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa niaba ya wananchi wa Mutukula, tunayo barabara ya Mutukula – Kakunyu. Hii ni barabara ya usalama kilometa 46 ambayo inaimarisha usalama katika eneo letu, tukijua kwamba tumepakana na nchi ya Uganda, na yenyewe ipo katika upembuzi na usanifu. Mheshimiwa Ulega naomba na hii barabara ni ya muhimu sana kwa Wilaya ya Missenyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kushukuru wananchi wa Missenyi kwa barabara ya Bunazi Junction - Kagera Sugar kilometa 25. Hii barabara tangu mwaka 2023 tulikuwa kwenye kuomba, mkandarasi alisaini, lakini mwaka huu Serikali imetupatia fedha shilingi milioni 300 tumelipa fidia, imetupatia fedha shilingi bilioni 5.4 mkandarasi ameshapewa advance ana-mobilize vifaa vyake kuanza kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru zaidi Serikali kwamba katika bajeti yake imeweka tena shilingi bilioni mbili katika barabara hii. Kwa hiyo, mkandarasi wetu anafanya kazi akiwa na uhakika kwamba akiomba certificate inayofuata atalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara ya Ujenzi kwa barabara ya Minziro - Mutukura ambayo imeendelea kufunguliwa. Imeshafungua takribani kilometa nane na hapa imenitengea tena kilometa nne, shilingi milioni 100. Hii ni barabara ya kimkakati, na ninashukuru sana kufungua mazingira ya kiuchumi kwa wananchi wetu wa Mutukula na Minziro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa kuboresha maeneo ya Makao Makuu ya Wilaya yetu hasa Bunazi, kuna takribani mita 400 kiwango cha lami ambacho imenitengea zaidi ya shilingi milioni 105 na kuboresha barabara ya Nyabiyanga kwenda Kasambya, wananchi hao waweze kuwa katika barabara zenye ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo haya, tuendelee kushukuru barabara yetu ya Kyaka – Katoro - Ibwela mpaka Ketema na yenyewe imeanza na kilometa kumi, lakini basi niombe speed iongezeke ili na upande wangu wa Missenyi, upande wa Kyaka - Katoro uweze kufikiwa na tuweze kutengeneza barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naendelea kushukuru kwa ajili ya barabara ya Minziro – Kasambya, ilikuwa na changamoto, Mheshimiwa Naibu Waziri alifika kwa sababu sasa hivi imenyanyuliwa kwa kiwango kizuri kama tuta, wananchi hao kero ya maji yaliyokuwa yanajaa barabarani na wananchi wetu waliokuwa wanaenda kuhiji kule Minziro, wanaenda kwa usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, tuliomba taa za barabarani Kyaka, zimefungwa, lakini ni chache, Bunazi na Mutukura bado. Naomba sasa tumalizie kipande hicho ili wananchi hao waweze kufaidi taa za Mheshimiwa Dkt. Samia. Pia, naomba barabara ya Mshenye ambayo inaenda Mshenye -Bugandika – Kitobo - Buyango hadi Ruzinga na yenyewe iingie kwenye usanifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati namalizia, namshukuru Mheshimiwa Waziri, sasa namkaribisha angalau afanye ziara Wilayani Missenyi ili tuweze kukagua hizo barabara na kuweza kuhakikisha kwamba zinajengwa katika kipindi kinachokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)