Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoitendea haki nchi hii. Vilevile namshukuru na nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kama Mtendaji Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, pongezi zangu za pili zinakwenda kwa Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Ulega na msaidizi wake, mate wangu, Mheshimiwa Engineer Kasekenya na bila kumsahau Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mohamed Besta, kuruta mwenzangu, Operation Programme ya Chama, Ruvu JKT. Vilevile, nampongeza Mtendaji Mkuu wa Wizara hii dada yangu Aisha.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kuziongelea barabara kuu mbili zinazoingia Liwale. Barabara ya Nangurukuru – Liwale na Nachingwea – Masasi – Liwale. Hapa niweke rekodi sawasawa. Barabara hii ya Nachingwea – Masasi – Liwale upembuzi yakinifu ulikamilika mwaka 2014. Barabara hii kama ingejengwa kipindi kile, maana yake leo ingekuwa ni miongoni mwa barabara zile za kufanyiwa service.
Mheshimiwa Spika, vilevile, kumbukumbu hizo zisipotee, barabara hizi ninazozungumzia, zimezungumziwa kwenye bajeti zote nilizokuwepo katika Bunge hili. Tangu wakati wa Mheshimiwa Eng. Kamwelwe, akaja Mheshimiwa Engineer Dkt. Chamuriho, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Mheshimiwa Bashungwa na leo Mheshimiwa Ulega. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana barabara hizi zijengwe, na nasema muda wote, barabara hizi zilikuwa zinatengewa fedha lakini fedha haziji. Kwa mwaka huu nina imani Mheshimiwa Ulega barabara hii anakwenda kuijenga. Imani yangu inanipa, kwa sababu yeye ni mtoto wa Mhuba na mimi ni mtoto wa binti Mhuba hivyo hivyo. Kwa hiyo, yeye ni wa nyumbani.
Mheshimiwa Spika, naomba sana impendeze barabara hii mwaka huu ijengwe. Nimeiona kuna kilometa 72 Nanguruku – Liwale; kilometa 55 Nachingwea – Liwale. Basi ninaomba sana barabara hizi mbili zijengwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanapobandua lami au wanapopanua barabara huwa ninachukulia mfano kama vile mama anamwambia mwanaye, usile huu ugali wa jana umechacha, kwa hiyo, anamtafutia ugali mpya ampe; lakini kwenye nyumba hiyo hiyo, boma hilo hilo yuko mtoto wa mama mkubwa, mama mdogo hajala.
Mheshimiwa Spika, naomba busara iwatume kumpatia chakula yule mtoto ambaye tangu jana hajala, badala ya kumpa huyu ambaye jana amekula ila sasa unaogopa leo asile hiki chakula kimechacha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maana yangu ni nini? Ni kwamba barabara sasa, maana kuna watu wengine hapa wanaomba taa za barabarani, wengine hapa wanaomba barabara zipanuliwe, mimi kule kwangu naomba barabara ili ziweze kupitika, wananchi wale waweze kufaidi matunda ya nchi hii na mazao ya wakulima yaweze kufika kwenye masoko. Mheshimiwa Ulega niliomba tu dakika tano niyasema hayo.
Mheshimiwa Spika, juzi Mwenezi Taifa alikuja Liwale, mimi wakati wa kurudi, nikalala njiani, nimelala porini. Juzi nimejipendekeza hapa niende kwenye May day nimeingia leo hapa, nimelala njiani lakini jana ilikuwa nihudhurie hapa lakini nimelala porini, nimekuja Dar es Salaam leo asubuhi, nimeunganisha nipo Dodoma. Nikuombe sana, watu wanateseka.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)