Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyoko Mezani. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuishi hadi leo. Pia nashukuru kwa ushirikiano mkubwa ninaoupata kutoka kwa wananchi wa Urambo na familia yangu.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Ulega; Naibu wake, Engineer Kasekenya; Katibu Kkuu wake, Aisha Amour; na Naibu wake, Dkt. Charles Msonde na Watendaji wote wa Wizara ya Ujenzi. Kwa kweli Wizara ina kazi kubwa sana, lakini kwa jinsi Mheshimiwa alivyowateua, wao wana uwezo mkubwa na watazikabili shughuli zote ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutusaidia miradi mikubwa sana Urambo. Kwa sababu ya muda nitaitaja michache tu, maji kutoka Lake Victoria ambayo yameshakaribia kujaa sasa. Pia, kituo cha kupozea umeme ambapo tulipata Bahati Jumamosi iliyopita; Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati alifika akatoa baraka zake, sasa hivi tunapata umeme moja kwa moja. Tunamshukuru sana Dkt. Samia.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuishukuru Wizara ya ujenzi kwa kutupa miradi miwili mikubwa ambapo nashukuru kwamba Serikali inatujali sisi watu wa Urambo. Kwanza ni barabara inayopita katikati ya Urambo kwenda Ulyanhulu, inapita katikati ya soko la ndizi. Soko la ndizi ni kubwa sana na lina watu wengi sana, tena akina mama ndio wengi zaidi. Wameipandisha ile barabara. Ilikuwa TARURA, sasa hivi imekuwa ya TANROADS.

Mheshimiwa Spika, ombi langu ni kwamba ile barabara ifanyiwe haraka sana kwenye kazi ya kuweka alama kwa sababu inapita katikati ya soko, halafu iwekewe taa, sasa hivi haina taa. Tunaomba taa ili kunusuru maisha ya watu. Nawaomba Wizara ya Ujenzi waongeze fedha za marekebisho ya alama za barabarani. Yaani kuweka alama ili watu waweze kupona na ajali.

Mheshimiwa Spika, pia, naishukuru Serikali kwa kutupa Barabara ya Tutuo – Usoke au Usoke – Tutuo, maana ni kwamba sasa wanatufungulia mlango. Nimeona katika miradi ya mwaka huu 2025/2026 wameuweka katika kikundi ambacho kitapata usanifu. Kwa hiyo, barabara hii itafanyiwa usanifu. Naiomba sana Wizara ya Ujenzi, hii ni barabara ambayo itatufungulia milango ya magari mengi kutoka Kahama kwenda Sikonge - Tutuo hadi Mbeya. Kwa hiyo, tunaomba iwekewe fedha za kutosha.

Mheshimiwa Spika, la tatu napenda kuwaomba Wizara ya Ujenzi kwa heshima na taadhima watusaidie kuweka taa. Barabara ya Kigoma inapita Urambo, inakuja huku mbele, ina maeneo mengi ambayo ajali ni nyingi.

Mheshimiwa Spika, nitaje maeneo ambayo tunahitaji kuwekewa alama, ikiwemo Vumilia, naomba taa na alama; pia, Mbaoni, Kona ya kuingia stendi ya mabasi na barabara inayotoka Polisi kuja kuungana na Barabara ya Kigoma nayo iwekewe taa na alama kwa sababu ajali zinakuwa ni nyingi sana. Halafu na maeneo ya Kona ya Polisi ambayo inajulikana kama ni eneo la Kasu, tunaomba nalo liwekewe alama na taa. Vilevile, Maili Nne, Katuli, Kona ya Usoke na Tutuo nazo ziwekewe alama.
Mheshimiwa Spika, maeneo mengi haya niliyoyataja naomba Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Naibu wake wayachukue ili wayawekee taa kwa sababu tumepata ajali nyingi sana. Hata juzi tu walifariki watu wawili kutokana na kwamba wanavuka wanatoka kwenye barabara ndogo wanaingia kwenye barabara kubwa ya Kigoma, inatuletea matatizo sana.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika, barabara inayotoka Kigoma inapokata kona ikitoka Kigoma inakata kona mkono wa kushoto kuingia Urambo Mjini nayo imeleta ajali nyingi sana. Kwa hiyo, naomba maeneo haya yafanyiwe kazi ili kweli tuone nia ya Serikali ya kuokoa maisha ya wananchi wa Urambo.

Mheshimiwa Spika, vilevile, nilikuwa nafikiria kwamba kukaa na barabara ambazo hazina alama ni hatari sana. Naomba, na tena ninarudia kuwaomba, kwamba waweke fedha za kutosha ili zisaidie kuokoa maisha ya watu kwa kuweka alama.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Engineer wetu wa TANROADS wa mkoa, Engineer Mlimaji, anafanya kazi kubwa sana na anashirikiana na sisi. Kwa hiyo, tunamwombea kila la heri na afuatilie hii miradi tukiamini kwamba barabara ndizo zinazofungua maeneo na kuletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, narudia kumwomba tena Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, nina imani naye, kwamba barabara ile inayopita katikati ya soko iwekewe taa na alama haraka iwezekanavyo, halafu kila mwaka wawe wanaongeza kilometa moja kwa sababu ndiyo inayokwenda kuunganisha Ulyanhulu. Tunaomba iongezewe badala ya kilometa moja, basi angalau ziwe mbili kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, ukichukua kilometa moja kila mwaka na ni kilometa 59, si itachukua miaka hamsini na ngapi, na wengine tutakuwa tumeshakwenda Mbinguni! Kwa hiyo, tusaidiwe basi barabara ile iongezewe kilometa, ahsante sana. (Makofi).

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya, ahsante sana.

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nawatakia kila la heri na ninaunga mkono hoja. (Makofi)