Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Stella Simon Fiyao

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara hii ya Ujenzi, Wizara ambayo ni muhimu sana na inayotegemewa kwa asilimia kubwa sana na wananchi wote wa chini, masikini, na matajiri, wote wanaitegemea Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa na mambo machache kutokana na muda. Jambo la kwanza nitaomba nizungumzie Barabara ya Igawa – Tunduma. Sote tunajua umuhimu mkubwa wa barabara hii. Zaidi ya 73% ya mizigo inayopitia katika Bandari ya Dar es Salaam inakwenda kupita katika mpaka wa Tunduma, kwa kuwa mizigo mingi inapita inakwenda huko nchi za SADC, kwa hiyo, barabara hii ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, barabara hii imekuwa kuna changamoto sana. Wananchi wanajua kwamba barabara hii inachangia kwa asilimia kubwa kwenye pato la Taifa lakini changamoto ambazo tumekuwa tukikabiliana nazo wananchi tunafika mahali tunafikiri kwamba hivi Serikali wanakiona hasa kile kinachoendelea Tunduma au hawaoni? Kama wanaona, je, ni hatua gani za haraka na za dharura ambazo wanazichukua ili kutunusuru wananchi wa Mji wa Tunduma? Hali siyo nzuri kwa kweli. Tunayasema haya huku tunafikiri kwamba hivi kwenye hii Wizara hakuna fedha za dharura za kuweza kutusaidia pale Tunduma?

Mheshimiwa Spika, mlundikano mkubwa wa magari uliopo Tunduma kwa kweli ni hatari. Siyo magari ya mizigo tu, yako magari ya mafuta ambayo nayo yanakaa kwenye foleni pale zaidi ya masaa, kitu ambacho pia ni hatari na kinaweza kuhatarisha hata mazingira. Serikali hebu walione hili.

Mheshimiwa Spika, sisi tunajua umuhimu wa barabara hii, lakini tuone, wanakuja na mpango wa haraka. Hata kama barabara hii wameiingiza kwenye PPP, lakini ukweli ni kwamba changamoto ni kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, tunajua jitihada kubwa ambazo anazifanya Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kwamba anafungua uchumi wa nchi yetu, lakini watuone kwa jicho la namna ya pekee kabisa, watuangalie Tunduma, hali siyo nzuri. Kuna umuhimu mkubwa wa kutengeneza barabara nne ili kunusuru maisha ya Wanatunduma na ili kuokoa muda. Jamani tusaidieni, yaani wakati tunasimama kuzungumza mara mbili mbili hapa kwa habari ya Mji wa Tunduma, lakini sisi tunaoishi pale tunaona.

Mheshimiwa Spika, unajua kuna wakati nafikiri Mawaziri hata wakija pale huwa ule msongamano wanau-balance. Kwa hiyo, hawaoni adha ambayo wananchi wa Mji wa Tunduma tunakutana nayo. Natamani siku moja wakija, mahali ambapo wanaweza kutumia dakika tano wakitumia masaa matano pengine wanaweza kufikirifikiri namna ya kutusaidia Wanatunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatusemi tunayakataa yale malori, tunayakubali kwa sababu ni sehemu ya kuchochea uchumi wetu, lakini je, wanatuchukuliaje na wanatuweka kwenye mazingira gani wananchi wanaoishi kwenye ule mji? Serikali waone namna ya kutusaidia ili kutunusuru na ile adha ya foleni ambayo imekuwa ni too much. Hali siyo nzuri. Mahali pa dakika tano unatumia masaa Matano. Wao wakija wana nafuu.

Mheshimiwa Spika, nimesema hapa, mawaziri wakija pale huwa panakuwa balanced, wanapata namna nzuri ya kupita, lakini wanaweza kufikiria kuhusu wananchi ambao wanaamka na kulala pale? Ile hali ikoje? Kwamba wameshindwa kustusaidia! Watusaidie basi walau njia nne zianzie Tunduma au hata Chimbuya, pengine wanaweza kutupunguzia ile adha ambayo tunakutana nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waangalie basi, kwani ni kilometa ngapi? Mpaka ule unaingiza kiasi gani cha fedha? Mbona ni mamilioni ya fedha yanaingia kupitia ule mpaka. Namna gani wanashindwa kutusaidia? Kutoka custom kuelekea Chimbuya tu, yaani kwa kuanzia tu ili watutie moyo tujue kwamba Serikali wanaliona lile ambalo linaendelea pale Tunduma. Watutie moyo hata kwa kilometa 10 ama 20 watakuwa wametusaidia na Tunduma tutajua Serikali wanathamini uwepo wa ule mpaka...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, tunaomba watusaidie kuepukana na ile adha ya mlundikano wa magari kwa kututengenezea njia nne ambazo pengine basi zianze tu pale pale. Tumesema yaani walau kwa kututia moyo...

SPIKA: Mheshimiwa Stella, ahsante sana.

MHE. STELLA S. FIYAO: ...zianze pale Custom ziishie hata Chimbuya halafu ndipo waendelee na huko kwingine. Muda wangu umekwisha?

SPIKA: Umekwisha.

MHE. STELLA S. FIYAO: Aah, hii ni hatari. Nashukuru.