Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, nami nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ambaye ameniwezesha jioni ya leo kuwa katika ukumbi huu na kuchangia Bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi. Pia, naomba nimpongeze sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuboresha miundombinu ya nchi yetu bila kumsahau Waziri mwenye dhamana, ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, Naibu wake na Ofisi nzima ya Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijielekeze moja kwa moja katika jimbo langu. Rais wetu wa Awamu ya Nne, Marehemu Dkt. Mkapa alitoa ahadi ya kujenga Barabara ya lami kutoka Nangoma hadi Nayumbu. Barabara hii imeanza kujengwa, lakini kwa kiwango cha chini sana, rate yake ni ndogo mno.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada zinazofanywa na Mkoa wa Mtwara, chini ya Eng. Dotto, naiomba Wizara iongeze kiwango cha lami ambacho kinatakiwa kijengwe kila mwaka. Nimeangalia katika bajeti ya mwaka 2025 sijaona ni kiwango gani cha lami kitaendelea kujengwa katika Barabara ya kutoka Nangomba hadi Nanyumbu.
Mheshimiwa Spika, naomba Wizara iangalie barabara hii ambayo ilikuwa ni ahadi ya mzee wetu, na ingekuwa bora kabisa ikamalizika. Barabara hii inakwenda sambamba na uwekeji wa taa za barabarani.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri katika bajeti yake ameongea kwamba anazo taa za kutosha na kwamba miji yote itawekewa taa. Sasa hii ni barabara ambayo imeanza kujengwa, na sasa hivi ina kilometa kama sita, lakini haina taa hata moja. Ni matarajio yangu kwamba atakapohitimisha hotuba yake atatoa neno.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, pia tuliomba Wizara ichukue barabara ya kutoka Mangaka – Sengenya – Matekwe ihamishwe kutoka TARURA kwenda TANROADS. Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu swali langu, alikubali ombi hilo na kwamba barabara hiyo ingechukuliwa. Nimeiangalia katika hotuba yake sijaona barabara hiyo.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu kwamba atasema neno, kwamba ni lini barabara hii itachukuliwa na TANROADS; kwa sababu TARURA kiwango cha fedha wanachokipata ni kidogo na matengenezo yake ni ya chini sana. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri afanye hilo jambo.
Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusu taa za barabarani. Sisi pale tulipata mradi wa kuwekewa taa za barabarani, lakini mkandarasi ameshindwa kuendelea na zoezi hili kwa sababu hajalipwa. Kuna mkandarasi pale anaitwa Shibesh amefanya kazi hiyo pale Nanyumbu, na Mangaka Mjini, lakini ameshindwa kumaliza kwa sababu hajalipwa fedha zake na hiyo kazi hajaimalizia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Wizara itueleze ni lini mkandarasi huyu atalipwa fedha ili aweze kumalizia uwekaji wa taa za barabarani katika Mji wetu wa Mangaka ambayo ndiyo Makao Makuu ya Wilaya ya Nanyumbu.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, naomba tena nichukue nafasi hii kuipongeza sana Wizara na kumpongeza sana Engineer wangu wa Mkoa wa Mtwara ndugu yangu Doto kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuhakikisha kwamba miundombinu yetu inaboreshwa.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)