Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Napenda nimshukuru Mungu kwa kunipa nafasi siku ya leo tena niweze kuongea kwenye hii Hotuba ya Wizara ya Ujenzi. Napenda niishukuru Serikali jinsi inavyopambana kuboresha nchi yetu, lakini muda hautoshi nilenge moja kwa moja kwenye hoja.
Mheshimiwa Spika, Waziri mpya ambaye ameteuliwa hivi karibuni sina cha kumshukuru, bali nina maombi. Barabara ya kutoka Katoro kwenda Ushirombo, naomba kwenye bajeti yake itengewe fedha iweze kufanyiwa ukarabati ikiwezekana iwekewe lami kabisa, maana ni barabara muhimu sana kwa watu wa Bukombe pamoja na Mbogwe.
Mheshimiwa Spika, ipo barabara ya kilometa 72 kutoka Kashero kupitia Mbogwe kwenda Lugunga mpaka Masumbwe. Nikisema hivyo, Naibu Waziri wa Ujenzi anaijua kwa sababu ni mwenyeji maeneo hayo. Hii barabara tunaomba iwekwe kwa kiwango cha lami maana hata kwenye ilani imeingizwa kwamba, ni barabara inayounganisha mkoa na wilaya.
Mheshimiwa Spika, suala la tatu, kuhusu taa za barabarani. Ninayo maeneo ambayo yanahitaji taa za barabarani, nina Mji wa Lulembela ni mji mkubwa sana, ni mji wa pili ukitoa Mji wa Masumbwe, Lulembela ni ya pili kwa wingi wa watu. Kwa hiyo, pale watu wa Lulembela wamenituma kuomba hapa kwamba taa za barabarani kama vile 100 hivi na kwenye hotuba imeelezwa kwamba, taa wanazo. Kwa hiyo, natamani mwezi wa kumi nifanye kampeni nikiwa kwenye taa za barabarani pale Lulembela. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine kutoka Kanegere mpaka Lubeho ni kilometa 20. Hii ni barabara kuu iendayo Congo kutoka Dar es Salaam. Nashukuru kwa yale matangenezo yanayofanyika, lakini yale maeneo yana wafanyabiashara wengi, tunahitaji taa za barabarani sasa kuanzia Kanegere kwenda Lubeho. Haya maeneo Mheshimiwa Kasekenya naomba Waziri anayafahamu, yawekewe taa za barabarani ili wafanyabiashara waweze kufanya biashara zao vizuri na kazi iendelee.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni madaraja. Kutoka Masumbwe kwenda Mwabomba kuna daraja kubwa pale Mheshimiwa Eng. Kasekenya analifahamu. Pamoja na kwamba, limetengewa bajeti, lakini mpaka sasa hivi halijaanza kutengenezwa na kila mvua zikianza kunyesha zile barabara huwa ni korofi sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naoimba Serikali haraka iwezekanavyo kabla hatujaingia kwenye nyakati zile ngumu za hatari, iweze kurekebishwa ili kusudi wananchi wa maeneo haya waweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ninaloliomba hapa, kuna Mji wa Segese kupitia Mbizi kuja Mpakali - Masumbwe Mjini. Naomba eneo hili lichukuliwe na TANROADS kutoka TARURA, hata kwenye vikao vya kimkoa nimeshalipendekeza, kwa sababu ni barabara muhimu ambayo inaingiza mapato mengi. Sasa ikichukuliwa na ninyi watu wakubwa wa TANROADS itakuwa inafanyiwa marekebisho ya kutosha, na uchumi wa maeneo ya Mbogwe utafunguka.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo lingine hapa ninalotaka niliombe ni stendi ya malori. Mji wa Masumbwe ni mkubwa, pale madereva wanapenda kila wakifika lazima wapumzike, magari yanapaki barabarani. Kwa hiyo, nyakati za usiku watu wanapofanya biashara zao, huwa wanapata shida sana, na ajali zinatokea nyingi. Tulishatenga eneo ili kusudi parking ya malori itengenezwe ili madereva hao wanapofika Mji wa Masumbwe waweke magari yao pazuri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wizara hii nilishaongea na Meneja wa Mkoa anajua. Kwa hiyo, haraka iwezekanavyo hiyo parking iweze kuboreshwa ili watu wanapokuwa wakisafiri kwenda nchi za nje, wakifika Mji wa Mbogwe Masumbwe wapumzike pazuri ili kusudi malori yakae pembeni yasikae barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, napenda kukushukuru wewe kadiri unavyotuendesha kwenye Bunge lako hili Tukufu. Hakika mama tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu, wala siyo unafiki unatutendea Wabunge, japokuwa unatupa muda huu ambao umepangwa kwa siku ya leo dakika tano tano, lakini tuna imani kwamba, ujumbe wetu unafika.
Mheshimiwa Spika, cha muhimu tu, tuiombe Serikali, haya mawazo tunayoyatoa hapa, yaani muda tunaoutumia huu mchache kuzungumza hapa, ni vitu muhimu ambavyo vinatakiwa na wananchi. Kama mnavyofahamu sisi ndio wawakilishi wa wananchi, hatuzungumzi maisha ya kwetu, hatuzungumzi mawazo yetu hapa, ndiyo maana nikasema nitampongeza Waziri sana haya niliyoyasema hapa machache kama atayafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa siku ya leo haipo sababu ya kushika Shilingi ya Waziri isipokuwa naomba tu haya niliyoyazungumza, ikiwemo taa za barabarani na madaraja akayaboreshe, na sasa atakuwa mtu bingwa sana Mheshimiwa Ulega. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Mungu akubariki sana. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Wabheja sana, wabheja sana.