Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii tena ya kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi aliyonipatia kusimama tena mbele ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa bajeti ambayo nilikuwa naangalia tu zile za maendeleo. Ukifungua ukurasa Namba 16, utagundua kwamba, Bajeti ya Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ilikuwa karibu shilingi trilioni 1.7 hivi, lakini mwaka 2025/2026 Bajeti ya Maendeleo imeshakwenda kuwa takribani shilingi trilioni 2.1. Ukiangalia ongezeko lake, ni karibu 22.94%. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo sasa inaonekana kuna ongezeko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nawapongeza sana wataalam kwa sababu, wao ndio wachakataji wa shughuli hii; Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na wataalam wengine kwa namna ambavyo wamefanya kazi kubwa katika bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda ukurasa wa tano, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, kuna miradi hapo inaoneshwa, ambayo inatuunganisha sisi kama nchi na nchi nyingine, maana yake ni miradi ya Kimataifa. Utaona kabisa kuna miradi, kama Mradi wa Tanzania na Malawi kupitia Barabara ya Mpemba – Isongole, kilomita 50.3. Kwa hiyo, ina maana kazi hii inayofanyika na TANROADS tayari imeshatuhusianisha sisi na Mataifa mengine.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia tena ukurasa huo huo utaona kuna Tanzania na DRC kupitia Barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga Port, kilomita 107. Hii ni kazi kubwa ambayo inaonesha wazi kwamba siyo diplomasia tu, namna tunavyoweza kuwasiliana na wenzetu katika kufanya shughuli hizi. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam kwa kazi kubwa ambayo wamekuja nayo hapa.

Mheshimiwa Spika, vilevile iko miradi mingi katika ukurasa huo ya Kitaifa, ambayo inaonekana kwamba, kuna kuunganika mkoa na mkoa. Kuna mahali imeunganishwa wilaya na wilaya, kuna kazi kubwa inafanyika. Changamoto kubwa tu ambayo nimeiona, pamoja na ongezeko hili, inaonekana mpaka Aprili, 2025, Bajeti ya Maendeleo ambayo ilipangwa kutolewa na Serikali imeshatolewa kwa asilimia kama 90.9, lakini utaona kuna miradi mingine bado haiendi kwa kasi sana.

Mheshimiwa Spika, maana yake, kuna dharura nyingi katikati humu na bajeti yetu haiingii kule inakotakiwa kuingia. Kwa hiyo, naomba sana, dharura hizi sijajua tutazifanyaje, lakini inaonekana zinaingia mahali na watu wetu inawezekana wanachelewa au hawalipwi kama ilivyokuwa imekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimboni Busanda, hii ya Kitaifa ambayo iko huku ndani, asubuhi nilikuwa nauliza Swali Na. 232, niliuliza kabisa barabara yetu kutoka pale Geita kwenda Iloge kupitia Bukole na Nyarugusu, lakini nimeona hapa Ukurasa Namba 28 imeshaoneshwa pale, imeandikwa wazi kwamba ni mpango wa Serikali hii barabara iwe imesainiwa mwisho wa mwezi Mei.

Mheshimiwa Spika, mwezi Mei ndiyo huu, Nawaomba sana Wizara kwa sababu, maandishi yale najua hatutayabadilisha. Mwisho wa mwezi Mei huu tukaone kinachofanyika, kusaini ili barabara hii iweze kutengenezwa kwa sababu, inapita kwenye miradi mingi ya migodi ambayo italeta faida ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile asubuhi hiyo tu nilisema, barabara yetu ya kutoka Ushirombo T3 kuja Katoro kwenye Barabara ya T4 kuna changamoto hapa, kipande kile cha kutoka Nyikonga kuja Katoro kinaonekana maelezo yake ya fedha hayakunyooka sana. Hivyo, ukimwuliza mtu kwamba, ni kiasi gani cha fedha hapa? Kitatoka wapi? Atakueleza tu fedha itakapopatikana, lakini Barabara imeshaingia kwenye bajeti. Niombe sana, hii iwe defined, ili kusudi Barabara hii ipate nafasi ya kwenda kutengenezwa.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, tumesema wazi kwenye kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ibara Namba 55 (C - G) inaongelea habari ya madaraja. Haya madaraja tayari sisi tunayo Kanda ya Ziwa, Daraja la Kigongo - Busisi. Jana nimesikia linaombewa libadilishiwe jina, lakini Kigongo - Busisi liko zaidi ya 99%.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme wazi kwamba, kuna kazi kubwa imefanyika ambayo inaonekana na ninaamini yako madaraja mengine inawezekana nisiyataje hapa, lakini kuna kazi kubwa imefanyika kwenye Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba, wananchi wetu wanapata maendeleo.

Mheshimiwa Spika, ninaamini, kama bajeti hii tuliyoomba sasa tutaisimamia vizuri, tukahakikisha kwamba kila mmoja anakaa mahali pake na kufanya kazi yake vizuri, utekelezaji wa bajeti hii utakuwa mzuri na nchi yetu itaendelea kupitika.

Mheshimiwa Spika, wote tunajua mvua inayoendelea kunyesha nchini kwetu hapa, kwa hiyo, barabara nyingi sana zimeharibika. Niwaombe sana ndugu zangu wa Wizarani, ndugu zangu wa TANROADS, akiwemo Meneja wangu Mhandisi Ezra Magogo kuhakikisha kwamba kazi hii, mvua inyeshe, lakini wananchi wetu wanafanya shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)