Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Innocent Edward Kalogeris

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu ya Wizara ya Ujenzi. Nitumie nafasi hii, nami, kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia, lakini kubwa zaidi kukupongeza kwa kazi kubwa ambayo umeifanya katika kuendesha Bunge katika kipindi hiki cha uhai wake ambapo tunaelekea mwisho kufikia tarehe 27.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya kuboresha miundombinu katika nchi hii. Vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, mdogo wangu Ulega, pamoja na Mheshimiwa Eng. Kasekenya, Naibu wake, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa taasisi ambazo chini ya Wizara, TANROADS, TBA, TAMESA, Bodi ya Mfuko wa Barabara na nyingine zote kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kusimamia miundombinu katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pongezi zangu za dhati zimwendee Mheshimiwa Rais kwa utayari wa yeye kuona kwamba, Barabara ya Bigwa – Kisaki inajengwa kwa kiwango cha lami, Barabara ya Ubena – Zomozi – Ngerengere tayari nayo inajengwa kwa kiwango cha lami pamoja na kufanya upembuzi yakinifu kutoka Ngerengere kwenda Mvuha – Kisaki hadi Matemele Junction kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere na vilevile kwenye Hifadhi kubwa ya Mwalimu Nyerere. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais katika hilo, mimi na mdogo wangu Mheshimiwa Tale.

Mheshimiwa Spika, wamepita Wabunge wengi na kati ya Wabunge waliopita alikuwepo mpaka Naibu Waziri wa Ujenzi, kaka yangu Mheshimiwa Hamza Mwenegoha. Barabara ilikuwa haijajengwa, lakini kwa kitendo cha tarehe 7/2/2024 Mkandarasi wa Chinese Railways ameweza kusaini mkataba wa shilingi bilioni 132.4 kujenga kwa kiwango cha lami kutoka Morogoro kwenda mpaka Mvuha, kilomita 78. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais na kujipongeza sisi wenyewe Wabunge kwa kazi kubwa ambayo tumeifanya na hatimaye mkataba ukasainiwa.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Mheshimiwa Ulega, aliniambia katika kipindi kile tunaingia kwenye kipindi cha Kamati kwamba, fedha yote ya kwanza itakayopatikana ataipeleka kule, ili mkandarasi aanze kazi Wanamorogoro Kusini, Wanamorogoro Kusini Mashariki nao waone matunda ya uhuru kwa kupata barabara ya lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa Barabara ya Ubena – Zomoni, tayari imeishaanza. Mkandarasi kapewa advance payment na kazi inafanyika. Kwa hiyo, ni kielelezo tosha kwamba, tutafika Kisaki maana yake tunakwenda Ngerengere, lakini Ngerengere upembuzi yakinifu na nimeona kwenye kitabu cha bajeti kuna fedha nyingine zimetumbukizwa ili kazi hiyo ikamilike, tujue tathmini na tujue thamani ya mradi. Naamini katika Bunge lijalo tutafika Kisaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nampongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kwa Barabara ya Bigwa – Kisaki, kipande cha Morogoro mpaka Mvuha, kukabidhiwa mkandarasi, maana ilikuwa TANROADS hawezi kufanya kazi yoyote, lakini nilimwomba kwa hali iliyokuwepo na kaweza kutoa fedha. Mkandarasi amefanya kazi nzuri na sasa hivi kutoka Morogoro mpaka Mvuha japo tunatembea kwenye vumbi, lakini tunaweza kwenda kwa kasi.

Mheshimiwa Spika, Ombi langu tu kwa TANROADS hebu wahakikishe kwamba, tunaendelea kuboresha Barabara kutoka Mvuha mpaka kwenda Kisaki maana yake ni kama pale kuna mahali panaitwa Kisalike, barabara ni mbaya sana, wananchi wetu wanapata adha. Kwa hiyo, naomba tu TANROADS watukamilishie kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo ningependa kuchangia ni kwenye suala la Mfuko wa Barabara. Kelele zote ambazo zinapigika humu ndani ya Bunge ni kwamba, TANROADS hawana fedha. Hata TARURA hawana fedha, lakini Bunge limetenga fedha kwenye mafuta, ambayo ni kwa ajili ya kwenda kufanya kazi za Barabara.

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu. Kamati katika ushauri wetu tumetoa kutoka Januari, 2024 hadi Februari fedha ambazo zimekusanywa, zilikuwa ni shilingi bilioni 919 na point, lakini hadi kufikia mwezi Februari fedha ambazo zimetoka Hazina kwenda kwenye Mfuko wa Barabara ni shilingi bilioni 289 tu, shilingi bilioni 530 badi ziko Hazina. Nini kielelezo chake?
Mheshimiwa Spika, ni kwamba, tunawapa wakati mgumu Wizara ya Ujenzi kuweza kufanya kazi za barabara wakati fedha hiyo ingepelekwa, ingefanya kazi kubwa na matokeo yangeonekana. Mvua nyingi zimepiga, fedha ambazo ziko ringfenced kisheria zinaendeleaje kubaki kwenye Hazina?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, atoe fedha hiyo ampelekee mdogo wangu Mheshimiwa Ulega akafanye kazi. Kule ndugu yangu alivyoingia alikuwa kijana mdogo, lakini leo ukimwangalia, kachoka kwa sababu, wanaumiza vichwa, fedha hakuna, wanakuwa wazee. Hebu pelekeni fedha hiyo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya, ahsante sana, muda wako umekwisha.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, umekwisha! Ooh, nadhani inatosha, lakini ujumbe umekwenda. Naunga mkono hoja. (Makofi)