Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami nimshukuru Mungu kwa fursa ambayo nimeipata leo ya kuchangia Wizara hii. Nawapongeza Wizara na Serikali yote kwa ujumla kwa namna ambavyo dira ya Wizara imeweza kutekelezwa vizuri, ambapo inazungumzia habari ya kuwa na miundombinu endelevu itakayochochea maendeleo ya kijamii pamoja na kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii imefanya kazi kubwa hasa katika kuunganisha mikoa. Madaraja na kila miundombinu iliyotakiwa imeweza kujengwa. Tunawapongeza sana, kazi hiyo ni kubwa sana. Tunawapongeza kwa sababu ni mafanikio makubwa katika kukuza na kuchochea uchumi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ninalo jambo moja dogo na la msingi sana kuhusiana na suala zima la barabara zinazotolewa kwa wakandarasi kwa ajili ya ujenzi. Nitolee mfano tu katika Mkoa wa Mwanza, nilikuwa ninajaribu kupitia kwenye wilaya, nilifikiri labda ni kwangu tu peke yake, kwamba barabara ambazo zinatolewa hazikamiliki. Hizi barabara nitakazozitaja zote ni za mweaka 2023/2024. Airport Igombe – Kayenze kilometa 46 amepewa mkandarasi kilometa 10 toka 2023/2024 lakini mpaka leo hakuna hata kilometa moja imejengwa na mkandarasi hajafika site.

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Nyakato – Steel VETA mpaka Igombe imeanza 2017, kilometa 18 mpaka leo haijatimia. Kwenye hii taarifa, wanaonyesha kuna upembuzi yakinifu umekamilika kwa kilometa tatu zinazozungumzia suala la Nyakato – VETA – Busweru, eneo ambalo tayari limeshajengwa. Kule ambako hakujajengwa, nadhani wamepitiwa katika kuweka taarifa hizo. Ni mbele kule Shibula kwenda TX ndiko ambako hakujajengwa.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nataka kulizungumzia ni Barabara ya Isandula – Magu – Ngudu kilometa 50, ujenzi ni kilometa 10 na kazi bado. Mwanangwa – Misasi – Salawe inaunganisha katika Wilaya ya Kahama kilometa 150, ujenzi ni kilometa tatu, lakini ujenzi huo bado. Ngudu – Jojilo – Mabuki, kilometa 28, ujenzi ni kilometa tatu. Kamanga – Katunguru – Sengerema kilometa 32, ujenzi ni kilometa tatu. Nansio – Rugezi kilometa 11, ujenzi ni kilometa saba.

Mheshimiwa Spika, natoa masikitiko kwa sababu barabara zote hizi zinaunganisha maeneo ambayo uchumi wa Jiji la Mwanza ndiko unakotoka, kwa sababu ni lazima waingie majini kuleta mazao yao. Sasa, kama barabara hizi hazikamiliki lengo la kuchochea uchumi katika jamii linakuwa pia halijafikiwa sana.

Mheshimiwa Spika, naomba sana, kandarasi hizi zimekaa muda mrefu na siyo kwa Mwanza tu, ni almost kwa nchi nzima. Mimi nimechukulia sample kwa Mwanza kwa sababu kila Mbunge anayesimama analalamika. Kwa hiyo, naomba sana kazi inayofanyika ni kubwa na nzuri. Tumwombe Mungu tusipate tena madhila ya pengine kuwa na mvua nyingi ambazo zinaharibu barabara halafu unakuta bajeti inalegea katika eneo moja. Kwa hiyo, naomba sana katika hili tuangalie ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza kwenda.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa kuwajali wakandarasi wazawa ambao tulikuwa tumeambiwa hapa; kwenye zabuni ambazo wamepewa za thamani ya shilingi bilioni 50 bado ni kidogo kwa sababu hawa wana uwezo mkubwa na wanaweza kufanya kazi kama watapewa. Wanaonekana goi goi pale ambapo fedha inakuwa haitoki, naye pale pale anakuwa anashindwa kukataa kazi. Amepewa kazi anaipokea na hawezi kupata fedha, na matokeo yake unakuta wanapata portion ndogo katika keki kubwa ya Taifa. Lengo letu au lengo la Serikali ni kuwaimarisha hawa waweze pia kuwa wakandarasi wakubwa na waweze kufanya kazi zetu kwa uzuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia Daraja la Busisi – Sengerema ambalo Mbunge ameomba liitwe hivyo, daraja hili linakwenda kuchochea uchumi mzuri katika maeneo hayo, lakini kutoka pale, ukishavuka, ukitaka kwenda maeneo mengine huwezi kufika kwa sababu barabara hazijatengenezwa. Ukitaka kwenda Buyagu uende mpaka kule Msalala kwa wakwe zangu bado pia ni changamoto. Kwa hiyo, naomba sana, tunapounganisha miundombinu, tuangalie pia kule kwenye source ya uchumi ambako kuna wazalishaji mali wengi ambao wanatakiwa pia mizigo yao iweze kufika katika maeneo.

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Wizara. Mheshimiwa Ulega mjukuu wangu pamoja na Engineer Kasekenya, kazi wanayoifanya ni kubwa. Ombi langu, kama fedha ni kidogo zisitolewe kazi nyingi. Tutoe hizo zilizopo zikamilike. Tunaacha viporo vingi matokeo yake wananchi wanalalamika, pia, malipo yanachelewa. Kwa hiyo, twende kulingana na bajeti, tunamaliza hili na tukilianza basi tulimalize. Kilometa 50 unatoa kilometa tatu na 150 unatoa kilometa tatu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Haya, ahsante sana.

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)