Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nami nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa hii nafasi kuchangia. Kipekee namshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kule kwetu Manyoni. Namshukuru na nimpongeze ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, akiwa Wizara ya Mifugo alifanya mambo makubwa Manyoni, alitujengea mnada mmoja mkubwa sana, mkoa mzima uko pale.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, bila kumsahau DG wa TANROADS, lakini kule mkoani kwangu na Mheshimiwa Ulega aliniletea Meneja wa Mkoa Engineer Singano, anafanya kazi nzuri sana. Kwa kweli namshukuru na ninaomba asimtoe Singida, amepambana sana kule kwenye barabara korofi ambazo kisiasa zilikuwa hazijakaa vizuri, lakini sasa hivi anazitatua. Kwa hiyo, naomba asije akanitolea yule Meneja, tunaenda kwenye uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina maeneo mawili ningependa kuchangia Wizara ya Ujenzi, na kaka yangu, Mheshimiwa Ulega anajua daraja lake la Sanza. Siku hizi Naibu Waziri namwita Mzee wa Sanza kwa sababu kila siku anataja Daraja la Sanza kwenye maswali.
Mheshimiwa Spika, Daraja la Sanza lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi, ni Daraja la kimkakati, taarifa nyingi zinaonesha tayari mkandarasi alishapatikana, hatua iliyobaki na taarifa inasema ni kusaini mkataba.
Mheshimiwa Spika, sasa namwomba Mheshimiwa Ulega hebu hili Daraja la Sanza twende tukalikamilishe, mkandarasi asaini mkataba kwa sababu wananchi wanasubiri sana na Mheshimiwa Rais alienda Manyoni mwaka 2023, kwa kweli aliwaahidi wananchi na aliwapa matumaini kwamba, lazima Daraja la Sanza litajengwa. Kwa hiyo, hili mimi niliomba niweke msisitizo kwa hili Mheshimiwa Waziri Ulega Daraja la Sanza liwe kwenye priority zake kwenye huu mwaka ambao tunaenda.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili, Manyoni tuna kituo cha pamoja cha ukaguzi wa magari (One Stop Inspection Station) cha Muhalala. Hiki kituo kipo vilevile Nyakanazi Kagera Bukoba. Ujenzi wa hiki kituo ulisimama mwaka 2017/2018 na kilishafikia takribani 60%, cha Nyakanazi kilishafikia 50%.
Mheshimiwa Spika, wale ambao mnapita kuelekea Mwanza, kabla hujafika Manyoni pale Mlimani, kuna nyumba zipo pale zimejengwa. Sasa taarifa niliyonayo ni kwamba, Serikali imeshafanya jitihada nyingi sana kuhakikisha kwamba, inafufua huu mradi, na kwa kiufupi nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu huu mradi ulikuwa umetelekezwa, lakini kwa commitment ya Rais, mradi huu unaenda kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu ni kwamba huu mkataba upo kwa Attorney General (AG) kwa ajili ya upekuzi na taarifa yao inasema hivyo. Sasa ningeomba hili zoezi la upekuzi basi lisichukue muda mrefu kwa sababu tayari huu mradi umekaa muda mrefu haujakamilika.
Mheshimiwa Spika, huu mradi ni mzuri sana, utachochea sana uchumi wa Manyoni, vilevile, utaenda kukuza na kusaidia sana kwenye ukusanyaji wa mapato ya TRA, lakini unaenda kulinda barabara yetu hii ambayo kimsingi malori makubwa yanapita kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, huu Mradi wa Muhalala wa ukaguzi wa pamoja wa magari uwekee kipaumbele na fedha. Taarifa niliyonayo, fedha zipo, kwa sababu ni fedha za EU, tatizo tu ni kwamba, ni kufuata formalities za kumpata mkandarasi mwingine na tayari mkandarasi mwingine alishapatikana, ni suala la mkandarasi kusaini mkataba mwingine. Sasa hili sidhani kama linahitaji karne au decade, ni suala ambalo linaweza likafanyika within two weeks na mkandarasi akapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho nina maombi. Nimeona kwenye taarifa yao humu wameweka barabara ya Manyoni East – Heka – Sanza - Ikasi - Chali – Igongo - Bihawana Junction ya kilometa 192. Hii barabara ni ya kimkakati kwa sababu inalisha Mkoa wa Dodoma ambao kimsingi ni Makao Makuu. Vilevile, inaweza ikatumika kama diversion road inapotokea dharura kati ya Manyoni na Dodoma. Tayari imeshawekwa kwenye upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Mheshimiwa Waziri hii barabara naomba uiweke katika vipaumbele vyako, ni barabara ya kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara ya pili ni barabara ya kutoka Singida – Ikungi – Londoni - Kilimatinde takribani kilometa 117 nayo kwenye taarifa imewekwa kwamba, inafanyiwa upembuzi yakinifu. Hii ni barabara ya kimkakati ikitokea dharura kutoka Ikungi kuja Manyoni tunaweza tukatumia hii barabara ya kutoka Ikungi - Londoni – Solya - Kilimatinde kwa ajili ya kufika Dodoma. Kwa hiyo, ningeomba isiishie tu kuwekwa kwenye taarifa, lakini ningeomba ifanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)