Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi. Nami namshukuru Mungu kwa kunipa pumzi jioni hii niweze kuchangia Bajeti ya Wizara hii adhimu, Wizara ambayo ndiyo mishipa ya nchi.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira yake njema ya kuifungua nchi na kuunganisha mkoa na mkoa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napongeza pia juhudi za Wizara hii katika kuhakikisha miundombinu hii ambayo ndiyo matarajio yetu, inakuwa imara kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, zipo changamoto, lakini nampongeza Mheshimiwa Waziri, kijana wangu huyu, Mheshimiwa Ulega, Baba Tulia, kwa weledi wake. Amepokea kijiti hiki katika kipindi ambacho tunaamini ataisaidia nchi hii.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yake, Ukurasa wa Sita, ameonesha, ameanzia ukurasa wa tano, namna ya kuunganisha makao makuu ya mikoa na mikoa. Paragraph ya 16, ukurasa wa sita, Sehemu ya Nne, ameonesha pia Barabara ya Singida – Mbeya, sehemu ya Mlongoji – Itigi – Mkiwa, eneo ambalo ndiyo mimi naliwakilisha katika Bunge lako hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yuko mkandarasi pale anaitwa CHICO, ni mkandarasi mahiri sana kwa kazi zake. Tumeona jinsi anavyojenga barabara maeneo mengine, na kwa hakika kazi yake ni nzuri.
Mheshimiwa Spika, ziko changamoto. Naomba Serikali kwa ujumla, Wizara hii ya Ujenzi na Wizara ya Fedha, Mkandarasi huyu ame-raise certificate nyingi, anadai fedha nyingi, anadai zaidi ya shilingi bilioni tisa na point. Sasa amesimamisha kazi huu ni zaidi ya mwezi wa 11 toka kazi imesimama.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa eneo lile matarajio yao yalikuwa ni kwamba barabara hii ikifunguka na wenyewe watanufaika na Uchumi, na watakimbizana katika kutafuta riziki zao kwa namna ambayo ni halali. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Mbeya.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mbeya unapakana na Zambia kwa maana mtu akitoka nchi Jirani, anavuka Tanzania kwenda nchi nyingine, hawezi kupita hapa Dodoma. Akitokea Mbeya akaja kwangu Itigi atapita Singida.
Mheshimiwa Spika, aidha, anakwenda kupitia kule Daraja la Sibiti kwenda Mara ambako atapakana na Nchi ya Kenya au atapita kwenda Babati – Arusha – Namanga au atapita Babati – Arusha – Moshi – Holili. Akipita njia hii atapunguza kipande kirefu cha barabara ukilinganisha na kama anatokea njia hiyo apite, kwa mfano, mpaka ule wa Namanga. Akitokea Namanga kuja Arusha - Babati, aje Dodoma, aje afike Mbeya, ndiyo aende Tunduma, atakuwa amezidisha zaidi ya kilomita 150.
Mheshimiwa Spika, tunataka tuisaidie nchi hii na Bunge lako Tukufu, na Mheshimiwa Rais wetu, dhamira yake hii njema. Tunaomba sana Mawaziri wa Wizara hii na Waziri wa Fedha asaidie kuwalipa hawa wakandarasi ambao wako nchi nzima. Kila Mbunge anayechangia hapa kuna sehemu ime-stuck.
Mheshimiwa Spika, tunajua kweli tulikuwa na malengo mazuri. Baadhi ya maeneo tulitakiwa tuyamalizie, lakini tulipomaliza, basi tuangalie namna ya kukwamua hii miradi ambayo imekwama, miradi muhimu sana. Zile kilometa 25 Mheshimiwa Ulega akimlipa huyu mkandarasi, akirudi site, muda mfupi sana atakuwa ameshamaliza ataendelea na zile kilometa nyingine 31 tulizomwongezea juzi, point sita ambazo Mheshimiwa Rais alikuja pale na akaona namna ambayo wananchi wa Itigi na Mkoa wa Singida walivyo na dhamira nzuri ya kuunganishwa na wenzao.
Mheshimiwa Spika, barabara hii pia ina changamoto ya upitaji, yaani imeharibika mno baada ya mkandarasi kusimama. Zile diversions ambazo alitengeneza, hazirekebishiki na watu wanapita kwa tabu sana, lakini vipande ambavyo havina mkandarasi pia, Meneja wa Mkoa kila ukimwuliza inaonesha naye ana tatizo hili hili la kwamba, hana fedha ya kufanya matengenezo ya dharura.
Mheshimiwa Spika, kipande cha kutoka Lulanga kwenda Itagata kuna sehemu ambayo mvua ikinyesha, kama haya manyunyu yaliyonyesha jana Dodoma hapa, basi tena hatuwezi kupita. Naiomba Serikali isaidie. Kuna maeneo mengi barabara hii ambayo ni mazuri, kwa mfano, ukitoka Kintanula kwenda Mwamagembe ni pazuri, lakini kutoka Rungwa kuja Kintanula pana changamoto. Tunaomba sana Serikali itusaidie kumrudisha mkandarasi barabarani.
Mheshimiwa Spika, vilevile yuko mkandarasi anasimamiwa na Wizara hii ya TANROADS pale Itigi, kilometa 10. Naye tunaomba aongezewe fedha kidogo anazodai ili amalizie, na kuna taa zetu za barabarani.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja, lakini tusaidie Mkandarasi yule arudi wa Tronic pale Itigi na CHICO...
SPIKA: Umeshasikika Mheshimiwa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: ...tutafaidika sana watu wa Itigi na tutafurahi tunapoelekea katika uchaguzi. Ahsante sana. (Makofi)